Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Simulizi ya kusikitisha ya uraibu wa dawa za kutuliza maumivu
Takribani dawa za kutuliza maumivu zenye nguvu milioni 40 zilitolewa kwa wagonjwa nchini Uingereza mwaka wa 2022/23.
Dawa hizi za opioidi ni pamoja na viambato kama vile mofini, tramadol na fentanyl na zote zinaweza kusababisha uraibu.
Huduma ya Taifa ya Afya (NHS) Uingereza imekuwa ikijaribu kupunguza matumizi ya dawa hizo, miongozo imebadilishwa na idadi ya vidonge vinavyotolewa imekuwa ikipungua, lakini karibu 10% ya wakazi wa Uingereza bado wanazitumia.
Hakuna takwimu za hivi karibuni za idadi ya watu wanaotegemea dawa za kutuliza maumivu za opioidi lakini BBC imekutana na mama mmoja ambaye anataka kuwasaidia watu wengine kutokana na uraibu wao.
Helen Dews ameishi na maumivu ya kudumu kwa karibu miaka 20.
Pamoja na diski iliyoharibika mgongoni mwake, Helen pia ana tishu za kovu na stoma mbili (tundu lililotengenezwa kwa upasuaji kwenye tumbo ambalo huruhusu kinyesi kutolewa kutoka kwa mwili moja kwa moja kupitia mwisho wa matumbo hadi kwenye mfuko wa kukusanya.)
Anasema awali aliagizwa kutumia dawa za kodeini na tramadol ili kujaribu kukabiliana na maumivu ambayo yalimsumbua mwilini, kabla ya kuhamishwa kwenye matumizi ya dawa za mofini na fentanyl.
"Kitu pekee wanachofikiri wanaweza kufanya na maumivu ni kukupa dawa zaidi za kutuliza maumivu," alisema.
Anasema dawa hizo zimekuwa na athari kubwa katika maisha yake na jinsi anavyoishi.
"Maisha yanabadilika sana, inaumiza ubongo wako ili usifikiri vizuri na kupoteza kumbukumbu.
"Sikuweza kukumbuka chochote."
Helen anasema aligundua kuwa kulikuwa na tatizo wakati alipoona dawa yake ya fentanyl ya kupunguza maumivu, ilitakiwa kubadilishwa kila baada ya siku tatu, haikuwa na athari sawa na alitambua kwamba alikuwa akiibadilisha kila siku.
"Nilijua kulikuwa na kitu ambacho hakiko sawa, na nyuma ya akili yangu nilifikiri ungekuwa upande wa uraibu, lakini niliaibika sana," alisema.
Binti yake Aimee Lord pia alikuwa amegundua hilo lakini hakutaka kusema lolote akihofia kumkasirisha mama yake.
“Aliposema anataka kuonana na madaktari na kuzungumza nao kuhusu hilo, nikamwambia ‘Nitakwenda nawe’.
"Nilifarijika kidogo kwa sababu mada hiyo ilikuwa imependekezwa. Sikulazimika kuileta mimi mwenyewe."
Helen hatimaye alielekezwa kufika kwenye kituo cha kutoa huduma ya dawa za kulevya na pombe Forward Leeds mnamo 2022.
"Ilibadilisha kila kitu, nilielewa kilichokuwa kinakoseka, nilielewa kile nilichokuwa nikihisi ni cha kawaida na kile nilichokuwa nikipitia kilikuwa cha kawaida vile vile."
Pia alishtushwa na kuambiwa na wafanyakazi wa huduma hiyo kwamba walishangaa kuwa bado yuko hai.
"Kwa sababu nilikuwa kwenye dozi ya juu sana na kwa sababu ya dawa nyingine pia ninayotumia, alishangaa sikuwa nimezidisha dozi."
Kwa Aimee ilikuwa inatisha na kuogopesha.
"Walinipa kifurushi cha naloxone, ambacho hutumika kubadili kipimo cha opioid.
"Amekuwa akitumia dozi hii ya juu muda huu wote na kumbe ningeweza kurudi kutoka kazini na kumkuta amefariki dunia na sikujua hilo,"mtoto wake alisema.
Helen sasa amepunguza matumizi yake ya opioidi hadi kiwango cha chini kabisa kabla ya upasuaji anaopaswa kufanyiwa, lakini anakubali kuwa kupunguza matumizi ya dawa hizo za maumivu ilikuwa kibarua kigumu.
"Huwezi kula, unataka kutapika, mwili wako wote unauma, mwili wako wote na akili yako vinaathirika, sikujua kitu kama hicho."
Uraibu wa dawa za kutuliza maumivu tayari ni suala zito nchini Marekani.
Mamilioni ya watu nchini Marekani sasa wamezoea kutumia tembe na mabaka yanayotokana na opiamu.
Nchi ilishuhudia karibu vifo 500,000 kutokana na matumizi ya kupita kiasi ya dawa za kupunguza maumivu kati ya 1999 na 2019, kulingana na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Marekani.
Nchini Uingereza, Forward Leeds anaanzisha timu maalum ya kukabiliana na uraibu wa dawa za kutuliza maumivu.
Kelly Stockdale, kutoka huduma ya usaidizi, anasema ni "tatizo kubwa" ambalo, anaamini, wengi hawalitambui kuwa tatizo kwa ukubwa unaostahili.
"Inawezekana watu hawaelewi unaweza kupata uraibu wa opioidi na inakubalika kwa sababu inauzwa kwenye duka la kuuza dawa."
Kelly anaeleza kwamba hangeweza kamwe kujua kuhusu suala hilo kabla ya kufanya kazi katika huduma ya matibabu ya madawa ya kulevya.
"Nilijua dawa za mitaani ni nini, nilijua heroini ni nini, sikutambua kuwa kujiondoa kwenye utumizi wake itakuwa sawa na opioidi nyingine yoyote."
Anasema shirika hilo linawasiliana na watu wengi ambao wanatatizika kutokana na dawa za kutuliza maumivu.
Vijana wanaweza kuwa awali walikunywa dawa hizo kwa ajili ya "kipandauso au maumivu ya hedhi", anasema, lakini baada ya muda mfupi wanaweza kujikuta wakitaka dozi za juu zaidi.
"Katika kizazi cha zamani utaona zaidi kwamba wamekuwa kwenye maagizo ya kurudia dawa hizo kwa muda mrefu bila kugundua kuwa ziligeuka na kuwa tegemezi kimwili."
'Nimebadilika sana'
Helen sasa ana matumaini zaidi kuhusu maisha yake ya baadaye anapojifunza kudhibiti maumivu yake kwa kutumia dozi za chini.
"Lazima nijifunze mimi ni nani sasa kwa sababu nimetumia dawa hizi kwa muda mrefu, nimebadilika sana."
Awali alisita kuzungumza juu ya uraibu wake hadharani lakini anasema anatumai simulizi yake inaweza kuwasaidia wengine kutafuta usaidizi.
"Ni sawa ikiwa nitaaibika kidogo kuliko kutomsaidia mtu," anaongeza.