Ukraine: Imekuwa vigumu kupata watu wa kwenda vitani

fdvc

Chanzo cha picha, Sarah Rainsford/BBC

    • Author, Sarah Rainsford
    • Nafasi, BBC
  • Iliyochapishwa

Kamanda Pavlo Zhilin na kikosi chake cha doria wanapoonekana kwenye mitaa ya Cherkassy, ​​​​watu mara nyingi hubadilisha njia ili kuwakwepa.

Pavlo ni afisa wa jeshi anayetafuta askari kwa ajili ya jeshi la Ukraine. Miaka miwili baada ya Urusi kuivamia Ukraine kwa kiasi kikubwa, hakuna watu wanaojitolea kwa wingi kwenda vitani.

Wale wanaotaka kupigana wamefariki, wamejeruhiwa, au wamekwama mstari wa mbele wakingojea kupumzika kidogo ili kuwapisha wapiganaji wapya wanaowasili.

Shauku kama ile ya siku za kwanza ya kwenda vitani imepungua, si rahisi sasa kuwapata watu katika mitaa ya Cherkassy wanaotaka kwenda vitani, ​​hali ni sawa na hiyo katika maeneo mengine.

Ukraine imechoka

fdc

Chanzo cha picha, Sarah Rainsford/BBC

Maelezo ya picha, Pavlo alipoteza mkono wake huko Bahmut

''Watu wanaona kana kwamba vita viko mahali fulani mbali. Lakini huu ni uvamizi na watu hawaonekani kujali," anasema Pavlo.

"Tunahitaji watu waungane, kama vile siku ya kwanza. Tuungane kama ndugu."

Huduma ya usalama ya Cherkassy huzima akaunti za mitandao ya kijamii zinazowatahadharisha watu wakati timu ya uhamasishaji inapokuwa mitaani.

Akiwa na umri wa miaka 24, Pavlo alijitolea kwa ajili ya nchi yake. Februari 2022, alikuwa akitumikia jeshi wakati vikosi vya Urusi vikikusanyika kwenye mpaka.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Alipigana karibu ya Kiev, na kisha huko Donbas, ambapo vita visivyo na huruma vilipiganwa. Katika majira ya joto ya mwaka huo, alihamishiwa Bahmut.

"Tulishambuliwa kwa makombora. Nilipoteza mkono wangu," anaelezea shambulio lililomjeruhi vibaya. Alijipenyeza chini ya vichaka na kuanza kuomba msaada.

Askari huyo anakiri kwamba kufika hospitali alihisi kama mzigo: si tu kwa sababu alikuwa ameokolewa, lakini kwa sababu alikuwa mbali na mstari wa mbele.

Majeraha ya Pavlo yalikuwa makubwa. Mkono wake wa kulia ulikatwa chini ya bega. Bado anahisi maumivu. Lakini bado alitaka kuendelea kuhudumu, hivyo akawa afisa wa uhamasishaji.

Baada ya yote aliyopitia, nashangaa kwa nini wanaume wengine wanakwepa kwenda vitani.

"Siku moja, watoto wao watawauliza walichokuwa wakifanya wakati wa vita. Watajibu, 'nilikuwa nimejificha," anasema Pavlo.

Ukraine imelipa gharama kubwa kwa ajili ya kujilinda.

Pavlo alipoulizwa ikiwa amepoteza marafiki wowote katika vita, anasema "wale marafiki wa karibu, hakuna aliyeachwa. Wengine ni kama mimi [wamejeruhiwa]. Wengine wamekufa."

Serhiy

jhn

Chanzo cha picha, Sarah Rainsford/BBC

Maelezo ya picha, Serhiy alijeruhiwa katika vita

Mji wa Irpin, karibu na Kyiev, ulichukuliwa na vikosi vya Urusi mwanzoni mwa vita. Kuna majengo yaliyoharibiwa na mabaki ya makombora kila mahali, pamoja na sauti za ujenzi.

Kwa wale ambao wamepoteza kila kitu. Sasa wanaishi kwenye nyumba ya vyumba viwili na bafu katika nyumba zilizojengwa. Nusu ya watu wanaoishi hapa ni wakazi wa Irpin wenyewe. Wengine walihamia kutoka maeneo ya karibu.

Lilia Saviuk na mumewe wamehamia hapa kutoka Kakhovka mashariki, ambayo bado iko chini ya vikosi vya Urusi.

Mwanzoni mwa vita, mtoto wao Serhiy alitekwa huko Irpin na kuwekwa kwenye chumba cha chini ya ardhi. Lilia anasema aliteswa.

Serhiy alipoachiliwa, aliondoka eneo hilo na mara moja akajiunga na jeshi ili kupigania Ukraine.

Wakati Lilia anatazama simu yake kunionyesha picha, picha za majeraha ya kutisha zinaonekana. Mguu mmoja wa mwanawe ulikatika vipande, na vikaanguka chini.

Serhiy alijeruhiwa huko Avdeeyevka, mapigano makali yalizuka na hata maafisa wa Ukraine walikiri kwamba jeshi lilikuwa na silaha duni na upungufu wa wanajeshi.

Lilia na mume wake hawakuweza kuondoka Kakhovka kwa sababu wazazi wao wazee walikataa kuondoka nao. Kwa hivyo, walibaki na waliishi kwa hofu kwamba Warusi wangegundua kwamba mtoto wao alikuwa askari.

Hatimaye waliondoka eneo hilo kwenda kukaa na Serhiy hospitalini akiwa amejeruhiwa, lakini Lilia analia kwamba anaona aibu amewaacha wazazi wake peke yao.

kjm

Chanzo cha picha, Sarah Rainsford/BBC

Maelezo ya picha, Mama wa Serhiy anasema madaktari "walifanya miujiza".

"Tunawapigia simu na kuwauliza hali zao."

Ananionyesha video; akisukuma kiti cha magurudumu cha mwanawe. Wote wawili wanacheka kwenye theluji. Pia kuna picha za makovu kwenye ngozi ya mwanawe. Liliana anasema madaktari "walifanya miujiza."

Hata hivyo, Serhiy alimwambia mama yake kwamba atarudi vitani baada ya kupona. Alisema kuna ukosefu wa askari huko. Rafiki zake wanamuhitaji.

“Nadhani tayari ameshatimiza wajibu wake,” anasema Liliana huku machozi yakimtoka.

"Kama mama, ni dhambi kusema hivyo, lakini naweza kulala vizuri akiwa hospitali. Siwezi kulala akiwa mstari wa mbele."

"Nafurahi mwanangu yuko hospitalini sasa, ingawa sitakiwi kusema hivyo. Nafurahi kuwa hayuko mstari wa mbele."

Vladislav

k,

Chanzo cha picha, Sarah Rainsford/BBC

Maelezo ya picha, Mtoto wa Irina alifariki katika mlipuko wa bomu la chini ya ardhi

Nje kidogo ya Cherkassy kuna safu ya makaburi mapya. Makaburi haya ni ya wanajeshi wa rika mbalimbali kutoka mji huu waliofariki katika vita.

Ukraine inawachukulia waliokufa kama mashujaa, lakini maombolezo yameachwa kwa familia zao.

Bendera ya taifa inaning'inia katika kila kaburi na zimepambwa kwa maua. Picha za askari na maafisa waliovalia sare za kijeshi zimewekwa kwenye misalaba au kuchongwa kwenye mawe ya marumaru.

Irina bado hawezi kuweka picha ya mtoto wake kwenye kaburi lake. Picha aliyoitumia kwenye mazishi ya mtoto wake bado ipo nyumbani. Hayuko tayari kwa hilo.

Vladislav Baykanov aliuawa katika mlipuko karibu na Bakhmut Juni 2023. Ni kijana ambaye bado alikuwa hajafikisha umri wa miaka 23.

"Ninaamini mwanangu alikufa akifanya jambo lililo sawa," Irina anasema. Binti yake amesimama karibu naye na kulia kimya kimya.

"Mimi ni mwalimu na huwa nawaambia wanafunzi wangu; tuko sahihi, tunalinda nchi yetu na watoto wetu. Mwanangu alitulinda," anasema Irina.

"Litakuwa jambo baya zaidi tukifanywa watumwa na Urusi. Ni ngumu sana. Lakini hakuna kurudi nyuma. Hatuwezi kukata tamaa," anaongeza.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah