Warusi wanaotuhumiwa kwa uhalifu wanapewa chaguo la kwenda vitani badala ya mahakamani

    • Author, Olga Ivshina
    • Nafasi, BBC
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Machi 28, polisi walifika kwenye nyumba ya Andrey Perlov huko Novosibirsk, Siberia. Wakimshutumu kwa kuiba takribani rubles milioni tatu ($32,000; £24,000) kutoka katika klabu moja ya soka ya Novosibirsk, ambako alikuwa mkurugenzi mkuu - yeye na familia yake wanakanusha hili.

Perlov, mwenye umri wa miaka 62, ni mshindi wa medali ya dhahabu ya Olimpiki, baada ya kushinda mbio za kilomita 50 mwaka 1992.

Amekuwa kizuizini kwa zaidi ya miezi sita na familia yake inasema anashinikizwa akubali kupigana nchini Ukraine. Ameambiwa kesi dhidi yake itasitishwa na inaweza kufutwa vita vitakapomalizika.

Mpango wenyewe

Sio siri kwamba wafungwa wameandikishwa kupigana nchini Ukraine. Na sasa uchunguzi wa BBC unaweza kufichua jinsi hali ilivyobadilika na hata ambao hawajapatikana na hatia wanaandikishwa.

Sheria za hivi sasa zinabainisha kuwa waendesha mashitaka wa mawakili wa utetezi - wanalazimika kisheria kuwafahamisha watu wanaoshtakiwa kwa makosa ya uhalifu kwamba wana chaguo la kwenda vitani badala ya mahakamani.

Sheria hiyo, ilipitishwa Machi 2024, inamaanisha ikiwa watajiandikisha, mashtaka na uchunguzi wowote utasitishwa. Kesi zao kwa ujumla zitafungwa moja kwa moja mwishoni mwa vita.

Olga Romanova, mkurugenzi wa Russia Behind Bars - NGO inayotoa usaidizi wa kisheria kwa wafungwa anasema:

“Polisi sasa wanaweza kumkamata mtu juu ya maiti ya mtu aliyemuua. Wanamfunga pingu na kisha muuaji anasema: 'Oh ngoja, nataka kwenda kwenye operesheni maalum ya kijeshi,' na wanaifunga kesi yake ya jinai."

Tulipokea rekodi iliyovuja ya mpelelezi akimuelezea mwanamke mmoja faida za kutia saini mkataba na jeshi la Urusi - kwa mume wake ambaye tayari aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu kwa wizi.

"Anaweza kufungwa miaka sita zaidi kwa uhalifu huu mwingine," anamwambia. “Nilimpa nafasi ya kusaini makubaliano. Ikiwa ombi lake litakubaliwa ataingia vitani na tutafunga kesi hiyo.”

Ikiwa mtuhumiwa atatia saini, ndani ya siku chache kesi ya jinai husimamishwa, na huenda kwenye mstari wa mbele wa vita mara moja.

Wanasheria wathibitisha

Wanasheria watatu wanaofanya kazi nchini Urusi wamethibitisha kuwa hilo limekuwa kawaida nchini kote. Wengine hujiandikisha kwa matumaini ya kuepuka jela - lakini si njia rahisi, kama kijana Yaroslav Lipavsky yalivyomkuta.

Alitia saini mkataba na jeshi baada ya kushutumiwa kusababisha "madhara makubwa kwa afya na kikundi cha watu."

Mpenzi wake alijigundua kuwa ni mjamzito na ili kuepusha kushtakiwa, Lipavsky alijiandikisha katika jeshi mara tu alipofikisha miaka 18.

Aliondoka Urusi kwenda Ukraine na wiki moja baadaye alifariki - moja ya askari mwenye umri mdogo zaidi kufa katika vita.

Haijabainika ni watu wangapi wanaotuhumiwa kwa uhalifu wamechagua kupigana badala ya kufunguliwa kesi, lakini mabadiliko haya ya sera yanaonyesha hitaji la Urusi la kuimarisha vikosi vyake.

Michael Kofman, mchambuzi wa masuala ya kijeshi katika Shirika la Carnegie Endowment for International Peace, anasema, “serikali inadhani hawa ni watu ambao inaweza kuwaondosha, na hawatakuwa na athari kubwa na mbaya kwa uchumi kiujumla."

Kuwaandikisha wafungwa

Wakati kikundi cha mamluki cha Wagner kilipowaandikisha wafungwa kwa mara ya kwanza, kiongozi wake marehemu, Yevgeny Prigozhin, aliwalenga wafungwa katika jela zenye ulinzi mkali, akisema alihitaji "vipawa vyao vya uhalifu" kama malipo ya msamaha.

BBC na tovuti ya Urusi Mediazona zimeona na kuthibitisha nyaraka za siri zinazotoa maelezo kuhusu mchakato wa kuwasajili wafungwa.

Kwa kuchambua vitambulisho vya wafungwa waliokufa nchini Ukraine na malipo yaliyofanywa kwa familia zao, tunajua kuwa Wagner iliajiri karibu wafungwa 50,000 kutoka magerezani, na wakati fulani walikuwa wakipoteza hadi wapiganaji 200 kwa siku vitani. Na wengine wengi walijeruhiwa.

Vitambulisho vya wafungwa huanza na herufi K, ambayo inasimamia "kolonya" au gereza.

Nambari tatu za kwanza zinatambulisha gereza walikotoka na nambari tatu za mwisho zinamtambulisha mwajiriwa.

Rekodi za malipo zinaonyesha zaidi ya wafungwa 17,000 waliuawa wakijaribu kuuteka mji wa Bakhmut mashariki mwa Ukraine kati ya Julai 2022 na Juni 2023 pekee.

Ili kuziba hasara hiyo, Wagner, na baadaye Wizara ya Ulinzi, wameongeza mikakati yao ya kuajiri ili kupanua uwezo wao wa kuajiri.

Wale wanaokataa

Baadhi ya watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu wanakataa mpango huo mpya kwa sababu wanapinga vita, wengine kwa sababu ya hatari ya kufa au kujeruhiwa kwenye uwanja wa vita, na wengine kwa sababu wanataka kubaki Urusi nyumbani kupiga kesi zao.

Lakini ukikataa mamlaka inakupa shinikizo kubwa, anasema Alina binti wa Andrey Perlov.

"Alikataa na tukapiga kelele kubwa kwenye vyombo vya habari vya ndani kwa hivyo alipelekwa kwenye seli yenye ulinzi mkali, na baadaye walimletea mkataba tena."

Anasema alipokataa kwa mara ya pili, alikatazwa kuonana na familia yake au kuwapigia simu.

Bado wana matumaini ya kuthibitisha kwamba hana hatia, lakini mara ya mwisho Alina alipomwona baba yake mahakamani katikati ya Julai, alikuwa amepoteza uzito sana. "Ni mchangamfu," anasema, "lakini ikiwa hali itaendelea, watamdhoofisha."

Tuliiuliza serikali ya Urusi kuhusu kesi ya Andrey Perlov na ikiwa inawashinikiza isivyo haki wafungwa kujiunga na jeshi. Hawakujibu.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah