Jinsi vifaa vya kielektroniki vinavyoathiri miili yetu

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Vifaa vya kielektroniki huathiri mwili wako kwa njia ambazo huenda huna habari, lakini bado unaweza kuchukua hatua za kupunguza athari hizi.

Tunapowaza kuhusu athari za matumizi yetu ya simu za rununu, huwa tunazingatia zaidi upande wa kisaikolojia. Lakini hivi majuzi, niligundua uvimbe mdogo, mgumu kwenye kidole changu, haswa mahali simu yangu inapokaa; hii ilinifanya nijiulize: simu yangu inaathiri vipi mwili wangu kwa ujumla?

Niliwasiliana na baadhi ya wataalamu ili kujua. Na jibu, kama nilivyotarajia, halikuwa la kutia moyo

Uchunguzi wa kisayansi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba simu yako na vifaa vingine vya kielektroniki huenda vinabadilisha umbo la shingo yako, kuharibu macho yako, kuathiri mwendo wako, na kudhoofisha misuli yako. Baadhi hata wanahofia kwamba maisha yetu yanayotegemea teknolojia yanazeesha haraka. Baadhi ya matatizo haya ya kimwili, yanaweza kusababisha kupungua kwa utambuzi au masuala mengine makubwa zaidi ya kiafya.

Sijui unachukilia vipi hilo? Sijui, lakini siko tayari kukaa mahali pamoja kwa muda mrefu kwa sababu kukaa kwa muda mrefu ni sehemu ya tatizo. Kwa bahati nzuri, ikiwa hutaki teknolojia iathiri mwili wako, kuna mambo unayoweza kufanya kukabiliana na hilo.

Uti wa mgongo kuathirika

Ikiwa unasoma taarifa hii kwenye simu yako, huenda unainamisha kichwa chako ili kuitazama.

Hali hii, inayojulikana kama "kuinamisha kichwa mbele," inaweza kuweka shinikizo la hadi kilo 27 kwenye shingo yako.

Kuendelea kufanya hivyo baada ya muda, kunaweza kuathiri uti wako wa mgongo, na kua kupasuka kwenye viungo na misuli, na hata kupungua kwa uwezo wa mapafu. Wakati mwingine huitwa "shingo ya teknolojia."

Inaweza pia kubadilisha kabisa mwonekano wa mwili wako.

Ina fulani ya mazoezi maalum, kwa ushauri wa daktari, inaweza kusaidia kutatua tatizo hili. Hata hivyo, kuna kitu rahisi anachoweza kufanya mara moja, kama vile kuinua simu yako juu.

Inua simu yako katika usawa wa jicho, kwa urefu wa mkono kutoka usoni. Mbinu hii ya kutumia vifaa vya kielectoriniki pi a inapendekezwa kwa wachunguzi wa kompyuta.

Wataalamu wengine wanasema kwamba kuchukua mapumziko kutoka kwa skrini kunaweza kuwa na manufaa. Jaribu kuchukua mapumziko ya dakika 20 kila baada ya nusu saa.

Muwasho wa ngozi na mikunjo kwenye shingo

Hivi majuzi, wasiwasi mpya umeibuka: Je, maumivu ya shingo yanayotokana na matumizi ya vifaa vya kielektroniki husababisha mikunjo shingoni?

"Inaeleweka kinadharia," anasema Justine Hextall, mtaalamu wa magonjwa ya ngozi na Mwanachama wa Chuo cha Royal College of Physicians nchini Uingereza.

Anaongeza kuwa kukaa ukiwa umeinamisha kichwa husababisha mikunjo shingoni, kwa hivyo kuinama mbele kila mara na kuinua shingo kunaweza kuwa tatizo.

Hata hivyo, Hextall anasema kwamba hakuna tafiti za kuaminika zinazothibitisha uhusiano huu. Anashauri dhidi ya kununua bidhaa zozote zinazouzwa mtandaoni zinazodai kutibu "maumivu ya shingo yanayosababishwa na kutumia vifaa vya kielektroniki."

Hata hivyo, kuna matatizo mengine ya ngozi ambayo yanasababishwa na wasiwasi, hasa kwa watumiaji wa saa za kidigitali ambao wanazivaa mkononi kwa muda mrefu.

Anasema, "Mazingira ya unyevunyevu, kama eneo la chini ya saa, huchangia ukuaji wa fangasi, ambayo inaweza kusababisha muwasho. Hii inaweza kuharibu kinga ya ngozi, Hextall pia anasema inaweza kusababisha mzio unaotokana na bidhaa za kielektroniki, ikiwa ni pamoja na nickel, rubber, latex, na kundi la kemikali zinazoitwa acrylates.

Anaelezea kwamba suluhisho ni rahisi: vua saa yako ya mkononi mara kwa mara na osha ngozi yako. Pia anapendekeza kutumia krimu ya kinga ikivaa saa siku nzima.

Kudhoofika kwa macho

Viwango vya myopia, au kutoona vizuri, vimeongezeka sana kwa miongo kadhaa. Kwa kuangalia kilichobadilika, ni rahisi kusingizia teknolojia.

"Hiyo inaweza kuwa kweli, kwa kiwango fulani lakini si kwa jinsi unavyoweza kufikiria," kulingana na Donald Motty, profesa wa ophthalmology katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Ohio nchini Marekani.

"Tulifanya utafiti wa muda mrefu kuhusu ukuaji wa macho ya watoto ambao ulidumu kwa zaidi ya miaka 20, tukiangalia sababu za hatari za kuanza na kuendelea kwa myopia," anasema Motti. Mojawapo ya maswali muhimu ilikuwa ni kuchunguza uhusiano kati ya myopia na "kazi ya karibu," ikimaanisha kazi zinazohitaji kuzingatia kitu kilicho karibu na uso, kama vile simu. "Jibu lilikuwa: hapana," anaongeza.

Lakini utafiti huo ulifichua jambo lingine: Kutumia muda nje kunaonekana kuwa na athari ya kinga. "Wazo ni kwamba mwanga mkali nje huchochea kutolewa kwa dopamine kutoka kwa retina," anasema Motti, na hii inaonekana kuathiri jinsi jicho linavyokua.

Teknolojia ni sehemu ya mabadiliko ya kimataifa kuelekea kutumia muda mwingi ndani. Kwa maana hii, Moti anaamini vifaa vyako vinaweza kuwa na athari hasi isiyo ya moja kwa moja kwenye macho yako.

Moti anaongeza kuwa unatakiwa kutumia muda mwingi nje. Hii haisaidii macho yako pekee, bali pia inakusaidia kulala vizuri zaidi.

"Hakikisha tu unatumia mafuta ya kuzuia jua na miwani ya jua ili kuepuka athari mbaya za mwanga wa jua," anasema.

Mikono dhaifu

Nguvu ya kushikilia kitu inachukuliwa kuwa kiashiria muhimu cha afya kwa ujumla, na kiashiria hiki kinazidi kutambuliwa.

Utafiti mmoja ulibaini kuwa nguvu ya kushikilia ni kiashiria bora cha kifo cha mapema kuliko shinikizo la damu. Nguvu ya kushikilia inapungua katika nchi nyingi, haswa miongoni mwa vijana.

"Kupungua (kwa nguvu ya kimwili) kati ya vizazi haiangazii mikono dhaifu pekee, bali pia inaweza kuwa kiashiria cha mapema cha afya ya vizazi vijavyo," anasema Johannes Biller, profesa wa sosholojia ya matibabu katika Chuo Kikuu cha Matibabu cha Lausitz nchini Ujerumani.

Anaongeza: "Kuna uwezekano mkubwa kwamba mabadiliko kuelekea kazi ya ofisini ambayo inamlazimu mtu kukaa mahali pamoja kwa muda mrefu inachangia kupungua kwa uwezo wa mwili," na hii pia inaweza kuathiri nguvu ya kushikilia.

Unatakiwa kuwa na uwezo wa kubana mpira wa tenisi kwa nguvu na kudumisha shinikizo hilo kwa sekunde 15 hadi 30. Lakini sio nguvu ya kushikilia pekee; pia inahusi kuboresha utimamu wako wa mwili kwa ujumla. Kwa kuzingatia hilo unashauriwa kufanya mazoezi mara kwa mara.

Utendakazi wa mikono na macho

Teknolojia inaonekana kuathiri ujuzi wa misuli, ambao ni uwezo unaounganisha akili na mwili kufanya mienendo sahihi.

"Teknolojia inaweza kuboresha ujuzi wako katika mambo kama vile kupiga na kusogeza," anasema Sebastian Suget, profesa wa saikolojia ya maendeleo na elimu katika Chuo Kikuu cha Regensburg nchini Ujerumani. "Lakini tukiangalia ukuaji wa ujuzi wa misuli kwa ujumla, na hasa ujuzi mzuri wa misuli, ushahidi unaonyesha madhara mabaya."

Tunajua mengi zaidi kuhusu athari za teknolojia kwa watoto kuliko kwa watu wazima. Utafiti wa Sughit unaonyesha uhusiano kati ya muda ulioongezeka wa kutumia skrini na kupungua kwa ujuzi wa misuli.

Je, vifaa vya kielektroniki "vimeathiri" kabisa mienendo yetu ya utotoni?

Hii inatia wasiwasi hasa kwa sababu kuna uhusiano kati ya ujuzi wa misuli na ukuaji wa utambuzi wa kitaaluma kwa watoto na vijana.

Ushauri wa Sughit si kuogopa au kupiga marufuku bidhaa hizo, ni kudhibiti utumizi ili isiathiri maisha ya kila siku.

Kazi zinazoendelea za mikono, kama vile kuandaa chakula au kujihusisha na sanaa na ufundi, zinaweza kusaidia. Sughit hufanya kazi ya useremala, lakini pia unaweza kujifunza kucheza ala ya muziki au hata kuandika.

"Sio mwisho wa dunia," anasema Sughit. "Hizi ni athari ndogo. Lakini hata kama athari hizi ni za wastani kwa mtu binafsi, vizazi vyote vinakabiliwa na hatari ya kupungua kwa kiwango cha ufahamu katika jamii, na kutoweza kufikiria kihalisi, kwa sababu mikono ndiyo sehemu kuu ya mawasiliano inayotuunganisha na ulimwengu."