Kombe la dunia 2022: Pazia la michuano 'tata' zaidi kuanza leo huko Qatar

World cup

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Baada ya miaka 12 ya maswali mengi, ukosoaji na dhana, Kombe la Dunia la Fifa hatimaye linaanza leo Jumapili nchini Qatar. Maandalizi ya mashindano ya kwanza kabisa kufanyika katika nchi ya Kiislamu huko Mashariki ya Kati yamegubikwa na utata na mizozo kadhaa.

Lakini Fifa imeyataka mataifa yote 32 yanayoshindana "kujielekeza kwenye soka" na wenyeji Qatar watafungua dimba dhidi ya Ecuador kwenye Uwanja wa Al Bayt (1:00 usiku kwa saa za Afrika mashariki).

BBC Sport inaangazia utata wa michuano ya mwaka huu na msisimko ulivyo nchini Qatar, na nani anaweza kutwaa Kombe la Dunia.

'Utata gani uliozunguka fainali za mwaka huu?

World cup

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Fifa Gianni Infantino anayatetea mashindano ya mwaka huu

Michuano ya Qatar 2022 inachukuliwa kama moja ya michuano ya Kombe la Dunia linalozungumzwa zaidi na lenye utata katika historia.

Nchi hiyo ya Ghuba ilishinda maombi ya kuandaa michuano hii ikizipiku nchi za Korea Kusini, Japan, Australia na Marekani, lakini kulikuwa na madai ya kuenea kwa rushwa katika mchakato huo, ambayo Qatar imekuwa ikikanusha kila mara.

Mnamo Februari 2021, gazeti la Guardian lilisema wafanyakazi wahamiaji 6,500 kutoka India, Pakistan, Nepal, Bangladesh na Sri Lanka walikufa nchini Qatar tangu iliposhinda zabuni yake ya Kombe la Dunia. Idadi hiyo inatokana na takwimu zilizotolewa na balozi za nchi hizo nchini Qatar.

Hata hivyo, serikali ya Qatar ilisema idadi hiyo ilikuwa ya kupotosha, kwa sababu sio vifo vyote vilivyorekodiwa ni vya watu wanaofanya kazi katika miradi inayohusiana na Kombe la Dunia.

Serikali ilisema rekodi zake za ajali zilionyesha kuwa kulikuwa na vifo 37 vya vibarua katika maeneo ya ujenzi wa viwanja vya Kombe la Dunia kati ya mwaka 2014 na 2020, ni vitatu tu kati yao "vinahusiana na kazi".

Hata hivyo, Shirika la Kazi Duniani (ILO) lilisema hiyo ni dharau. Kumekuwa na hofu juu ya jinsi mashabiki wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja (LGBT) wanavyoweza kutarajia kutendewa ikizingatiwa nchi hiyo inazingatia sheria za Sharia, na mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria nchini Qatar.

Mashirika yanayojihusisha na Fifa kuhusu mchuano huo yamesema "kumekuwa na hatua za polepole" na "bado kuna wasiwasi".

sepp blatter

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sepp Blatter

Sepp Blatter, ambaye alikuwa rais wa Fifa na mtu aliyetangaza kuipa Qatar michuano hiyo mwaka 2010, alisema juma lililopitwa kwamba uamuzi wa kuipa Qatar uenyeji lilikuwa "kosa" kubwa.

Siku moja kabla ya michuano hiyo, rais wa Fifa Gianni Infantino aliyashutumu mataifa ya Magharibi kwa "unafiki" katika ripoti yake kuhusu rekodi ya haki za binadamu ya Qatar.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari huko Doha, Infantino alizungumza kwa karibu saa moja akionekana kuilinda na kuitetea Qatar na mashindano hayo.

Siku 29 kuanzia leo yanapoanza mwisho (Novemba 20 hadi Desemba 18), hili litakuwa Kombe dunia fupi zaidi tangu lile lililofanyika Argentina mwaka 1978.

Mashabiki watarajie nini?

World cup

Chanzo cha picha, Getty Images

Nchi ambayo ina idadi ya watu chini ya milioni tatu, Qatar inatarajia kupokea jumla ya wageni milioni 1.2 kutoka duniani kote katika mashindano haya.

Fifa ilisema karibu tiketi milioni tatu zimeuzwa kwa ajili ya michuano hiyo, huku taifa mwenyeji likiongoza katika orodha ya nchi zilizo na idadi kubwa ya tiketi, karibu asilimia 37 ya mauzo.

Tamasha la Mashabiki katika eneo la Al Bidda limekuwa kivutio likipambwa na taa za rangi zinazomulika juu, huku muziki ukisikika- ingawa hukatishwa kwa dakika kadhaa kila inasikika Adhana (wito kwa sala) kutoka misikiti iliyo karibu.

Pombe haiwezi kunywewa hadharani katika nchi ya Kiislamu, lakini sheria hii imelegezwa kidogo kwa ajili ya mashindano kwani mashabiki wanaweza kununua kinywaji katika maeneo yenye maalumu na sio ndani ya uwanja.

Nani anapigiwa chapuo kutwaa kombe?

World cup

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baadhi ya wachezaji wa Kikosi cha Brazil, wakiwasili Qatar kwa ajili ya mashindano ya kombe la dunia

Brazil haijashinda Kombe la Dunia tangu 2002, ikiwa ndio taifa la mwisho ambalo halitoki Ulaya kubeba kombe hilo.

Kikosi hicho cha Tite kinapigiwa chapuo kushinda taji la sita la michuano hiyo hata na takwimu za Opta.

Lakini Argentina inayonolewa na Lionel Scaloni inashika nafasi ya pili ya kuwa mabingwa kwa mara ya tatu, ikiingia katika mashindano haya baada ya kucheza michezo 36 mfululizo bila kufungwa.

Waingereza wanaonolewa na Gareth Southgate wamekuwa na kiwango kibovu katika wakati usiofaa, wakiwa hawajashinda katika michezo sita iliyopita wanatarajiwa kupiga hatua moja zaidi kutoka ile ya nusu fainali miaka minne iliyopita.

Orodha ya majeruhi inazidi kuongezeka

World cup

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Benzema, kuikosa michuano ya mwaka huu kwa kuumia

Fainali za mwaka huu zinamkosa mchezaji bora wa dunia wa mwaka huu. Inamkosa mmoja wa nyota wakubwa, mshambuliaji wa Ufaransa Karim Benzema ambaye usiku wa kuamkia leo, iliumia paja mazoezini.

Mshambulizi wa Senegal Sadio Mane pia atakosekana kwenye viwanja vya Qatar. Mchezaji huyo wa zamani wa Liverpool amefanyiwa upasuaji wa jeraha la goti alilopata akiichezea Bayern Munich siku 10 tu kabla ya mechi ya ufunguzi.

Benzema na Mane wanaungana na wachezaji wengine waliotarajiwa kuwepo, akiwemo Paul Pogba (Ufaransa), Timo Werner (Ujerumani), Reece James (England), Diogo Jota (Ureno) na Giovani Lo Celso (Argentina) ambao wanakosekana kwa sababu ya kuumia.

Mshambulizi wa Manchester City Erling Haaland na Mohamed Salah wa Liverpool ni wachezaji wawili wakubwa ambao hawatacheza michuano ya mwaka huu kwa vile nchi zao hazijafuzu.

Skip Unaweza kusoma pia and continue readingUnaweza kusoma pia

End of Unaweza kusoma pia