Serikali ya Tanzania yavikosoa vyombo vya habari vya kimataifa

.

Chanzo cha picha, Gerson Msigwa

Maelezo ya picha, Gerison Msigwa , msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Msemaji wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa amevikosoa vyombo vya habari vya nje akivitaka kufuata maadili na misingi ya uandishi wa habari.

Msemaji huyo wa serikali ambaye alikuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar Es Salaam amevitaja vyombo vya habari vya CNN, Aljazeera, BBC na DW akisema kwamba vimekuwa vikichapisha habari za upande mmoja zenye nia ovu kwa Tanzania.

'Sio haki kwa vyombo vya habari kuchapisha habari za upande mmoja na baadaye kusema kwamba maafisa wa serikali walipotafutwa hawakupatikana', alisema msigwa, akizitaka kuchapisha taarifa zinazozingatia 'usawa, haki na uwajibikaji.'

Msigwa hususan amekitaja chombo cha habari cha CNN kama kilichokiuka maadili kwa kuchapisha habari zilizojaa 'tuhuma' dhidi ya serikali bila kutoa nafasi kwa serikali kujibu.

Aliitaka idhaa hiyo ya Marekani kuwasiliana na serikali kwa lengo la kuchapisha maudhui ya ukweli, akitaja sera ya wanasheria ya 'principle of natural Justice' inamaanisha kwamba huwezi kuandika habari za kumtuhumu mtu bila kumpatia mtu huyo fursa kujitetea.

'Natoa wito kwa CNN waje upande wa serikali wachapishe maudhui ya ukweli, waache kuchapisha habari za upande mmoja'. Aliongezea Msigwa.

'Walichofanya CNN pia kilifanywa na BBC, DW na Aljazeera na sio haki', alisema Msigwa.

'Tutazungumza na vyombo vya kimataifa, tutavipatia nafasi kuja kwetu na kujieleza nasi tujieleze'

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Matamshi yake yanajiri kufuatia ripoti za mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania ambao Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi kwa karibia asilimia 98 ya kura.

Licha ya kubinywa kwa mtandao uliovizuia vyombo vya habari nchini humo kuandika taarifa za yale yaliotokea wakati wa Uchaguzi huo, vyombo vya kimataifa vilifanikiwa kuandaa taarifa za ghasia hizo za uchaguzi hatua ambayo imezua shutuma kutoka kwa serikali.

Maandamano hayo ya kutaka mabadiliko mbalimbali ikiwemo mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki, yameelezwa kuwa miongoni mwa machafuko makubwa zaidi nchini katika miongo ya karibuni.

Zaidi ya vijana 600 wwalikamatwa na kufunguliwa makosa yakiwemo ya uhaini. Hata hivyo wakati wa kulifungua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wiki iliyopita Rais Samia alitangaza msamaha kwa vijana hao akisema kuwa vijana hao wengine walifuata mkumbo hivyo waachiwe kwa utaratibu na kurejeshwa kwa familia zao.