Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ligi ya mabingwa yarejea – Habari zote unazopaswa kujua, nani yuko katika kundi gumu na nani ataibuka mshindi
Manchester City wanaanza kutetea taji lao la Ligi ya Mabingwa wiki hii wakati mechi za makundi zikianza. Kikosi cha Pep Guardiola kimeungana na Arsenal, Manchester United na Newcastle kutoka Ligi Kuu ya Uingereza, huku Newcastle wakirejea katika ligi hiyo baada ya kukosekana kwa miaka 20.
Hizi hapa ni taarifa zote muhimu kuhusu Ligi ya Mabingwa 2023-24. Timu gani ipo katika kundi lipi?
Newcastle wamepangwa Kundi F pamoja na mabingwa wa Ufaransa Paris St-Germain, miamba wa Italia AC Milan na washindi wa zamani wa Ligi ya Mabingwa, Borussia Dortmund.
City watakuwa Kundi G, likionekana kuwa sio kundi gumu - watakapomenyana na RB Leipzig, Red Star Belgrade na Young Boys.
Mabingwa wa Scotland, Celtic wanacheza katika hatua ya makundi kwa msimu wa pili mfululizo. Watakuwa katika kundi moja na Feyenoord, Atletico Madrid na Lazio.
Manchester United watamenyana na wababe wa Ujerumani, Bayern Munich. Wengine ni FC Copenhagen na Galatasaray katika Kundi A.
Arsenal wanachuana na Sevilla, PSV Eindhoven na Lens.
Majina makubwa yamekosekana
Katika ligi hii hakuna matarajio ya kumwona Cristiano Ronaldo wala Lionel Messi, hakuna hata mmoja atakayeshiriki Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Ronaldo alikuwa mmoja wa watu wa kwanza wenye majina makubwa kuhamia Saudi Arabia – anachezea Al Nassr – wakati Messi yuko Marekani na Inter Miami.
Wengine watakao kosekana ni mchezaji wa Brazil, Neymar na mshambuliaji wa Ufaransa, Karim Benzema wamejiunga na Ronaldo kwenye Ligi ya Saudia. Wako pamoja na Al Hilal na Al-Ittihad.
Lakini bado tutaona baadhi ya majina makubwa ya wakati huu, mshambuliaji wa Ufaransa, Kylian Mbappe akiwa PSG na mpachika mabao wa Man City, Erling Haaland akitafuta kuvunja rekodi zaidi.
Lamine Yamal mchezaji mwenye umri wa miaka 16 mwaka huu alikua mchezaji mdogo zaidi wa Barcelona kwa wakati wote na pia ni mchezaji mdogo zaidi na mfungaji mdogo zaidi wa Uhispania.
Tarehe za Mechi
Siku ya kwanza: 19-20 Septemba.
Siku ya pili: 3-4 Oktoba.
Siku ya tatu: Oktoba 24-25.
Siku ya nne: 7-8 Novemba.
Siku ya tano: 28-29 Novemba.
Siku ya sita ya mechi: 12-13 Disemba.
Mechi za 16 bora: 13-14, 20-21 Februari 2024 na 5-6, 12-13 Machi.
Robo fainali: 9-10, 16-17 Aprili.
Nusu fainali: 30 Aprili, 1 Mei, 7-8 Mei.
Fainali: 1 Juni.
Washindi watarajiwa ni nani?
Fainali ya msimu huu itafanyika Wembley. Huku Man City wakipewa nafasi kubwa ya kushinda Ligi ya Mabingwa, mbele ya Real Madrid na Bayern Munich, kulingana na takwimu na utabiri wa Euro Club Index.
City wana 37% ya nafasi ya ushindi, Real 13% na Bayern 11%, na kuna 19% ya jina jipya kuchukua kombe. City, Real, Bayern na Barcelona kila moja ina angalau 90% ya kutinga hatua ya mtoano.
Huu utakuwa msimu wa mwisho wa muundo uliopo sasa wa timu 32 katika awamu ya makundi. Zimegawanywa katika makundi nane ya timu nne-nne, na mbili za juu kujazia 16 bora. Lakini mabadiliko makubwa yanakuja 2024-25.
Muundo huo mpya utajumuisha timu 36, huku nafasi mbili kati ya nne za ziada zikitolewa kwa nchi ambazo vilabu vyake vimefanya vyema zaidi katika msimu uliopita.