Uchaguzi Kenya 2027: Uchaguzi unaoanza mwaka mmoja kabla ya kura

G

Chanzo cha picha, SOCIALS

    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 9

Vurugu zilizozuka katika mkutano wa Linda Mwananchi kaunti ya Homa Bay nchini Kenya Jumapili zimeongeza joto la kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Gari moja lilichomwa moto, watu kadhaa akiwemo waandishi wa habari walijeruhiwa na washukiwa 17 wakakamatwa. Mashambulizi yalianza Jumamosi usiku baada ya kundi la watu kuvamia Hoteli ya Homa Bay Tourist na kuharibu mali.

Licha ya madai ya kuzuiwa kufika eneo la mkutano, kundi hilo linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna liliendelea na mkutano Nyandiwa, ambako alihutubia kuhusu demokrasia, haki za binadamu na umoja wa kisiasa.

Tukio hilo linaashiria kuanza kwa kipindi cha kisiasa ambacho tayari kinapamba moto nchini Kenya, huku wanasiasa wakianza kushuka mashinani kutafuta uungwaji mkono kuelekea uchaguzi wa tarehe 10 Agosti 2027.

Lakini kwa nini uchaguzi huo unaanza kuzungumziwa sasa, wakati bado kuna takriban mwaka mmoja kabla ya Wakenya kupiga kura?

Jibu ni kwamba nchini Kenya, uchaguzi hauanzi siku ya kupiga kura.

Unaanza mapema zaidi.

Kwa mtu anayefuatilia siasa za Kenya kutoka nje, kuelewa uchaguzi wa 2027 kunahitaji kuanzia kwenye swali rahisi: Nani anasimamia uchaguzi huo na nchi iko tayari kwa kiwango gani? Makala haya yatakuchorea taswira kamili kinachoendelea kwa sasa nchini Kenya.

Hesabu ya kisiasa imeanza

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Rais William Ruto tayari anatafuta muhula wa pili madarakani, huku upande wa upinzani ukianza kupanga namna ya kumkabili.

Vyama vinatafuta miungano, wanasiasa wanapima nguvu zao katika maeneo mbalimbali na mikutano ya hadhara inaanza kuwa sehemu muhimu ya kampeni za kutafuta uungwaji mkono.

Kwa upande wa Ruto, kambi yake pia inatarajiwa kuzuru maeneo mbalimbali nchini kunadi sera za serikali na kuimarisha uungwaji mkono.

Lakini wakati wanasiasa wakianza kuingia mashinani, upande wa kiufundi wa uchaguzi nao tayari umeanza kwa kasi.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, ndiyo yenye jukumu la kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi nchini Kenya. Kazi yake haiishii katika kuhesabu kura. Tume hiyo inasimamia usajili wa wapiga kura, uteuzi wa wagombea, maandalizi ya vituo vya kupigia kura, vifaa vya uchaguzi pamoja na usafirishaji wa matokeo.

Kwa uchaguzi wa 2027, IEBC ina vituo 24,559 vya usajili katika maeneo bunge yote 290. Vituo hivyo pia vitatumika kama vituo vya kupigia kura.

Tume pia inatumia mfumo wa KIEMS, teknolojia inayosaidia kuthibitisha utambulisho wa wapiga kura kwa kutumia alama za vidole, kuchanganua nyaraka za utambulisho na kutuma matokeo kwa njia ya kielektroniki kutoka vituoni.

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Kenya Augaaustine Omondo akielezea kuhusu siasa za kenya amesema ''Uchaguzi wa Kenya si tukio la siku moja, ni mchakato mkubwa unaohitaji maandalizi ya teknolojia, usalama, mawasiliano, usafirishaji na maelfu ya maafisa''.

Gharama ya kuandaa Uchaguzi Kenya

d

Chanzo cha picha, AFP

Tume ya IEBC iliwasilisha bungeni makadirio ya shilingi bilioni 63.9 kwa ajili ya uchaguzi wa 2027.

Fedha hizo zinahusisha kila kitu kuanzia uchapishaji wa karatasi za kura hadi usafirishaji wa vifaa na matokeo.

Uchapishaji wa karatasi za kura pekee ulikadiriwa kugharimu shilingi bilioni 5.9. Usafirishaji ulihitaji shilingi bilioni 3, huku vifaa na usafirishaji wa vifaa vya uchaguzi vikikadiriwa kufikia shilingi bilioni 4.9.

IEBC pia ilisema inahitaji fedha kwa ajili ya kuboresha mifumo yake na kubadilisha vifaa vya KIEMS.

Lakini kuna pengo kubwa kati ya kiasi ambacho IEBC ilisema inahitaji na fedha ilizopewa.

Bunge liliidhinisha shilingi bilioni 41.3 pekee, kiasi ambacho IEBC imesema hakitoshi kuendesha uchaguzi kikamilifu.

Kwa hiyo, moja ya changamoto kubwa kuelekea 2027 ni kuhakikisha uchaguzi unapata fedha zinazohitajika bila kuathiri maandalizi yake.

Mamilioni ya wapiga kura wapya - Vijana

Wakati IEBC ikiandaa vifaa na mifumo, upande mwingine wa uchaguzi nao umeanza kujengwa: wapiga kura wenyewe.

Kati ya Septemba 2025 na Aprili 2026, IEBC iliendesha zoezi la usajili wa wapiga kura katika maeneo bunge yote 290.

Zaidi ya watu milioni 2.6 walijiandikisha kama wapiga kura wapya.

Nairobi pekee ilisajili karibu wapiga kura wapya 277,000.

Kanda ya Kati mwa Kenya iliongoza kwa zaidi ya wapiga kura wapya 527,000. Kiambu pekee ilisajili karibu 129,000, huku Nakuru ikiwa na zaidi ya 102,000 na Meru karibu 68,000.

Rift Valley iliongeza zaidi ya wapiga kura 380,000, huku Magharibi mwa Kenya ikiongeza zaidi ya 273,000.

Pwani ilisajili karibu 200,000, Ukambani karibu 192,000 na Nyanza ya Luo karibu 190,000.

Kaskazini Mashariki ilisajili idadi ndogo zaidi, ikiwa na wapiga kura wapya wasiopungua 98,000.

Idadi hiyo ya wasajili wapya wa kupiga kura ni vijana. Kupitia mitandao ya kijamii walihamasishana kwenda kujisajili na kujenga kauli ya 'Niko Kadi', wakiamini kuwa uchaguzi wa mwakani utawahusu.

Isitoshe, kundi hili la vijana linapigiwa upatu kubadilisha karata ya idadi ya wapiga kura na kuufanya uchaguzi kuwa na ushindani mkubwa.

Lakini idadi ya watu waliojiandikisha si lazima iwe sawa na idadi ya watu watakaopiga kura.

Hapo ndipo uchaguzi wa Kenya wa 2022 unatupa funzo muhimu.

Kura milioni 14.3 ziliamua urais wa 2022

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika uchaguzi wa 2022, Kenya ilikuwa na wapiga kura zaidi ya milioni 22.1 waliosajiliwa. Lakini ni asilimia 64.77 pekee waliojitokeza kupiga kura. Hiyo inamaanisha takriban Wakenya milioni 14.3 ndio waliopiga kura.

William Ruto alishinda urais kwa kura 7,176,141, sawa na asilimia 50.49. Raila Odinga alifuata kwa kura 6,942,930, sawa na asilimia 48.85. Tofauti ilikuwa takriban kura 233,000.

Kwa uchaguzi ulioshindwa kwa tofauti ndogo kiasi hicho, kila kura ilikuwa muhimu.

Lakini zaidi ya idadi ya kura za kitaifa, ramani ya maeneo yaliyompigia kila mgombea ndiyo iliyokuwa muhimu.

Ngome za kisiasa zilivyomsaidia Ruto

c

Chanzo cha picha, Reuters

Ushindi wa Ruto uliimarishwa na uungwaji mkono mkubwa katika Mlima Kenya na eneo la bonde la ufa yaani North Rift. Kaunti 10 za eneo la Mlima Kenya zilikuwa na takriban wapiga kura milioni 5.7 waliosajiliwa, karibu asilimia 27 ya wapiga kura wote nchini. Ruto alipata karibu asilimia 77 ya kura zilizopigwa katika eneo hilo, akivuna takriban kura milioni 2.9.

Katika eneo la North Rift, kaunti kadhaa zilimpatia Ruto takriban kura milioni 1.6. Kwa pamoja, maeneo hayo mawili yalimpatia takriban kura milioni 4.54, karibu asilimia 63 ya kura zote alizopata kitaifa.

Kwa upande mwingine, Raila alikuwa na ngome kubwa Nyanza. Kisumu ilimpa asilimia 97.4 ya kura, Homa Bay asilimia 98.9 na Siaya asilimia 98.6. Lakini uchaguzi huo ulionyesha pia kwamba kuwa na wafuasi wengi katika eneo fulani hakutoshi. Lazima wafuasi hao wajitokeze kupiga kura.

Mombasa ni mfano muhimu. Licha ya kuwa ngome ya muda mrefu ya ODM, idadi ya waliojitokeza kupiga kura ilikuwa asilimia 44 pekee.

2027 ni uchaguzi tofauti

S

Na hapa ndipo uchaguzi wa 2027 unatofautiana na ule wa 2022.

Kenya imeingia katika kipindi hiki bila mmoja wa watu muhimu zaidi katika siasa zake za kisasa.

Raila Odinga, aliyewahi kuwania urais mara tano, alifariki tarehe 15 Oktoba 2025 akiwa na umri wa miaka 80. Kwa miongo kadhaa, Raila alijenga harakati ya kisiasa iliyovuka mipaka ya maeneo na vizazi na kuwa na mamilioni ya wafuasi.

Sasa, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi, swali kubwa ni nani atakayerithi nguvu hiyo ya kisiasa. Na jibu lake linaweza kubadili kabisa hesabu za uchaguzi wa 2027.

Nani anataka kuingia Ikulu?

Joto la kisiasa linaongezeka huku viongozi wa serikali na upinzani wakiendelea na shughuli za kisiasa za hadharani katika jitihada za kuwavutia wafuasi kwenye kambi zao.

Rais William Ruto tayari ameonyesha azma ya kutafuta muhula wa pili.

Lakini moja ya maswali yanayozunguka kambi yake ni nani atakayekuwa mgombea mwenza wake. Kwa sasa, Kindiki Kithure ndiye Naibu Rais wa Kenya. Hata hivyo, wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema huenda ikawa vigumu kupatiwa wadhifa huo ambao aliupata baada ya Rigathi Gachagua kuondolewa. Oburu Oginga na Kithure Kindiki wameonyesha nia ya kushiriki katika kinyanganyiro hicho.

Upande wa upinzani nao unaanza kupanga safu zake. Majina yanayotajwa ni pamoja na Kalonzo Musyoka, Fred Matiang'i na Martha Karua, huku Edwin Sifuna pia akitajwa katika baadhi ya mijadala ya kisiasa.

Hata hivyo, siasa za Kenya zinaweza kubadilika haraka. Miungano inaweza kubadilika, wagombea wanaweza kujiondoa na vyama vinaweza kuungana kabla ya tarehe ya uteuzi. Ndiyo maana katika siasa za Kenya, mwaka mmoja ni muda mrefu sana.

Muda muhimu kuelekea uchaguzi

D

Kwa maafisa wa umma wanaopanga kuwania nafasi za kisiasa katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, tarehe ya mwisho ya kujiuzulu kutoka katika nyadhifa zao ni 9 Februari 2027, siku sita kabla ya uchaguzi. Vyama vya kisiasa vina hadi 16 Machi 2027 kuwasilisha kwa IEBC orodha za wanachama wao.

Pia vinapaswa kuwasilisha majina ya watu wanaotarajia kuwania nafasi kupitia kura za mchujo za vyama, pamoja na tarehe na maeneo zitakakofanyika.

Wagombea huru wanapaswa kuwasilisha majina yao na nembo wanazotumia kwa IEBC kufikia 9 Mei 2027, huku wakihakikisha kuwa si wanachama wa chama chochote cha kisiasa kilichosajiliwa.

Vyama vya kisiasa pia vinapaswa kuwa vimeendesha kura zao za mchujo na kutatua malalamiko yote yanayotokana na zoezi hilo kufikia tarehe hiyo.

Dirisha la uteuzi wa wagombea litafunguliwa kuanzia 29 Mei hadi 11 Juni 2027.

Baada ya uteuzi huo, malalamiko yoyote yatakayotokana na mchakato huo yanapaswa kutatuliwa ndani ya siku 10. Malalamiko hayo yanapaswa kuwa yamewasilishwa kabla au ifikapo 12 Juni.

Kufikia 27 Julai, vyama vya kisiasa na wagombea huru wanapaswa kuwa wamewasilisha majina ya mawakala wao wa kitaifa, kaunti, maeneo bunge na vituo vya kupigia kura.

Kampeni rasmi zitaanza 29 Mei na kuendelea hadi 7 Agosti, saa 48 kabla ya Wakenya kwenda kupiga kura.

Kampeni zitaruhusiwa kuendeshwa kila siku kati ya saa moja asubuhi na saa kumi na mbili jioni.

Kisha, baada ya miezi kadhaa ya maandalizi, uteuzi wa wagombea, kampeni na miungano mipya ya kisiasa, Wakenya watafika katika vituo vya kupigia kura tarehe 10 Agosti 2027.

Wasiwasi kuhusu uaminifu wa uchaguzi

Lakini kuna jambo jingine ambalo linaweza kuamua namna Wakenya watakavyoupokea uchaguzi huo: imani katika mchakato wa uchaguzi.

Chaguzi zilizopita zimekuwa zikikabiliwa na madai ya ukiukaji wa taratibu, udanganyifu na wizi wa kura.

IEBC inasema imeanza maandalizi ya kuhakikisha uchaguzi wa 2027 unakuwa wa uwazi, shirikishi na huru kutokana na ushawishi wa kisiasa.

Kamishna wa IEBC Alutalala Mukhwana amesema uchaguzi huo utaendeshwa kwa kufuata sheria.

Hata hivyo, amekiri kuwa siasa haziwezi kuondolewa kabisa katika mchakato wa uchaguzi, kwa sababu wanasiasa ni sehemu muhimu ya kuhamasisha wapiga kura.

Kuhusu teknolojia, IEBC inasema vifaa vipya vya KIEMS vinavyoagizwa kutoka nje vitawekewa mifumo ya ziada ya usalama ili kupunguza uwezekano wa hitilafu.

Lakini kwa Wakenya, swali si teknolojia pekee. Ni kama wataamini matokeo yatakayotangazwa.

Chaguzi ndogo za Ol Kalau zilichora taswira kuhusu mustakabali wa chaguzi zijazo.

Vile vile, kuna wasiwasi baada ya ripoti mpya iliyotolewa na Wakfu wa Kofi Annan imeonya kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa ghasia katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Hata hivyo, idara za polisi zimeeleza kuwa zimeanza kuweka mikakati kudhibiti uhuni unaojitokeza kipindi hiki cha kampeini.

Mzozo kuhusu siku ya uchaguzi

Mjadala wa uchaguzi wa 2027 hauishii kwenye wagombea na kampeni. Kumekuwa pia na changamoto za kisheria kuhusu tarehe ya uchaguzi.

Ombi lililowasilishwa Mahakama Kuu lilitaka uchaguzi huo uahirishwe ili Katiba ifanyiwe marekebisho makubwa.

Mapendekezo hayo yalihusisha, miongoni mwa mambo mengine, kutathmini upya ukomo wa mihula ya rais na viongozi wengine pamoja na kuanzishwa kwa ofisi ya Kiongozi wa Upinzani yenye mamlaka ya kusimamia utendaji wa serikali.

Lakini Jaji Patricia Nyaundi aliamua kuwa marekebisho ya Katiba lazima yafuate taratibu zilizowekwa na Katiba yenyewe.

Kwa sasa, ratiba ya uchaguzi haijabadilika. Tarehe ni 10 Agosti 2027.

Bado siku 358, lakini hesabu tayari imeanza

Kwa Wakenya, uchaguzi wa 2027 unaweza kuonekana kuwa bado uko mbali. Lakini nyuma ya pazia, hesabu tayari imeanza.

IEBC inahesabu fedha na vifaa. Vyama vinatafuta wagombea na miungano. Wanasiasa wanapima nguvu zao. Wapiga kura wapya wamejiandikisha. Na wapinzani wa Ruto wanajaribu kujenga nguvu mpya baada ya kifo cha Raila Odinga.

Kilicho wazi ni kwamba uchaguzi huu hautakuwa tu kuhusu nani atakuwa rais. Utakuwa pia mtihani wa uwezo wa Kenya kuendesha uchaguzi wenye uaminifu, uwazi na ushiriki mkubwa wa wananchi.

Na kwa tofauti ya kura 233,000 iliyotenganisha washindi na washindwa mwaka 2022, swali moja linaweza kuwa muhimu kuliko mengine yote:

Ni Wakenya wangapi kati ya wale zaidi ya milioni 2.6 waliojiandikisha kwa mara ya kwanza watafika kituoni kupiga kura tarehe 10 Agosti 2027?

Jibu la swali hilo linaweza kuwa sehemu ya uamuzi wa nani atakayeingia Ikulu baada ya uchaguzi ujao.