Putin anakusanya washirika kuonyesha vikwazo vya Magharibi havifanyi kazi

    • Author, Steve Rosenberg
    • Nafasi, BBC
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Fikiria wewe ni Vladimir Putin. Nchi za Magharibi zinakutenga kwa sababu ya kuivamia Ukraine. Vikwazo vinalenga kuumiza uchumi wa nchi yako katika masoko ya kimataifa.

Na kuna hati ya kukamatwa kwako kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Je, utawezaje kuonyesha vikwazo hivyo vyote havifanyi kazi?

Wiki hii katika mji wa Kazan, Rais Putin atakutana na zaidi ya wakuu wa nchi 20 katika mkutano wa kilele wa mataifa yanayoinukia kiuchumi ya Brics. Miongoni mwa viongozi walioalikwa ni pamoja na Xi Jinping wa China, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian.

Ikulu ya Kremlin inasema ni moja ya "matukio kubwa juu ya sera za kigeni kuwahi kutokea" nchini Urusi.

"Ujumbe wa wazi ni kwamba majaribio ya kuitenga Urusi yameshindwa," anasema Chris Weafer, mwanzilishi wa taasisi ya ushauri ya Macro-Advisory.

"Ni ujumbe kutoka Kremlin kwamba Urusi inastahimili vikwazo. Na katika ngazi ya siasa za kijiografia Urusi ina marafiki wote hawa na wote watakuwa washirika wa Urusi."

Marafiki wa Urusi ni nani?

Brics ni Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Kundi hilo, ambalo mara nyingi hujulikana kama uzani wa kukabiliana na ulimwengu unaoongozwa na Magharibi, limepanuka na kujumuisha Misri, Ethiopia, Iran na Falme za Kiarabu.

Saudi Arabia, pia, imealikwa kujiunga.

Mataifa ya Brics yanachukua 45% ya idadi ya watu ulimwenguni. Uchumi wa nchi wanachama kwa ujumla una thamani ya zaidi ya dola za kimarekani trilioni 28.5. Karibu 28% ya uchumi wa dunia.

Maafisa wa Urusi wamedokeza kuwa nchi nyingine 30 zinataka kujiunga na Brics. Baadhi ya mataifa haya yatashiriki katika mkutano huo.

Akiwa na nia ya kupunguza ukali wa vikwazo vya Magharibi, kiongozi huyo wa Kremlin atatumia mkutano huu kuwashawishi wanachama wa Brics kuchukua sarafu mbadala dhidi ya dola kwa ajili ya malipo ya kimataifa.

"Matatizo mengi ambayo uchumi Urusi unakabiliwanayo yanahusishwa na biashara na malipo ya mpakani. Na mengi ya hayo yanahusishwa na dola ya Marekani," anasema Weafer.

"Hazina ya Marekani ina nguvu na ushawishi mkubwa katika biashara ya kimataifa kwa sababu dola ya Marekani ndiyo sarafu kuu ya kutatua hilo. Nia kuu ya Urusi ni kuvunja utawala wa dola ya Marekani. Inataka nchi za Brics kuunda utaratibu mbadala wa biashara - ili vikwazo visiwe na maana."

BRICS yenyewe

Lakini ndani ya Brics kwenyewe kuna mgawanyiko.

"Kwa namna fulani ni jambo zuri kwa nchi za Magharibi pale China na India zinaposhindwa kukubaliana kuhusu jambo lolote. Kwa sababu kama nchi hizo zingekuwa makini, Brics ingekuwa na ushawishi mkubwa," anabainisha Jim O'Neill, mtaalamu wa uchumi aliyefanya kazi na taasisi ya Goldman Sachs.

O'Neill anaamini "Bric" ilipaswa kuwa kitovu cha uundaji wa sera za kimataifa."

Lakini nchi hizo nne zimeendelea na maisha yao wenyewe, baada ya mataifa husika kuunda kundi lao la Bric – na kisha Afrika Kusini ikajiunga na kuwa BRICS. Wangejaribu kupinga utawala wa G7: mataifa saba makubwa zaidi kiuchumi duniani (Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani).

Sio India na China pekee ambao wana tofauti zao. Kuna mvutano kati ya wanachama wawili wapya wa Brics, Misri na Ethiopia. Na Iran na Saudi Arabia kwa muda mrefu wamekuwa wapinzani wa kikanda.

Wakati Urusi, ikichochewa na chuki dhidi ya Magharibi, inataka kuunda "utaratibu mpya wa dunia," wanachama wengine wa Brics, kama India, wana nia ya kudumisha uhusiano mzuri wa kisiasa na kiuchumi na Magharibi.

Huko Kazan, kazi ya Vladimir Putin itakuwa kuchunguza tofauti na kuchora picha ya umoja, huku akionyesha umma wa Urusi - na jumuiya ya kimataifa - kwamba nchi yake iko mbali na kutengwa.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi