'Sina hisia, lakini Jane hakuniangalia kama mzigo'

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Kwa miaka 11 sasa, Brian Waihenya amekuwa akitumia kiti mwendo baada ya kupata ajali mbaya ya gari iliyoumiza uti wa mgongo na kumbadilishia kabisa mwelekeo wa maisha.

"Ninatumia kiti mwendo kwa miaka 11 sasa tangu nilipopata ajali ya gari na kuumia uti wa mgongo," anasimulia Brian kwa utulivu. "Sina hisia kuanzia kifuani kushuka chini. Inaniathiri mambo mengi ikiwemo kukosa hisia wakati wa kwenda haja."

Kwa kijana huyu mwenye miaka 30 kutoka kaunti ya Nakuru, maisha yalionekana kama njia ya changamoto zisizoisha.

Lakini ndani ya giza la majonzi, mwanga wa upendo ulianza kung'aa kupitia njia isiyotarajiwa: mitandao ya kijamii.

"Tulikutana Facebook, leo tunaishi kama mume na mke"

"Tulikutana kupitia Facebook," anasema Brian huku akitabasamu kwa upole.

Kama ilivyo kwa kizazi cha sasa, ambacho mawasiliano mengi huanza mtandaoni, ndivyo ilivyokuwa kwa Brian na Jane Karumba. Walianza kama marafiki wa mtandaoni, Jane akivutiwa na simulizi na machapisho ya Brian kuhusu maisha yake baada ya ajali.

"Nilivutiwa sana na jinsi anavyoshiriki maisha yake bila woga," asema Jane kwa macho yenye mapenzi akimtazama mumewe. "Alikuwa tofauti. Kulikuwa na kina katika maneno yake moyo wa kweli."

Jane alianzisha mazungumzo kupitia ujumbe wa kawaida, lakini haikuchukua muda mrefu kabla ya urafiki wao kukua na kugeuka kuwa safari ya mapenzi isiyopimika.

Kila mahali unapoona Brian, basi huenda ukamuona Jane karibu naye si kwa sababu ya wajibu, bali kwa sababu ya upendo.

Brian anakiri kwamba kabla ya kukutana na Jane, wazazi wake hususan baba yake walikuwa msaada mkubwa katika maisha ya kila siku. "Alinisaidia kuoga, kuvaa, kunisaidia kutoka na kurudi nyumbani. Lakini Jane alikuja na kuleta kitu tofauti hakuniangalia kama mzigo."

Kwa Jane, haikuwa rahisi sana kwa kila mtu kuelewa uamuzi wake. Lakini wazazi wake walimuunga mkono, kwa imani kwamba alikuwa amefuata moyo wake. "Walisema ikiwa nimempenda kwa dhati, basi na wao wanaridhia," anasema kwa kujiamini.

Hatimaye, baada ya wazazi wa pande zote kukubaliana, mahari ililipwa na taratibu za kimila zikafuatwa, wakawa mke na mume.

"Najua ni nini kilichonivutia kwake"

Brian, ambaye ni mwandishi wa habari kitaaluma, ameibuka kuwa sauti yenye nguvu mtandaoni akielimisha jamii kuhusu haki, heshima na huduma kwa watu wenye ulemavu. Sasa akiwa na Jane kama mshirika wake mkuu, wanashirikiana kutoa elimu na matumaini kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Wanazungumzia kwa ujasiri masuala ya watu wenye ulemavu, changamoto wanazopitia, na umuhimu wa jamii kuwakubali bila ubaguzi. Pia, wanadhihirisha kwa vitendo kuwa mapenzi ya kweli bado yapo.

"Watu huniambia nimeolewa kwa sababu ya pesa," Jane anasema. "Lakini mimi najua ni nini kilichonivutia kwake moyo wake, juhudi zake, ujasiri wake."

Ingawa bado hawajapata watoto, wawili hao wana matumaini makubwa ya kuanzisha familia yao. Lakini hata kabla ya hilo kutimia, tayari wamejenga msingi imara wa ndoa yao.

"Hatuwezi kulala bila kusameheana," Brian anasema. "Tunajua tunavyohitajiana kwa hivyo kila tofauti huisha kwa mazungumzo na msamaha."

Wanawaambia wale walio kwenye mahusiano ya aina kama yao wasikate tamaa, na waishi kwa ukweli na kuaminiana.