Hakuna  anayeshinda vita vya Ukraine-mkuu wa ujasusi Kyrylo Budanov aiambia BBC

Iliyochapishwa

Mapigano nchini Ukraine kwa sasa yamekwama kwani Ukraine wala Urusi haziwezi kupiga hatua kubwa, mkuu wa shirika la ujasusi la kijeshi la Ukraine amesema, huku Kyiv ikisubiri silaha za hali ya juu zaidi kutoka kwa washirika wa Magharibi.

"Hali imekwama," Kyrylo Budanov aliambia BBC katika mahojiano. "Hakuna kinachosonga’

Baada ya wanajeshi wa Ukraine kuuteka tena mji wa kusini wa Kherson mwezi Novemba, vita vingi vikali vimekuwa karibu na Bakhmut, katika eneo la mashariki la Donetsk. Kwingineko, vikosi vya Urusi vinaonekana kujilinda wakati majira ya baridi yamepunguza kasi ya operesheni za ardhini za Ukraine katika mstari wa mbele wa kilomita 1,000 (maili 620).

Bw Budanov alisema Urusi "sasa iko katika kikomo kabisa " inakabiliwa na hasara kubwa sana, na anaamini kwamba Kremlin imeamua kutangaza uhamasishaji mwingine wa watu  kujiunga na jeshi. Lakini, aliongeza, vikosi vya Ukraine bado vilikosa rasilimali za kusonga mbele katika maeneo mengi.

"Hatuwezi kuwashinda katika pande zote kwa ukamilifu. Wala hawawezi kutushinda" alisema. "Tunatazamia kwa hamu ugavi mpya wa silaha, na kuwasili kwa silaha za hali ya juu zaidi."

Mapema mwezi huu, baada ya msururu wa vikwazo vya kijeshi vya Urusi, maafisa wa Ukraine walionya kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulizi mengine ya ardhini ya vikosi vya Moscow kutoka Belarus mwanzoni mwa 2023. Msukumo huo, walisema, unaweza kujumuisha jaribio la pili la kuuteka mji mkuu, Kyiv na kuhusisha makumi ya maelfu ya askari wa akiba wanaofunzwa nchini Urusi.

Bw Budanov, hata hivyo, alipuuzilia mbali shughuli za Urusi huko Belarus, ikiwa ni pamoja na harakati za maelfu ya wanajeshi, kama majaribio ya kuifanya Ukraine kuwaelekeza wanajeshi kutoka uwanja wa vita kusini na mashariki kuelekea kaskazini.

Hivi majuzi, alisema, treni iliyojaa askari wa Urusi ilisimama katika eneo karibu na mpaka wa Belarus-Ukraine na kurudi, saa kadhaa baadaye, na kila mtu  akiwa ndani.

"Walifanya hivyo kwa uwazi wakati wa mchana, ili kila mtu aione, hata kama [sisi] hatukutaka," akiongeza kuwa hakuona tishio lolote la kweli kutoka kwa wanajeshi huko Belarus. "Kufikia sasa, sioni dalili zozote za maandalizi ya uvamizi wa Kyiv au maeneo ya kaskazini kutoka Belarus."

Mahojiano hayo katika ofisi ya Bw Budanov yenye mwanga hafifu mjini Kyiv yalifanyika siku chache baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kusafiri hadi mji mkuu wa Belarus, Minsk, kwa mara ya kwanza katika zaidi ya miaka mitatu. Ziara yake hiyo iliibua uvumi kwamba anaweza kujaribu kumshawishi Rais Alexander Lukashenko, mshirika wa muda mrefu, kutuma wanajeshi wa Belarus nchini Ukraine 

Belarus imekuwa ikitumiwa na vikosi vya Urusi kama njia ya kuzindua mashambulizi, lakini Bw Budanov anaamini kwamba jamii ya Belarusi haitaunga mkono ushiriki wowote katika vita hivyo na wachambuzi wametilia shaka kiwango cha utayari wa wanajeshi wake 48,000. "Ndio maana Rais Lukashenko anachukua hatua zote kuzuia maafa kwa nchi yake," alisema.

Tangu kuchukua tena Kherson, vikosi vya Ukraine vimeshiriki katika mapigano ya kikatili na wanajeshi wa Urusi karibu na Bakhmut, katika vita ambavyo vimelinganishwa na Vita vya Kwanza vya Dunia. Kwa Urusi, kuuteka mji huo kungevuruga njia za usambazaji bidhaa za Ukraine  na kufungua njia ya kusonga mbele kuelekea ngome nyingine za Ukraine mashariki, zikiwemo Kramatorsk na Sloviansk.

Mashambulizi hayo, Bw Budanov alisema, yalikuwa yakiongozwa na Wagner Group, jeshi la mamluki la Urusi. Mwanzilishi wake, Yevgeniy Prigozhin, anaaminika kutaka kuuteka mji huo kama tuzo ya kisiasa, huku kukiwa na ushindani kati ya maafisa wakuu wa Urusi.

Mbali na uwanja wa vita, Urusi imefanya kampeni ya anga tangu katikati ya Oktoba, ikilenga miundombinu muhimu ya Ukraine kwa makombora na droni , na kuacha mamilioni bila umeme, joto na maji. Bw Budanov alisema huenda mashambulizi hayo yakaendelea, lakini akapendekeza Urusi isingeweza kudumisha kiwango cha mashambulizi hayo kwa sababu ya kupungua kwa hifadhi ya makombora, na kutokuwa na uwezo wa viwanda vya Urusi kuyajaza tena.

Ingawa Iran imetoa ndege nyingi zisizo na rubani zinazotumika katika mashambulizi ya Russia, mkuu huyo wa kijasusi anasema hadi sasa imekataa kupeleka makombora kwa Urusi, ikifahamu kwamba nchi za Magharibi huenda zikaiwekea hatua Tehran, ambayo tayari imewekewa vikwazo kutokana na mpango wake wa nyuklia.

Huenda vita vikakoma kwa sasa, lakini Bw Budanov anasisitiza kwamba hatimaye Ukraine itatwaa tena eneo lote ambalo sasa linakaliwa, ikiwa ni pamoja na Crimea, peninsula ambayo Urusi iliteka 2014. Anatarajia Ukraine kurejea katika mipaka yake ya 1991, wakati uhuru ulipotangazwa na kuanguka kwa Umoja wa Kisovyeti.