Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bowen: Netanyahu anajua kunusurika kwa Hamas ni sawa na kushindwa kwake
Na Jeremy Bowen
Mhariri wa BBC wa kimataifa
Baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo magumu kati ya wapiganaji na wapatanishi, wakati umefika wa kufanya maamuzi magumu.
Hamas imekubali rasimu ya makubaliano ya kusitisha mapigano, ambayo ni "mbali na kukidhi matakwa ya Israel", kulingana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Bado ameona ni muhimu kutuuma ujumbe ili kulijadili.
Israeli ilikubali pendekezo la kusitisha mapigano mwishoni mwa Aprili. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema ni "ukarimu wa kipekee".
Changamoto kubwa kwa wanaofanya mazungumzo mjini Cairo ni kuziba pengo kati ya matakwa ya Israel na hatua ya kusitisha mapigano inayokubaliwa na Hamas.
Vyanzo vya kidiplomasia nchini Qatar, ambayo ni sehemu ya juhudi za upatanishi na Misri na Marekani, viliniambia "kwa upana ni sawa na tu pendekezo la Israeli. Ni maneno machache tu yamebadilika na maelezo".
Israeli inaweza kuamua kwamba tofauti sio ndogo. Jambo moja kuu la kuzingatiwa limekuwa kwamba Hamas inataka usitishaji mapigano uwe wa kudumu, sio wa muda, na kufuatiwa na kujiondoa kwa Israeli kutoka Gaza.
Tunajua kwamba Israel imekuwa ikielekeza hatua zake katika awamu inayofuata ya vita kwa kudhani kuwa Yahya Sinwar, mkuu wa Hamas huko Gaza ambaye amekuwa mafichoni tangu tarehe 7 Oktoba, hawezi kamwe kukubali kusitishwa kwa mapigano.
Israel ilitumia kutokuwepo kwa pendekezo la kusitisha mapigano kutoka kwa Hamas kama kigezo cha uamuzi wake wa kuanzisha operesheni ya kijeshi huko Gaza.
Marekani iko wazi kabisa kwamba inapinga kabisa operesheni yoyote ya ardhini huko Rafah ambayo inaweza kutishia maisha ya raia zaidi wa Palestina.
Wakati Israel ilipowatahadharisha Wapalestina takriban 100,000 kuondoka majumbani mwao mapema Jumatatu, waziri wake wa ulinzi Yoav Gallant alimwambia mwenzake wa Marekani kwamba hakuna njia mbadala ya shambulio la Rafah.
Alisema hilo kwasababu Hamas ilikuwa imekataa kila pendekezo la kusitishwa kwa mapigano kwa muda na kuachiliwa kwa mateka.
Saa chache tu baadaye, Hamas ilitoa tangazo lake, ikiita kauli hiyo Gallant upuuzi wa Israel.
Bw Netanyahu yuko katika mvutano wa kisiasa. Mtindo wake wa uongozi kwa zaidi ya miaka 16 kama kiongozi wa Israeli umekuwa na tabia ya kuahirisha maamuzi magumu.
Iwapo wajumbe wa Marekani, wakiongozwa na mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani- CIA William Burns, wanaamini kuwa mapengo yanaweza kuzibwa, Bw Netanyahu anaweza kutarajia shinikizo kutoka Washington kukubaliana naye.
Hadi Jumatatu jioni, dhana ya Israel ya kufanya kazi ilikuwa kwamba Hamas haitakubali pendekezo la kusitisha mapigano. Benjamin Netanyahu na serikali yake, kama waangalizi wengi wa kigeni, walipofushwa macho wakati Hamas ilipotangaza uamuzi wake.
Kuna njia mbili za kuangalia kuhusu karata inayoweza kuchezwa na Hamas. Inaweza kuonekana kama hatua ya kukata tamaa ya shirika lililomwagika damu vibaya na karibu kuvunjwa kwa mashambulizi ya muda mrefu ya Israeli. Au ilikuwa ni hatua ya ujanja wa kisiasa ambayo imerudisha shinikizo kwa Bw Netanyahu. Maelezo hayo yanaaminika zaidi, kwani mipango na mawazo ya Israeli yalipuuzwa.
Lakini sasa Netanyahu anakabiliwa na shinikizo kali, kutoka pande zote, huu ni wakati wa maamuzi.
Shinikizo kubwa zaidi linatoka kwa Wayahudi wawili wenye msimamo mkali katika baraza lake la mawaziri - waziri wa fedha Bezalel Smotrich na Itamar Ben Gvir, na waziri wa usalama wa taifa.
Bw Netanyahu anahitaji kura zao ili kuuweka muungano wake mamlakani. Wanataka Israel iikalie Rafah na wametishia kuiangusha serikali ikiwa hataifanikisha. Kwao, kusitisha mapigano ni sawa na kujisalimisha.
Wakati huo huo, familia na wanaowaunga mkono mateka wa Israel wamekuwa wakiandamana, wakifunga barabara kuu kuitaka Israel ifanye makubaliano ya kuwarejesha nyumbani.
Familia za mateka zinaungwa mkono na wajumbe wa baraza la mawaziri la vita, Benny Gantz na Gabi Eisenkot, viongozi wawili wa upinzani waliojiunga na baraza la mawaziri baada ya mashambulizi ya Oktoba 7. Wanaweza kujiondoka kwenye serikali ikiwa, kwa kukosekana kwa usitishaji mapigano, mateka wataendelea kushikiliwa. Wamarekani pia wanataka makubaliano.
Uungaji mkono wa Rais Biden kwa Israeli, hata kama jeshi lake liliua idadi kubwa ya raia wa Palestina, unaathiri uungwaji mkono wake wa kisiasa.
Iwapo Bw Biden ataamua kuwa kuna wazo la usitishaji wa mapigano linalokubalika, atamshinikiza Benjamin Netanyahu kuliunga mkono.
Kiongozi huyo wa Israel atalazimika kuchagua kati ya kunusurika kwa serikali yake na uungwaji mkono muhimu ambao rais wa Marekani amempa katika miezi ya hivi karibuni.
Inaaminika sana Israel kwamba Bw Netanyahu anataka kurefusha vita ili kuzima shutuma kwamba binafsi alihusika katika makosa ambayo yaliipa Hamas fursa ya kuwaua takriban watu 1200 tarehe 7 Oktoba, wengi wao wakiwa Waisraeli na kuwachukua mateka 240 hadi Gaza.
Kusitishwa kwa mapigano pia kunaweza kumaanisha kuwa Benjamin Netanyahu hajapata "ushindi kamili" dhidi ya Hamas - mojawapo ya malengo yake makuu mawili ya vita. Nyingine ni kuwaachilia mateka, jambo ambalo pia hajafanikiwa.
Vita hivi vinaonyesha, kwa mara nyingine tena, jinsi ilivyo vigumu kwa nchi zenye nguvu kama Israeli kuyashinda mashirika dhaifu kama Hamas.
Kwa Hamas, kuishi kwao kunamaanisha ushindi, na Benjamin Netanyahu anajua kwamba, kwake, itakuwa kushindwa.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi