Marekani na Uingereza zahoji uhalali wa mchakato wa uchaguzi huo wa mtaa na matokeo yake Tanzania

Wapiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa Tanzania
Maelezo ya picha, Wananchi wakisubiri kushiriki shughuli ya upigaji kura
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Mabalozi wa Marekani na Uingereza nchini Tanzania wameelezea kutoridhishwa kwao na jinsi uchaguzi wa serikali za mitaa ulivyoendeshwa nchini humo.

Uchaguzi huo ambao ulifanyika siku ya Jumapili, ulisusiwa na vyama vikuu vinane vya upinzani kwa madai kuwa uliingiliwa na serikali.

Chama Cha Mapinduzi, CCM kilishinda kwa zaidi ya asilimia tisini katika uchaguzi huo.

Katika taarifa Balozi hizo mbili zimetoa tamko la kuunga mkono misimamo yao kuhusiana na zoezi hilo.

Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.

''Serikali ya Marekani inasikitishwa sana na taarifa za ukiukwaji katika uchaguzi wa serikali za mitaa'', ilisema taarifa hiyo.

Pia balozi hizo ziliongeza kuwa wasimamizi wa uchaguzi huo waliwatenga kwa kiasi kikubwa wagombea kutoka vyama upinzani katika mchakato wa uchaguzi.

''Hali hii ya mkanganganyiko inazua swali kuhusu uhalali wa mchakato wa uchaguzi na matokeo.''

Wapiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa Tanzania tarehe 24 Novemba
Maelezo ya picha, Wapigakura wakihakiki majina yao kabla ya kupiga kura

Balozi hizo pia zimeikosoa serikali ya Tanzania kwa kutaa kutoa vibali kwa wakati kwa waangalizi wanaokubalika na mashirika.

Hali hiyo wanasema inapoteza imani zaidi kwa mchakato mzima.

Hata hivyo, Waziri wa Tawala za Mikoa wa Tanzania (Tamisemi) Selemani Jaffo ambaye ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa uchaguzi huo amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la nchini humo akisema: "...ninachojua uchaguzi ulikuwa wa haki na ulifanyika kwa mujibu wa kanuni na sheria za nchi..."

Zaidi ya 90%ya wagombea wa upinzani waliambiwa kuwa hawawezi kushiriki uchaguzi huo kutokana na makosa kama ya kukosea kuandika jina, kuacha nafasi katika fomi na masuala mengine yanayohusiana na kuwasilishaji wa stakabadhi zao.

Chama tawala kwa upande wake kinasema kuwa 99% ya wagombea wake katika uchaguzi huo waliidhinishwa.

Baada ya vyama vinane vya upinzani nchini Tanzania kususia uchaguzi wa serikali za mitaa, kiongozi wa chama cha upinzani cha TLC (Tanzania Labor Party) Tanzania Augustino Lyatonga Mrema aalisema kuwa ''walichezewa rafu na kufanyiwa figisu''.

Maelezo ya sauti, CCM na upinzani Tanzania walaumiana juu ya uchaguzi wa serikli za mitaa

Bwana Mrema aliambia BBC kuwa wakala wa chama chake waliondolewa kwenye vituo mbalimbali vya uchaguzi na hivyo chama chake hakikuwa na uwakilishi.

Wapinzani nchini Tanzania wanadai mchakato mzima wa uchaguzi huo uliofanyika Jumapili ulitawaliwa na udanganyifu uliotekelezwa na Chama tawala CCM kwa ushirikiano na maafisa wa uchaguzi.

Hata hivyo katika mahojiano na mwandishi wa BBC Sammy Awami, msemaji wa CCM Bwana Humphrey Polepole ameiambia BBC kuwa wapinzani wameshindwa vigezo na sifa na kukana madai kuwa serikali ina mpango wa kuwaondoa wapinzani katika uchaguzi mkuu ujao.

Vyombo vya habari Tanzania vyaonywa

Katika hatua nyengine, msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania Dr Hassan Abbas amevionya vyombo vya habari kwa kile alichokiita kuwa baadhi yao "kushabikia, kutumika na kuwa mawakala wa kusambaza habari za uongo, uzushi na propaganda dhidi ya nchi yetu kutoka mashirika ya kimataifa au wawakilishi wa mataifa ya nje."

Japo hakuyataja matamko ya Marekani na Uingereza, onyo la Dkt Abbas lilitoka baada ya balozi hizo kupaza sauti zao na baadhi ya vyombo vya habari kuchapisha matamko hayo.

Ruka X ujumbe, 1
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe, 1

"Vyombo vya habari; vya ndani na nje ya nchi vilivyosajiliwa, kupewa ruhusa ya kutekeleza majukumu yao hapa nchini vinakumbushwa tena kwamba uandishi wa habari ni taaluma; ina haki zake, wajibu wake, misingi yake na zaidi sheria zake. Sheria zilindwe, zisibanangwe," amesisitiza Abbas katika onyo lake alolichapisha kwenye mtandao wa Twitter.

Kauli hiyo ya Abbas imetafsiriwa na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini humo kama kitisho kwa wanahabari.

Zitto Kabwe, ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo (ambacho ni miongoni mwa waliosusia uchaguzi huo) alijibu kwa kupitia mtandao huo akisema ni "vitisho."

Ruka X ujumbe, 2
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe, 2