Rais wa Ujerumani awaomba radhi Watanzania kuhusu uhalifu wa Wajerumani wakati wa Vita vya MajiMaji

Iliyochapishwa

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier siku ya Jumatano ameomba radhi na kueleza kufedheheshwa kwake na uhalifu uliofanywa wakati wa utawala wa kikoloni wa Ujerumani nchini Tanzania, wakati huo ikiitwa Tanganyika na kuahidi kuongeza uelewa kuhusu madhila hayo katika nchi yake, imerpoti tovuti ya DW.

Kadhalika taarifa hizo za Ujerumani kuomba radhi zimechapishwa na Makumbusho ya Taifa ya Tanzania katika ukurasa wake wa mtandao wa X, zamani Tweeter.

“Ningependa kuomba radhi kwa kile ambacho Wajerumani walikifanya kwa mababu zenu hapa,” alisema Steinmeier alipotembelea makumbusho ya vita vya Maji Maji, yaliyopo mji wa Songea, mkoani Ruvuma, Kusini mwa Tanzania.

Tanganyika ambayo baadaye iliungana na Zanzibar na kunda Tanzania ya sasa ilikuwa sehemu ya Afrika Mashariki ya Ujerumani (German East Africa), iliyojumuisha pia Rwanda na Burundi za sasa ambayo ilishuhudia umwagaji damu mkubwa zaidi katika historia ya ukoloni huo kati ya 1905 na 1907.

Wataalamu wanasema kati ya watu 200,000 na 300,000 kutoka jamii za makabila ya asili waliuawa kikatili na uharibifu wa mashamba na vijiji ulifanywa na wanajeshi wa Ujerumani wakati wa kile kinachoitwa ‘Uasi wa Maji Maji.’

Akieleza kufedheheshwa kwake kwa tukio hilo, Steinmeier alisema Ujerumani iko tayari kufanya kazi na Tanzania kuyatathmini kwa pamoja yale yaliyopita.

"Kilichotokea hapa ni historia inayotuhusu sisi na ninyi- historia ya mababu zenu na historia ya mababu zetu wa Ujerumani," alisema, akiahidi "nitazichukua simulizi hizi pamoja nami hadi Ujerumani, ili watu wengi zaidi katika nchi yangu wazijue."

"Nataka kuwahakikishia kuwa sisi Wajerumani tutashirikiana nanyi kwa pamoja kutafuta majibu ya maswali ambayo hayajajibiwa ambayo hayawapi amani," aliongeza.

Hatua hii ina maana gani?

Baada ya hatua ya Ujerumani kuomba radhi Watanzania kwa ukatili wakati wa ukoloni, Regina Mziwanda wa BBC amezungumza na mwanahistoria Mohamed Saidi, ambaye kwanza anaeleza maana ya hatua hiyo.

Ziara hiyo katika makumbusho imefanyika siku ya mwisho ya ziara ya siku tatu ya Steinmeier nchini Tanzania, ambapo Jumanne alifungua milango ya kurejeshwa Tanzania kwa vitu vya kale vilivyoporwa wakati wa ukoloni.

Ujerumani iko tayari kushirikiana na Tanzania katika "kurejeshwa kwa mali za kitamaduni na mabaki ya binadamu," alisema baada ya kukutana na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam.

Safari ya Steinmeier inakwenda sambamba na ziara ya Mfalme Charles III wa Uingereza nchini Kenya, ambayo pia ilitarajiwa kutawaliwa na mazungumzo kuhusu enzi ya ukoloni.