Roberto de Zerbi: Meneja wa Brighton anayelibadilisha soka

Iliyochapishwa

Pep Guardiola amefungua njia mpya ya uchezaji katika kipindi cha miaka 15 na kuathiri utamaduni wa soka kwa makocha wengine.

Lakini si wote walichukua mafundisho yake, wakayaelewa kwa kina na wakawa na ujasiri wa kusukuma mtindo huo mbele, kama meneja wa Brighton & Hove Albion, Mwitaliano Roberto de Zerbi.

Iwapo kuna mashabiki popote pale duniani ambao wanaweza hata kuanza kuelewa mapenzi na kujitolea kwa De Zerbi, basi ni mashabiki Brighton - klabu ambayo imetoka kwenye ukingo wa kutoweka katika Ligi Kuu ya Uingereza na Ligi na Ulaya.

Kocha huyo mzaliwa wa Brescia mwenye umri wa miaka 44, anachukuliwa na wengi kama mmoja ya makocha bora kuingia kwenye Ligi Kuu ya Uingereza ukiachana na Guardiola wa Manchester City.

Je, De Zerbi alifikaje Brighton?

Mara ya kwanza nilipokutana na De Zerbi ilikuwa Split, Croatia, klabu yake ya wakati huo Shakhtar Donetsk ilikuwa ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Hajduk Split ili kuchangisha fedha kwa ajili ya Ukraine kufuatia uvamizi wa Urusi.

Baada ya mchezo, tukiwa tunazungumza, niliona wachezaji kadhaa wakitoka kwenye chumba cha kubadilishia nguo huku wakitokwa na machozi.

Vita vya Ukraine vilimfanya asiwe na uchaguzi mwingine zaidi ya kuihama klabu hiyo ambayo wakati wa kusimamishwa kwa ligi hiyo, ilikuwa kileleni mwa jedwali. De Zerbi alichagua wakati huo kuwaambia wachezaji anaondoka - na huzuni ilitanda.

De Zerbi alisaini mkataba wa miaka minne katika uwanja wa Amex, Septemba 18 , 2022 kuwa kocha wa Brighton. Brighton ilijua kuhusu meneja huyo tangu enzi zake Sassuolo, timu hiyo ilipomaliza katika nafasi nane bora katika misimu miwili mfululizo. Ueuzi wa De Zerbi ulikuwa wa busara na ubunifu.

'Anaweza kuchukua nafasi ya Guardiola'

Sijui meneja yeyote duniani ambaye anazidi kupata heshima kutoka kwa makocha wakuu duniani kama De Zerbi.

Ninapata jumbe nyingi kuhusu yeye na mtindo wake kutoka kwa makocha wengine kuliko kocha mwingine yeyote. Wanavutiwa na wachezaji wake, jinsi anavyowaboresha na ushambuliaji wao.

Licha ya kufanya vibaya katika mechi tano za mwanzo. Lakini mazungumzo ya kulenga kufuzu Ligi ya Mabingwa yameanza katika korido za uwanja wa mazoezi wa Brighton, hivi karibuni.

Msimu uliopita Brighton, ambayo si miongoni mwa vilabu sita vikubwa nchini Uingereza, walimaliza msimu katika nafasi ya sita na walitoka kwa mikwaju ya penalti katika Kombe la FA .

Klabu hiyo sasa inakusudia kuhakikisha sio tu wanadumisha kiwango chao bali wanajijenga zaidi, na hiyo ni kwa sababu ya shinikizo la De Zerbi kwake mwenyewe na kwa kila mtu anayehusika na klabu.

Matarajio ni makubwa kwenye ajenda aliyoiunda. Klabu inajua Tottenham walitaka kumchukua msimu wa joto lakini aliamua kubaki. Wanataka aendelee kusalia Brighton ili kuipeleka kwenye hatua makubwa na bora zaidi.

Anafanana sana na rafiki yake, Guardiola. Wote wanataka kusonga mbele, na lile la muhimu zaidi - wanatumia falsafa sawa kuhusu jinsi mchezo unapaswa kuchezwa na Guardiola amekiri amejifunza baadhi ya mambo kuhusu soka kutoka kwa De Zerbi.

Hakuna shaka Manchester City wanamzingatia, na, ikiwa Guardiola ataondoka katika klabu hiyo msimu wa joto wa 2025, De Zerbi atakuwa kwenye orodha ya watakao chukua nafasi yake.

Kulipeleka soka kwenye hatua nyingine

Kimsingi, Guardiola alitengeneza njia ya kucheza mchezo huo ambayo imegawika awamu nne; kuanza kutoka nyuma, kuzungusha mpira katikati ya uwanja, kuandaa pasi ya mwisho na kufanya uamuzi wa mwisho.

Aina hiyo ya mchezo ambayo washambuliaji na wachezaji wa mbele wengi wanaweza kudai ni ya kawaida, makocha kama Guardiola na De Zerbi wanaamini inaweza kufunzwa na kuboreshwa.

De Zerbi anataka kupeleka soka katika kiwango kingine kutoka pale pa Guardiola, akifanya mambo ambayo hayajafanyika. Chini yake, wachezaji wana hatari zaidi na wana badilika kuliko hapo awali. Anaweka wachezaji wengi mbele na anafanya kazi kwa bidii kupanga mashambulizi.

Wachezaji wanafurahia kufanya kazi naye kwani wanaelewa kile kinachotarajiwa kufanya. Haikuwa wazi katika akili zao katika wiki chache za kwanza. Matokeo hayakuonekana haraka, na kulikuwa na sauti ambazo zilihoji nini alikuwa anajaribu kukifanya, lakini klabu haikumtilia shaka.

Alianza kama mkufunzi miaka kumi iliyopita na amebaki mwaminifu kwa falsafa yake wakati wote, huku akijifunza kutoka kwa makocha wengine kukuza maoni yake.

Ameizoea vipi Uingereza?

De Zerbi amemfanya kila mtu wa Brighton kuwa na hamu ya kufanya kazi, kubadilika, kuboresha na kujifunza, na amechukua maamuzi tofauti kutokana na ligi anayofundisha.

Huko Uingereza, wachezaji wanathamini zaidi nafasi ya kufurahiya siku baada mazoezi magumu. Amebainisha kuwa wachezaji wanarudi kwa kasi zaidi, baada ya siku ya mapumziko.

Nchini Italia, ambako alifundisha na wanafanya mazoezi kila siku. Amejifunza hitaji la kuwaruhusu wachezaji wake kuchaji miili yao.

Wachezaji wanasemaje?

Jason Steele ni mchezaji aliyezaliwa Brighton. Baada ya kukaa muda mwingi kama chaguo la pili, wakati mwingine hata kipa chaguo la tatu katika vilabu vya awali, chini ya De Zerbi mambo yamebadilika.

Steele anasema, "Zerbi anafanya kazi kila wakati, anajaribu hiki na kile, hujifunza, na haya yote yanaathiri wachezaji pia kwa namna chanya.''

Wakati fowadi wa Uhispania Ansu Fati alipokuwa akitafuta klabu gani ajiunge nayo baada ya kuondoka Barcelona, ​​kati ya Tottenham Hotspur au Brighton.

Alizungumza kwanza na Ange Postecoglou, na kisha De Zerbi ambaye alimwambia kama mchezaji wa zamani aliyecheza namba 10 anaelewa ugumu wa namba hiyo.

Mtindo wa kucheza wa Brighton, ulitosha kumshawishi Ansu kujiunga na klabu hiyo ya Uingereza.