Je! unavijua ‘vikosi vya adhabu’ vya Urusi vinavyopigana Ukraine?

WEQDASX

Chanzo cha picha, AFP

Iliyochapishwa

Kikosi hicho kina mamia ya wahalifu na wanajeshi na raia ambao waliingizwa katika vikosi vya adhabu vya Urusi vinavyoitwa Storm-Z (SZ) na kupelekwa mstari wa mbele nchini Ukraine.

Wapiganaji katika vitengo hivi walizungumza na shirika la habari la Reuters. Wachache wao wamesimulia maisha yao.

"Wapiganaji hao wana viwiliviwili tu lakini hawana akili," mwanajeshi aliyetumwa karibu na jiji la Bakhmut mashariki mwa Ukraine, aliiambia Reuters mwezi Mei.

Anasema alitoa matibabu kwa wapiganaji sita au saba wa kikosi hicho waliojeruhiwa.

Askari huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa sababu anaogopa kufunguliwa mashtaka nchini Urusi kwa kuzungumzia vita hivyo , alisema anasikitikia masaibu ya watu hao:

"Kama makamanda watamkamata askari yeyote akinuka pombe, mara moja wanampeleka SA."

Shirika la Habari la Reuters, ambalo lilichapisha ripoti ya kina kuhusu vikosi hivi, lilisema kwamba lilipowasiliana na afisa katika Kitengo Namba 40318, alikataa kuzungumzia suala la vikosi vya SA na akakata simu.

Vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na serikali ya Urusi viliripoti kuwepo kwa vikosi hivyo, wapiganaji wao walishiriki katika vita vikali na baadhi walipokea medali za ushujaa, lakini hawakufichua jinsi vikosi hivyo vinavyoundwa.

Reuters ilikuwa ya kwanza kuandika ripoti ya kina kuhusu jinsi vikosi hivi vinavyoratibiwa na kupelekwa mstari wa mbele, kwa kuzungumza na vyanzo vingi.

edcsx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vikosi vya adhabu vinajumuisha wafungwa wanaoahidiwa msamaha
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika kitengo nambari 40318, wapiganaji 13 waliohojiwa - ambao wanne ni kutoka kikosi cha SA, askari watatu kutoka vitengo vya kawaida – wote waliomba kutotajwa majina, kwa sababu ya hofu.

Reuters ilithibitisha utambulisho wa wapiganaji wote wanaoshiriki katika vikosi hivyo kwa kutumia rekodi za uhalifu, akaunti za mitandao ya kijamii, au kwa kuzungumza na wanajeshi wenzao na familia zao.

Vikosi vya Adhabu, kila kimoja kina wanajeshi 100 hadi 150 na kujumuishwa katika vitengo vya kawaida vya jeshi, kwa kawaida hupelekwa katika maeneo hatarishi zaidi na mara nyingi hupata hasara kubwa, kulingana na mahojiano ya Reuters na watu ambao waliwajua angalau wapiganaji watano wa vikosi hivyo.

Wapiganaji watatu kati ya watano wa Storm Z waliohojiwa na Reuters, na jamaa wa wapiganaji wengine watatu, walielezea mapigano ya kutisha ambayo yalisababisha kuuwawa kwa wenzao.

Mpiganaji mmoja, aliyepatikana na hatia ya wizi na kuandikishwa kutoka gerezani, alisema kwamba wanaume wote isipokuwa 15 kati ya 120 katika kitengo chake kilichounganishwa na Kikosi cha 237 waliuawa au kujeruhiwa katika mapigano karibu na mji wa Bakhmut mnamo Juni.

Kutumwa kwa timu kama hizo kunaashiria kuondoka kwa kundi la mamluki la Wagner - ambalo sasa limesambaratishwa baada ya uasi wa Juni - lilituma wafungwa kupigana kwenye mstari wa mbele, vitengo vya SA viko chini ya amri ya moja kwa moja ya Wizara ya Ulinzi.

Waliohojiwa walisema vikosi hivi vinajumuisha wafungwa wanaojitolea kupigana kwa ajili ya ahadi ya msamaha, na askari wa kawaida wanaoadhibiwa kwa ukiukaji wa nidhamu.

SZ ni muhimu kwa Wizara ya Ulinzi ya Urusi kwa sababu wanaweza kutumwa kama vikosi vya askari wachanga, kulingana na shirika huru linalofuatilia vita ambalo lilianzishwa nchini Urusi.

"Wapiganaji hao hutumwa kwenye sehemu hatari zaidi katika ulinzi na mashambulizi."

Ingawa Wizara ya Ulinzi ya Urusi haijawahi kukiri kuundwa kwa askari hao, ripoti za kwanza za kuwepo kwao ziliibuka mwezi Aprili wakati Taasisi ya Utafiti wa Vita, nchini Marekani, ilitaja kile ilichosema ni ripoti ya kijeshi ya Urusi iliyovuja.

Reuters haikuweza kubaini idadi ya wanajeshi wanaohudumu katika vikosi hivyo, lakini mahojiano na watu wanaofahamu suala hilo yanaonyesha kuwa kuna angalau wapiganaji mia kadhaa kwa kila kikosi.