"Napoteza uwezo wangu wa kuona kila kukicha"
Na, Paula Odek

Chanzo cha picha, Chelagat Kipkorir
Iwapo una uwezo wa kuona na ghafla ujipate huwezi kuona tena utajihisi vipi?
Bi. Chelagat Kipkorir ambaye ni mtoto wa tano katika familia kutoka nchini Kenya anakabiliana na hali ambayo ni nadra sana na isiyo na tiba ya ‘Retinitis Pigmentosa’, hali ambayo mtu anapoteza uwezo wake wa kuona kadiri anavyoendelea kuishi.
Mwaka wa 2013 Chelagat alijipata katika hali isiyo ya kawaida kwani hakuweza kuona nyakati za usiku na hata kutembea ilikuwa shida.
‘’Nilianza kuingia kwenye vidibwi vya maji, kugonga watu ninapotembea na endapo nitaangusha kitu chini basi ilikuwa vigumu kwangu kukipata lakini mtu mwingine angekipata kwa haraka sana,’’ Chelagat amesema.
Lakini kulingana na Chelagat, anakumbuka alipokuwa mtoto hakuweza kucheza mpira maarufu wa rede kwani kila wakati angeucheza mchezo huo, hakuwa akiona mpira.
‘’Labda huu si mchezo wangu, alisema’’.
Chelagat anasema alizaliwa na hali hiyo lakini hakutambua mapema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kulingana naye alidhani hali hii ilikuwa inasababishwa na jua kali.
Alienda kutafuta msaada wa mtaalamu wa macho lakini alimwambia kuwa hana uwezo wa kuona mbali na kupewa miwani ila baada ya miezi mitatu hali iliendelea kuwa mbaya zaidi ndipo familia yake ikaamua kutafuta usadizi zaidi wa wataalamu na hapo ndipo alipogundulika kuwa na hali aliyokuwa nayo na cha kusikitisha zaidi, ni kwamba aliarifiwa kuwa haina tiba, hivyo basi, hana cha kufanya zaidi ya kujikubali na kuishi na hali hiyo maisha yake yote.
Chelagat anasema baada ya ujumbe huo kutoka kwa daktari alikata tamaa papo hapo.
‘’Niliona nimepoteza kila kitu maishani mwangu’’
Chelagat amesema alikuwa na maswali mengi kama vile atawezaje kuishi bila kujiona kwenye kioo, kuwaona awapendao na atawezaje kuyakimu maisha yake.
Moja kwa moja akaanza akaanza kujiona akitumbukia katika mawazo ya kila aina na bila kujua akawa na tatizo la msongo wa mawazo.
Alianza kukosa usingizi na kujitenga na watu, kipindi hicho alikuwa ameshapoteza uwezo wa kuona kando kando.
‘’Changamoto yangu kubwa ilikuwa kukubali hali yangu, kwamba ipo siku nitapoteza uwezo wangu wa kuona kabisa.’’
Wakati huo Chelagat alikuwa chuo kikuu na ilimbidi kubadilisha kozi aliyokuwa akiifanya na kuanza kozi nyingine ambayo alihisi kuwa ingemfaa hata kama angepoteza uwezo wa kuona.
Alikubali vipi hali yake?

Chanzo cha picha, Chelagat Kipkorir
Chelagat amesema ilimchukua takriban miaka minne kujikumbali lakini pia, usaidizi kutoka kwa wataalamu wa saikolojia ambao walimuongoza na kuanza kumpatia mafunzo ya breli ulikuwa muhimu.
Igawa macho yake ni kama mtu asiye na tatizo na ni vigumu kujua kuwa ana tatizo kama hilo.
Hata hivyo ameisihi jamii kuwa endapo mtu anapitia hali kama hiyo, ajitokeze ili apate usaidizi na kurai familia zenye mtu aliye na ulemavu kama huo apewe nafasi ya kufanya analotaka maishani.
Licha ya hali yake yeye ni mchagamfu na mwenye tabasabu kila wakati, hupenda kupiga picha, kusoma, kusikiliza vipindi na kujumuika na watu wengine.
Retinitis Pigmentosa ni hali ya aina gani?
Ni hali iliyo nadra sana inayoathiri sehemu ya macho maarufu retina.
Hali hii humfanya mtu kupoteza uwezo wake wa kuona polepole.
Hali hii huweza kurithishwa kutoka kwa mzazi hadi kwa mtoto.
Kulingana na utafiti, mtu mmoja kati ya watu 4,000 hupatwa na hali hii.
Hali hii humfanya mtu kutokuwa na uwezo wa kuona kando kando na kutoona majina ya usiku.
Dalili za hali hii huanza mtu akiwa na umri mdogo na huwaathiri watu tofauti tofauti.
Dalili za Retinitis Pigmentosa
- Kutokuwa na uwezo wa kuona usiku
- Kutobaini rangi tofauti
- Kutokuwa na uwezo wa kuona kando kando
Matibabu
Hali hii haina tiba.













