Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ni upi umuhimu wa kimkakati wa Rafah na kwa nini kuna wasiwasi juu ya mashambulizi ya Israeli dhidi yake?
Angel Bermudez
BBC News World
Ni mpaka wa mwisho wa vita huko Gaza na huenda ukawa karibu kufungwa na jeshi la Israel.
Mji wa Rafah wa Palestina umekuwa kimbilio kuu kwa raia na kituo cha kuingizia misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Wapalestina, tangu mwanzo wa mgogoro kati ya Israel na Hamas.
Mji huu upo katika sehemu ya kusini ya Ukanda wa Gaza na ukiwa na kilomita za mraba 55, mji huu ni njia ya mwisho ya kuifikia Gaza ambayo haidhibitiwi na Israeli na umekuwa kwa miongo kadhaa eneo la kuwasili kwa msaada na mlango wa kutokea kwa wagonjwa, majeruhi na wasafiri.
Baada ya kuanza kwa vita vya sasa - vilivyosababishwa na shambulio la kushtukiza ambalo Hamas ilianzisha dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7 ambapo watu 1,200 waliuawa na wengine 240 walitekwa nyara, kwa mujibu wa mamlaka ya Israeli - Rafah ikawa kimbilio la mwisho la Wapalestina zaidi ya milioni moja, ambao wamehamishwa kutoka miji yao kutokana na mashambulizi ya mabomu na uvamizi wa ardhini wa Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF).
Kutokana na kuwasili kwa watu wengi, idadi ya watu wa Rafah iliongezeka kutoka wakazi 280,000 hadi karibu watu 1,400,000, ndiyo sababu imeainishwa na mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Norway, Jan Egeland, kama "kambi kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao duniani".
Lakini hadhi ya mji huu kama kimbilio kwa wale wanaokimbia vita ilianza kuhojiwa mwezi Februari mwaka huu, wakati Israel ilipoanzisha operesheni katika mji huo iliyosababisha vifo vya Wapalestina kadhaa na kuwawezesha mateka wawili kuokolewa.
Wakati huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliagiza Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) kuandaa zoezi la kuwaondoa raia kutoka Rafah, kwa lengo la kuanzisha mashambulizi makubwa huko.
Tangazo hilo lilizua wasiwasi miongoni mwa jamii ya kimataifa, na skuibua ukosoaji na onyo dhidi ya mipango ya Israel, ambayo walihofia itasababisha "janga la kibinadamu."
Hofu hiyo ilizuka tena Jumatatu hii, wakati IDF ilipoanza kusambaza vipeperushi katika mji wa Rafah vilivyokuwa na maelekezo ya watu 100,000 kuhama eneo moja mashariki mwa mji huo na kuelekea Khan Younis na Al-Mawasi.
Saa kadhaa baadaye, IDF ilianza mfululizo wa mashambulizi katika eneo la mji huo katika kile ilichokitaja kama "operesheni ndogo."
Hata hivyo, Rafah na kile kinachotoendelea huko kina umuhimu ambao ni zaidi ya operesheni ya ndani.
"Ngome ya mwisho" ya Hamas
"Haiwezekani kufikia lengo la vita bila kuiondoa Hamas na kuacha vikosi vinne vya Hamas huko Rafah," ofisi ya Netanyahu ilisema katika taarifa mwezi Februari.
Hii ni hoja ambayo rais ameendelea kusisitiza katika miezi hii.
Israel inasisitiza kuwa maelfu ya wapiganaji wa Hamas, pamoja na baadhi ya viongozi wake, wako Rafah.
Inaona kwamba lazima imalize kile inachokadiria kuwa ni batalioni 4 za Hamas zilizopo huko ili kumaliza kampeni yake inayolenga kumaliza nguvu za kijeshi za kundi hilo la Palestina la Gaza.
Inakadiriwa kuwa takriban Waisraeli 200,000 walilazimika kuondoka majumbani mwao baada ya kuanza kwa vita na Hamas na walilazimika kuhamia katika maeneo salama ya nchi hiyo, mbali na maeneo ya mpakani ambako wanaweza kuwa walengwa wa kundi hili au washirika wake wa Lebanon- kundi la wanamgambo wa Hezbollah wa Kishia.
Wengi wa watu hawa walikuwa tayari wameishi kwa miaka mingi chini ya unyanyasaji wa roketi ambazo zilirushwa kutoka Gaza kwenda Israeli mara kwa mara, hali ambayo serikali ya Netanyahu ilionekana kuvumilia kwa muda hadi hatimaye ikajibu kwa shambuliodogo ambao lilisababisha usitishaji mpya wa mapigano.
Hiyo ndiyo hali iliyopelekea mwisho wa shambulio la Oktoba 7, baada ya hapo sio mamlaka ya Israeli wala raia wake wengi wanaona kwamba kuishi na utawala wa Hamas wenye silaha huko Gaza sio hatari inayokubalika tena.
Hata hivyo, tangu kuanza kwa mzozo huo, wachambuzi kadhaa wa kisiasa na kijeshi wameonya kuwa wazo la Netanyahu la kulitokomeza kundi la Hamas ni gumu sana - au haliwezekani kabisa - kufikiwa na kwamba gharama za kbinadamu za kujaribu zitakuwa kubwa sana kutokana na mahandaki ambayo Hamas ilijenga chini ya Gaza kwa ajili ya ulinzi, na pia ukweli kwamba kwa upande wa juu ni vigumu kutofautisha kati ya wapiganaji na raia.
Serikali ya Israel inahakikisha kuwa vikosi vyake vinachukua tahadhari kubwa ili kutowaathiri raia, ambayo haijazuia watu 34,000 kufa Gaza tangu kuanza kwa vita, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kwa mujibu wa wizara ya afya ya ukanda huo, inayodhibitiwa na Hamas.
Mwandishi wa BBC wa masuala ya usalama Frank Gardner ameonya kuwa haijulikani ni nini Israel inaweza kufikia katika operesheni ya kijeshi dhidi ya Rafah.
"Miezi mitano iliyopita ya mashambulio makubwa katika Gaza yameshindwa kufanikisha kuachiliwa huru kwa mateka kwa muda mrefu. Mara ya mwisho idadi kubwa ya mateka walioondoka Gaza wakiwa hai ilikuwa mwezi Novemba na yalikuwa ni matokeo ya mabadilishano, yaliyojadiliwa kwa makini na Qatar na Misri," anasema.
"Jeshi la Israeli linatathmini kwamba vikosi vinne vya Hamas vimenusurika juu na chini ya ardhi huko Rafah na wanataka kumaliza kazi kama walivyopanga. Lakini hata kama watafanikiwa kuharibu vitengo hivi, uwezekano wa mateka kutoroka bila kujeruhiwa ni mdogo," anaongeza.
Uhusika wa siasa na miungano
Kisiasa, kile kinachotokea Rafah kinaweza kuathiri mazungumzo ambayo yamekuwa yakiendelea kwa miezi kadhaa na Hamas, yanayosimamiwa na Qatar na Misri, ili kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, pamoja na kuachiliwa kwa baadhi ya Waisraeli waliotekwa nyara, na Wapalestina waliowekwa kizuizini nchini Israel.
Kwa hakika, Jumatatu hii Hamas ilitangaza kwamba ilikubali pendekezo la silaha, ambalo lilileta baadhi ya maneno ya furaha na faraja miongoni mwa wakazi wa Gaza.
Hata hivyo, wigo wake wa kweli haujawekwa wazi, kwani serikali ya Netanyahu ilisema ilikuwa mbali na kukidhi matakwa ya Israel na kutuma tume ya mazungumzo mjini Cairo.
Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisifu pendekezo hilo ambalo lilikuwa mezani na kusema kuwa ni "ukarimu wa kipekee" kwa upande wa Israel, hivyo Hamas inapaswa kulikubali.
Hata hivyo, wiki hiyo ilipita bila maendeleo katika mazungumzo.
Mbali na vita huko Gaza, kuongezeka kwa mashambulio ya kijeshi ya Israel huko Rafah kunaweza kuongeza mvutano kati ya serikali ya Netanyahu na Marekani.
Rais Joe Biden ameweka wazi kukataa kwake mashambulizi bila kwanza kuwepo kwa mpango wa kulinda raia waliopo huko.
Kwa mujibu wa ikulu ya White House, Biden alithibitisha msimamo wake kwa Netanyahu wakati wa mazungumzo ya simu waliyoyafanya Jumatatu hii.
Mashambulio ya Rafah yanaweza pia kuathiri juhudi za serikali ya Marekani kufikia makubaliano ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israel na Saudi Arabia, ambayo - kwa kweli - tayari iliathiriwa na shambulio la Hamas mnamo Oktoba 7.
Ili kusonga mbele katika njia hiyo, Riyadh ina matumaini kwamba Israel itakubali kumaliza vita na Hamas na kujitolea kufuata njia ambayo inaongoza ya kuundwa kwa taifa la Palestina.
Kurejeshwa kwa uhusiano kati ya Israel na Saudi Arabia kunaonekana kama hatua muhimu sio tu kwa sababu ya athari zake za nchi mbili, lakini kwa sababu nchi zote mbili - kama Marekani - zinaangalia sera ya Iran katika Mashariki ya Kati na mpango wake wa maendeleo ya nyuklia kwa kutoaminiana.
Uhusiano mwingine muhimu ambao unaweza kuharibiwa na mashambulizi dhidi ya Rafah ni ule uliopo kati ya Israel na Misri, ambalo ilikuwa taifa la kwanza la Kiarabu kuitambua Israel.
Tangu kuanza kwa mgogoro wa sasa, serikali ya Abdel Fattah al-Sisi imekuwa na wasiwasi juu ya uwezekano wa kusambaa kwa vurugu za Gaza kutaishia kuwasukuma wapiganaji wa Hamas na viongozi kuelekea Sinai.
Cairo haiangalii kwa upendeleo wanachama wa Hamas, kundi ambalo lilianza kama tawi la Udugu wa Kiislamu wa Misri, na inawachukulia kama tishio kwa usalama wake.
Zaidi ya siasa ni athari za kibinadamu ambayo mashambulizi makubwa ya Israeli huko Rafah yanaweza kuwa nazo.
Katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na sauti nyingi miongoni mwa jamii ya kimataifa ambazo zimeonya kwamba kuna hatari kwamba mamia kwa maelfu ya Wapalestina wanaokimbilia katika mji huo watasukumwa na mashambulizi ya Israeli kuelekea mpaka na Misri. Nchi hiyo imesisitiza mara kadhaa kwamba haina nia ya kuwakaribisha wakimbizi wa Palestina katika ardhi yake.
Frank Gardner wa BBC anachukulia suala hilo kuwa ni jambo la "kutia wasiwasi zaidi". "Israel inakadiria kuwa idadi ya watu wa Gaza ambao wanaweza kuathiriwa (kwa uwezekano wa mashambulizi ya Israeli) kuwa 100,000. Mashirika ya misaada ya Palestina yanasema idadi hiyo inakaribia 250,000. Wengi wa watu hawa tayari wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao kaskazini mwa eneo hilo," anasema.
Ingawa Israel imeitaja operesheni hii kama shambulio dogo dhidi ya malengo maalum ya Hamas huko Rafah, daima kuna hatari ya kuongezeka kwa mapigano.
Kundi la Islamic Jihad, kundi jingine la Wapalestina lenye mafungamano na Hamas huko Gaza, limekuwa likirusha roketi kusini mwa Israel.
Mashambulizi hayo ya Israel pia yameiweka Jordan katika hali ya tahadhari, ambayo ni baada ya Misri kuwa jirani wa pili wa Kiarabu ambayo Israel ilianzisha uhusiano nayo wa kidiplomasia.
Katika mkutano na Biden katika ikulu ya White House, Mfalme Abdullah wa Pili alionya kuwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Rafah yanaweza kusababisha mzozo huo kusambaa katika eneo hilo na kutahadharisha kuwa huenda ukasababisha "mauaji mapya."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi