Wachezaji watano hatari waliosajiliwa Ligi Kuu ya Uingereza msimu huu

Iliyochapishwa

Klabu za ligi ya Premia zimetumia zaidi ya pauni bilioni moja (dola bilioni 1.3) kununua wachezaji wapya kabla ya kuanza kwa msimu mpya siku ya Ijumaa.

Arsenal wameongoza kwa kutumia zaidi ya pauni milioni 200 kununua Declan Rice, Kai Havertz na Jurrien Timber huku wakilenga kuwaangusha mabingwa watetezi Manchester City.

Manchester United, Newcastle, Liverpool na Chelsea pia zimekuwa zikikabiliana na ushindani mkali wa kumaliza katika nafasi nne za juu.

Lakini washindi mara tatu City wanasalia kuwa timu kali huku wakisaka taji la kihistoria la ligi kuu ya Uingereza kwa mara ya nne mfululizo.

AFP inaangazia uhamisho mkubwa zaidi wa wachezaji watano kwenye kipindi kirefu cha usajili :

Declan Rice (Arsenal)

Arsenal walikuwa wapinzani wa kushtukiza wa City kwa ubingwa msimu uliopita huku The Gunners wakiwa kileleni kwa muda mwingi wa kampeni kabla ya kushuka katika kipindi cha mwisho cha ligi.

Mpango wa Rice kujiunga na vijana wa Mikel Arteta licha ya kuripotiwa kutakiwa na City ilikuwa dalili nyingine kwamba Arsenal ni timu iliyo juu.

Arsenal ilibidi kuvunja rekodi yao ya uhamisho kwa dau ambalo linaweza kupanda hadi pauni milioni 105 kumzawadia mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza kutoka West Ham.

Pamoja na ada hiyo kuna matarajio makubwa kwa Rice kuthibitisha kwamba ataleta tofauti katika kumaliza subra ya miaka 20 kurudisha taji la Ligi Kuu la Uingereza kaskazini mwa London.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ana jukumu la kuendesha safu ya kiungo cha kati huko Emirates na kutoa fursa kwa washambuliaji wachanga wenye vipaji kushambulia mbele

Rasmus Hojlund (Man Utd)

Harakati za kumsajili nahodha wa England Harry kane Old Trafford hazikufua dafu na badala yake United ikamsajili mchezaji wa Denmark mwenye umri wa miaka 20 Hojlund ili kukimu mahitaji ya mshambuliaji.

Ada ya awali ya pauni milioni 64 kwa mchezaji aliyeigharimu Atalanta pauni milioni 17 tu mwaka mmoja uliopita imeibua hisia.

Hojlund alifunga mabao tisa katika msimu wake wa kwanza Serie A.

Lakini mabao yake sita katika mechi sita alizoichezea nchi yake yameonyesha mwanga wa uwezo wake.

Mwili mzuri, kasi ya juu na mizizi ya kutoka Scandinavia imemfanya Hojlund alinganishwe na nyota wa City Erling Haaland.

Josko Gvardiol (Man City)

Uhamisho mkubwa wa City umekuwa kwa beki wa kati wa Croatia Gvardiol katika dili kutoka RB Leipzig lenye thamani ya pauni milioni 78.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alishiriki katika harakati za taifa lake hadi nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka jana.

Hata hivyo, anakabiliwa na ushindani mkali Etihad huku Pep Guardiola akiwa na mabeki sita wa kati wa kimataifa wa kuchagua na kusisitiza kwamba hiyo "sio wengi sana" kwani mara nyingi alikuwa akichezesha beki wanne wa kati mwishoni mwa msimu uliopita.

Dominik Szoboszlai (Liverpool)

Kwa Liverpool kumaliza katika nafasi ya kukatisha tamaa msimu uliopita kulifichua hitaji la marekebisho ya safu ya kati iliyozeeka.

Szoboszlai na mshindi wa Kombe la Dunia wa Argentina Alexis Mac Allister wanaleta ahadi ya nguvu zaidi na tishio la magoli lakini uimarishaji zaidi unahitajika ili kuangazia kuondoka kwa nahodha Jordan Henderson, Fabinho, Alex Oxlade-Chamberlain, Naby Keita na James Milner.

Mchezaji wa kimataifa wa Hungary Szoboszlai pia anawasili Uingereza kutoka Leipzig kwa mkataba wa pauni milioni 60.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alifunga mabao 20 na kutoa asisti 22 katika mechi 91 kwa upande wa Ujerumani.

Sandro Tonali (Newcastle)

Fedha nyingi zinazotolewa na klabu za ligi ya Saudia zimekuwa tishio kwa klabu kuu za ligi ya Premia katika miezi ya hivi karibuni.

Hatahivyo hamu ya ligi hiyo ya Gulf kuwalenga wachezaji wa ligi ya Premia imezua hisia zaidi ya ilivyotarajiwa.

Wakiungwa mkono na hazina ya utajiri wa Saudia, Newcastle wamekataa katakata kishawishi cha kuashiria kurejea kwao Ligi ya Mabingwa kwa bila wachezaji wenye majina makubwa.

Klabu hiyo iliweka rekodi ya pauni milioni 60 kwa mchezaji wa Italia Tonali kutoka AC Milan.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23, alisaidia mashujaa wake wa ujana kunyakua taji la kwanza la Serie A kwa miaka 11 mnamo 2022 kabla ya kucheza nafasi muhimu katika kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.