Africa Eye: BBC yaoneshwa ushahidi kuwa vikosi maalum vya Afrika Kusini vilimuua mpelelezi mkuu

    • Author, Yeshiel Panchia
    • Author, Dino Mahtani
    • Author, Nick Norman-Butler
    • Nafasi, BBC Eye Investigations
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Mpelelezi mwandamizi wa polisi, Frans Mathipa, alikuwa amepambana kwa muda wa miezi minne ili kupata taarifa muhimu sana katika kesi aliyokuwa akiichunguza. Hatimaye, aliambiwa kuwa taarifa hiyo ilikuwa karibu kufikishwa kwake.

Lakini alihofia kwamba jitihada zake za kuipata zingeweza kugharimu maisha yake.

Siku mbili baadaye, gari lake lilikutwa limepinduka, alikuwa amepigwa risasi na kuuawa akiwa anaendesha.

Sasa, maafisa saba wa vikosi maalum vya Afrika Kusini, pamoja na afisa mmoja wa kijeshi, wamefunguliwa mashtaka ya kumuua Luteni Kanali Mathipa, afisa aliyekuwa akiheshimiwa sana, mnamo Agosti 2023. Wamekanusha mashtaka hayo.

Hakuna tarehe ya kusikilizwa kwa kesi yao, na kuna hofu kwamba kesi hiyo huenda ikachelewa kuanza. Hii ni kwa sababu wanaume watatu kati ya wanaoshtakiwa kwa mauaji wamekataa kutii amri ya mahakama iliyowanyang'anya dhamana.

Bado wanaendelea kufanya kazi katika vikosi maalum vya jeshi, na mmoja wao hata amepandishwa cheo.

Pia tumezungumza na vyanzo muhimu vilivyohusika katika uchunguzi wa polisi, akiwemo aliyekuwa mkuu wa zamani wa kitengo cha kupambana na ugaidi ndani ya The Hawks, kamanda wa Mathipa, pamoja na familia ya Mathipa, ili kujenga maelezo ya kina zaidi yaliyowahi kuwekwa wazi kuhusu matukio yaliyosababisha kifo cha mpelelezi huyo.

Taarifa hizo zinatoa ushahidi mzito unaoashiria kwamba vikosi maalum vya Afrika Kusini vinahusika na mauaji yake.

Hasa, nyaraka za polisi zinaonesha kwamba gari lililokuwa likimfuatilia Mathipa muda mfupi kabla ya kupigwa risasi lilikuwa limesajiliwa kwa kampuni ya kificho iliyohusishwa na vikosi maalum. Pia, taarifa za ufuatiliaji zilizopatikana ndani ya gari hilo zinaonesha kwamba gari lilikuwa eneo la tukio hilo la shambulizi la risasi.

Mmoja wa watu waliokuwa ndani ya gari hilo, Meja Sunnybooi Wambi, pia alionekana katika eneo la tukio la utekaji nyara unaodaiwa kufanywa na wanajeshi wa vikosi maalum, ambao ulikuwa ndio kesi ambayo Mathipa alikuwa akiichunguza, kwa mujibu wa nyaraka hizo.

Baada ya kifo cha Mathipa, vikosi maalum vilitoa onyo la kutisha kwa The Hawks, kulingana na nyaraka za polisi.

"Mnaweza kuteua maafisa 10 wa uchunguzi; tutawaua wote," polisi walisema ndilo lilikuwa onyo hilo.

Kesi ambayo Mathipa alikuwa akiichunguza ilikuwa nyeti sana.

Ilihusu raia wa Ethiopia aitwaye Abdella Abadigga, ambaye alidaiwa kuwa mpiganaji wa kundi linalojiita Islamic State (IS). Alikuwa amepewa hifadhi ya muda nchini Afrika Kusini mwaka 2008, lakini alikamatwa nje ya nchi mwaka 2017.

Baadaye, Abadigga alisafirishwa kwa siri kurudishwa Afrika Kusini na jeshi la Afrika Kusini pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani, ili atumike kama chanzo cha taarifa za kijasusi, lakini baadaye "alianza kujifanyia mambo yake mwenyewe", kwa mujibu wa Kanali Tollie Vreugdenburg, aliyekuwa mkuu wa zamani wa kitengo cha kupambana na ugaidi katika The Hawks.

Vyanzo kutoka jamii ya Waethiopia huko Johannesburg vilituambia kwamba Abadigga aliendelea kuwanyanyasa na kuwatoza fedha kwa nguvu watu katika eneo hilo la Waethiopia mjini Johannesburg. Serikali ya Marekani inasema fedha hizo zilitumika kufadhili IS.

Tuliliuliza Jeshi la Afrika Kusini ikiwa lilisaidia kuwezesha kurejea kwa Abadigga nchini humo. Pia tuliuliza Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwa ilitoa taarifa ya uongo kuhusu mpango wa kumrudisha Abadigga Ethiopia, huku kiuhalisia ikimsafirisha kwa siri kurudi Afrika Kusini akitumia pasipoti na kibali cha ukimbizi vilivyokuwa vimekwisha muda wake. Hakuna hata moja kati ya taasisi hizo iliyojibu.

Kwa hakika, Mathipa alikuwa akichunguza madai kwamba baadaye vikosi maalum vilimteka na kumuua Abadigga mnamo Desemba 2022. Mapema mwaka huo, Marekani ilikuwa imemuweka Abadigga chini ya vikwazo, ikimtaja kuwa mtafutaji na mkusanyaji wa fedha kwa ajili ya IS, pamoja na kuwa msaidizi wa karibu wa Bilal al-Sudani, mmoja wa viongozi wakuu wa IS nchini Somalia.

Nyaraka za mahakama zinaonesha kwamba baada ya Abadigga kutekwa, simu yake iliunganishwa na mnara wa mawasiliano uliokuwa karibu na kituo cha kijeshi. Vyanzo vya polisi vinasema simu hiyo ilitumika kupiga namba iliyokuwa nchini Somalia.

Pentagon haikujibu swali la BBC kuhusu ikiwa simu ya Abadigga ilisaidia kubaini mahali alikokuwa al-Sudani, ambaye aliuawa na vikosi maalum vya Marekani nchini Somalia mnamo Januari 2023, wiki chache tu baada ya Abadigga kudaiwa kutekwa.

Pia tulimuuliza Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ikiwa Abadigga alitekwa kwa agizo la Marekani. Alikataa kuzungumza.

Mathipa alipopewa jukumu la kuchunguza kesi hiyo, miezi minne kabla ya kuuawa kwake, tayari alijua kwamba vikosi maalum vilihusishwa na tukio hilo, lakini alikuwa akijaribu kupata ushahidi zaidi.

Alikuwa akiendeleza taarifa ambazo tayari zilikuwa zimekusanywa na kaka yake Abadigga, Ameen. Ameen alikuwa amefungua kesi ya mtu kupotea muda mfupi baada ya Abadigga kutoweka, na polisi wa eneo hilo walikuwa wamemteua afisa wa uchunguzi kushughulikia kesi hiyo.

Ameen pamoja na afisa huyo wa uchunguzi walipata picha za video za usalama,(CCTV) zilizoonesha shughuli zake za mwisho za Abadigga na mlinzi wake, Kadir Abotese, katika Mall of Africa, duka kubwa la manunuzi lililo pembezoni mwa Johannesburg.

Video hizo, ambazo BBC imeziona, zinaonesha mwanaume aliyevaa shati la buluu akimfuata Abadigga na mlinzi wake walipotoka kwenye eneo la migahawa kuelekea maegesho ya magari. Mwanaume huyo alilipa ada ya maegesho sekunde tatu tu baada ya Abadigga na Abotese kufanya hivyo.

Video ya CCTV ya kituo hicho cha ununuzi ina dokezo jingine muhimu sana: namba za usajili wa magari yaliyoshukiwa kutumiwa na watekaji nyara zinaonekana wazi.

Communications Trust (PCT), ambayo Ameen na afisa wa uchunguzi walikuja kugundua kuwa ilikuwa kampuni ya kificho ya vikosi maalum vya Afrika Kusini.

Wakati Abadigga alipopotea, miongoni mwa wakurugenzi wa PCT alikuwa Meja Jenerali Herbert Mashego, ambaye wakati huo alikuwa kamanda wa 5 Special Forces Regiment.

Nyaraka za polisi zinasema kwamba mkutano ulipangwa kati ya afisa wa uchunguzi na maafisa wa vyeo vya juu jeshini, akiwemo Brigedia Jenerali Yalo, ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa vikosi maalum.

Katika mkutano huo, afisa wa uchunguzi aliagizwa kumwambia Ameen kwamba hakukuwa na uhusiano wowote kati ya PCT na jeshi.

Kwa hiyo, uchunguzi ulipoonekana kufikia mwisho, kaka yake Abadigga alipeleka kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Johannesburg.

Katika kujibu hatua ya kisheria iliyochukuliwa na Ameen, vikosi maalum vilikana kuwa na taarifa yoyote kuhusu Abadigga au alikokuwa. Hata hivyo, vilikiri kwamba wanajeshi wao walikuwa Mall of Africa siku hiyo, lakini vikadai kwamba walikuwa huko kwa ajili ya mazoezi ya kijeshi.

Vilimtaja mwanaume aliyeonekana kwenye CCTV akiwa amevaa shati la buluu kuwa Meja Sunnybooi Wambi, na kusema kwamba alikuwa kamanda wa zoezi hilo. Pia walikiri kwamba magari yote yaliyokuwa yakishukiwa kuhusika na tukio hilo katika kituo hicho cha biashara yalikuwa mali yao.

Operesheni za ndani zinazofanywa na jeshi la Afrika Kusini zinahitaji idhini kutoka kwa serikali pamoja na ofisi ya urais.

Tulimuuliza aliyekuwa Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Afrika Kusini, Thandi Modise, na Rais Cyril Ramaphosa, ikiwa waliidhinisha zoezi la mafunzo lililofanyika Mall of Africa. Modise hakujibu, huku Ramaphosa akikataa kuzungumzia hilo.

Mwezi mmoja baadaye, Mathipa alipopewa jukumu la kuchunguza kesi hiyo, alitoa amri rasmi ya mahakama kwa vikosi maalum, akiwataka kuwasilisha maelezo kamili kuhusu zoezi hilo la mafunzo lililodaiwa kufanyika, pamoja na majina ya wanajeshi wote waliohusika.

Miezi mitatu baadaye, hatimaye alipoahidiwa kwamba atapewa fursa ya kuzifikia nyaraka hizo, Mathipa alipata hisia kwamba atauawa, kwa mujibu wa kamanda wake, Brigedia Paulina Sekgobela.

"Alipotoka ofisini kwangu alisema: 'Brigedia, unajua, watu hawa wataniua. Nitakufa,'" aliieleza BBC.

Siku ambayo Mathipa aliuawa, alipigiwa simu na mwanaume aliyejitambulisha kwa jina la Tebogo, ambaye alidai kuwa alikuwa na taarifa kuhusu kesi hiyo kwa ajili ya mpelelezi huyo. Hayo ni kwa mujibu wa binti wa Mathipa, Basetsana, ambaye wakati huo alikuwa nyumbani pamoja naye.

Mathipa na Tebogo walikubaliana kukutana katika kituo cha mafuta mjini Pretoria.

Tebogo aliposhindwa kufika, Mathipa aliendelea kuendesha gari, akiondoka eneo hilo kupitia barabara kuu.

Alipigwa risasi na kuuawa akiwa anaendesha gari. Polisi wa Afrika Kusini wanasema risasi hizo zilirushwa kwa silaha zenye nguvu kubwa za moto, aina ya silaha ambazo vikosi maalum vilikuwa na uwezo wa kuzipata.

Polisi pia wanasema picha kutoka kwenye vituo vya malipo ya ushuru barabarani zinaonesha kwamba mmoja wa watu waliokuwa ndani ya BMW nyeusi iliyokuwa ikimfuatilia Mathipa muda mfupi kabla ya kuuawa kwake alikuwa Meja Sunnybooi Wambi.

Wanaongeza kwamba gari hilo, kama ilivyokuwa kwa magari matatu yaliyohusishwa na kutoweka kwa Abadigga katika Mall of Africa, lilikuwa limesajiliwa kwa PCT.

Baada ya kifo cha Mathipa, wapelelezi wapya walipewa jukumu la kuendelea na uchunguzi. Hatua hiyo ilisababisha ujumbe mwingine wa kutisha kutoka kwa vikosi maalum, ambao ulifika katika kitengo cha ujasusi wa makosa ya jinai cha polisi.

Polisi wanasema ujumbe huo ulionya kwamba, bila kujali idadi ya maafisa watakaoteuliwa kuchunguza kesi hiyo:

"Tutawaua wote."

Kwa jumla, wanajeshi 12 wa Afrika Kusini wamekamatwa, akiwemo Luteni Kanali Sunnybooi Wambi, pamoja na mkuu wa sasa wa vikosi maalum vya Afrika Kusini, Brigedia Jenerali Solomon Lechoenyo. Wote wawili walipandishwa katika nafasi hizo baada ya polisi kuanza kuchunguza nafasi zao katika kesi hiyo.

Watu hao 12 wamefunguliwa mashtaka mbalimbali yanayohusiana na kutekwa na kuuawa kwa Abadigga na Abotese, mauaji ya Mathipa, udanganyifu, na kuzuia uchunguzi wa haki.

Wote wanakanusha mashtaka yote, na awali waliachiliwa kwa dhamana. Hata hivyo, baadaye dhamana ya watu sita kati yao ilifutwa, na wakaamriwa kujisalimisha kwa mamlaka na kuwekwa chini ya ulinzi.

Watatu kati ya hao sita, akiwemo Wambi, wamefunguliwa mashtaka ya mauaji ya Mathipa, pamoja na kutekwa na kuuawa kwa Abotese.

Jeshi limekataa kuwakabidhi kwa mamlaka za kisheria.

Mwezi Julai, mawakili wao walitaja matibabu ya afya ya akili kama sababu ya kutokuwepo kwao. Miaka mitatu baada ya kuuawa kwa Mathipa, hakuna tarehe ya kuanza kwa kesi iliyowekwa.

Wakati huohuo, mwili wa Abadigga haujawahi kupatikana.

"Mathipa alikuwa akifuatilia njia sahihi. Alikuwa akimkabili mtu mwenye nguvu anayehusika," anasema Vreugdenburg akimzungumzia mpelelezi huyo aliyefariki.

Binti wa Mathipa, Basetsana, anaeleza kwa uchungu:

"Tunataka haki. Sitamwona tena baba yangu... Kwa nini baba yangu? Kwa sababu alikuwa anafanya kazi yake."