Je, Iran imedukua mifumo ya maji katika majimbo saba ya Marekani?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Ana Faguy
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Watu kadhaa walipigwa na butwaa wiki iliyopita wakati jimbo la Minnesota nchini Marekani liliporipoti kwamba zaidi ya mifumo 30 ya maji imekumbwa na ''shambulio la kupangwa mtandaoni".
Siku kadhaa baadaye Shirika la Upelelezi la Marekani FBI lilionya kwamba mashambulio ya mtandaoni yameripotiwa katika majimbo saba na na baadhi ya mashambulio hayo ''yaliathiri vibaya shughuli zinazohusiana na usambazaji wa maji".
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, Shirika la Marekani la Usalama wa Mtandao na Miundombinu (Cisa) linadaiwa kuchunguza uwezekano wa Iran kuhusika katika mashambulizi yaliyotokea Minnesota. Cisa hajatoa kauli yoyote kuhusiana na saula hilo.
Japo Rais wa Marekani Donald Trump hajaelekeza kidole cha lawama kwa Iran, wataalamu wa masuala ya mtandao wameiambia BBC kwamba kuna uwezekano mkubwa shambulio hilo liliratibiwa na Tehran.
Haya ndiyo tunayojua.
Je, kuna mkono wa Iran?
Morgan Wright, mshauri wa zamani wa kupambana na ugaidi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ameimbia BBC kuwa mashambulizi ya aina hii kwa kawaida huhusishwa na Korea Kaskazini au Iran.
"Na tuna mgogoro na nani kwa sasa? Bila shaka, ni Iran. Kwa hivyo, wao ndio wanaoshika nafasi ya juu katika orodha ya mataifa yenye uwezo, na pia nia, ya kufanya jambo kama hili," alisema.
Wapelelezi wa Marekani pia wanachunguza ikiwa wadukuzi hao huenda walijifanya kuwa wanatoka Iran kama mbinu ya kuzidisha uhasama katikati ya mvutano wa Marekani na Iran, kulingana na kituo cha habari cha CBS, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jake Braun, aliyekuwa Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Mtandao wa Kitaifa katika Ikulu ya Marekani (White House), aliambia BBC kuwa utawala wa Trump unajihusisha na vita vyake vya habari, na hivyo huenda isiwe rahisi kukubali kuwa Iran iliingilia miundombinu ya maji ya Marekani, hata kama jambo hilo lingethibitishwa.
Katika mkutano wa baraza la mawaziri Ijumaa iliyopita, Trump, ambaye ni mwanachama wa chama cha Republican, aliwalaumu maafisa wa Minnesota—akiwemo Gavana Tim Walz—kwa "ukosefu mkubwa wa uwezo" uliosababisha kudukuliwa kwa mfumo wa maji.
Walz, mwanachama wa chama cha Democrat, alijibu hivi: "Trump anajua vyema nani anayehusika na shambulio hili, na anajua kuwa majimbo mengine pia yaliathirika."
Iran bado haijatoa tamko lolote kuhusu matukio haya, lakini Tehran imekanusha mara kwa mara kuhusika na mashambulizi mengine ya mtandaoni kwa miaka mingi, ikiwemo yale yaliyolenga mifumo ya maji, kampeni za urais, hospitali, na kampuni ya kasino huko Las Vegas mwaka 2014.
Baada ya tuhuma za mwaka 2016 zilizohusisha kulengwa kwa benki na bwawa la maji nje kidogo ya Jiji la New York, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran alisema Marekani inapaswa kuthibitisha tuhuma hizo.
Iran "haijawahi kuwa na mpango wowote wa kuchukua hatua hatari katika ulimwengu wa mtandao na haiungi mkono hatua kama hizo," msemaji Hossein Jaberi Ansari alisema kupitia televisheni ya taifa wakati huo.
Je, hii inaendena na mienendo ya Iran?
Iran ina historia ya kufanya aina hii ya shughuli, wataalamu waliambia BBC.
Walibainisha makundi yanayounga mkono Iran, ambayo yaliyo nje ya nchi hiyo, huenda yamefanya shambulio hilo.
"Inafanya iwe vigumu kubaini nani hasa aliyehusika, kwa sababu kama mashambulizi na makundi yote yanatoka ndani ya Iran, ni rahisi sana kuhusisha tukio hilo na Iran," alisema Wright.
Alibainisha kuwa mbinu kama hiyo huwapa wahalifu mwanya wa kutekeleza uovu na kwa kutumia hoja zinazoonekana za kuaminika.
"Hufanya hivyo ili kuficha nyayo zao za moja kwa moja kwenye tukio hilo," alisema.
Uchunguzi wa BBC Verify umebaini kuwa mashambulizi mengi ya mtandaoni ya Iran dhidi ya Marekani na Israel mwaka huu yamefanywa na kundi linalofahamika kama Handala.
Wizara ya Sheria ya Marekani imelihusisha kundi hilo na Iran, ikisema limekuwa likihudumu kwa niaba ya Wizara ya Ujasusi na Usalama ya Iran (MOIS).
Hapo awali, Mkurugenzi wa FBI, Kash Patel, alilituhumu kundi la Handala kwa kupata taarifa binafsi na barua pepe katika siku za awali za mzozo na Iran.
BBC Verify ilibaini kuwa shambulio la mwisho la mtandaoni nchini Marekani lililodaiwa kufanywa na Handala lilitokea katikati ya mwezi wa Juni. Wadukuzi hao walidai kuvamia mfumo wa kituo cha maji huko California ikiwa ni jibu kwa shambulio la Marekani dhidi ya miundombinu ya maji ya Iran.
Hizi hapa ni baadhi ya operesheni nyingine za udukuzi ambazo zimehusishwa na Iran:
- 2026: 2026: Idara ya Sheria ilizuia operesheni ya udukuzi iliyofanywa na kundi la Handala iliyolenga kampuni ya teknolojia ya tiba. Operesheni hiyo pia ilifichua taarifa nyeti kuhusu maafisa wa serikali na jeshi la Israel.
- 2024: Iran ilishutumiwa kwa kudukua kampeni za urais nchini Marekani kwa lengo la "kuchochea migawanyiko, kudhoofisha imani katika mchakato wa uchaguzi wa Marekani, na kupata taarifa kinyume cha sheria" kuhusu maafisa ili kuisaidia Iran.
- 2023: Mifumo ya maji na maji taka nchini Marekani ilidukuliwa na kundi linaloshutumiwa kuwa na uhusiano na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) katika mwaka wa 2023 na baadaye mwaka wa 2024, kulingana na shirika la CISA. Vifaa vinavyodhibiti shinikizo la maji katika miji miwili ya Pennsylvania vilizimwa kwa muda kutokana na tukio hilo.
- 2020: Raia wawili wa Iran walishtakiwa kwa kujaribu kuingilia uchaguzi wa urais kwa kupata taarifa za siri za wapiga kura wa Marekani na kutuma ujumbe wa vitisho ukiwataka watu wampigie kura Trump.
- 2017: Wadukuzi walioko Iran pia walitumiwa kuendesha kampeni ya muda mrefu ya programu haramu iliyolenga serikali za mitaa, shule, pamoja na taasisi za afya na fedha, ingawa CISA ilibainisha kuwa shughuli za kundi hilo "huenda hazikuungwa mkono rasmi" na serikali ya Iran.
Je, inaweza kuathiri usambazaji wa maji?
Wataalamu waliambia BBC kuwa tishio kubwa zaidi la mashambulizi hayo ya mtandaoni halikuwa dhidi ya usambazaji wa maji wenyewe, bali ni kupunguza imani ya umma kuhusu usalama wa maji yao.
"Wanashambulia imani yetu kwa serikali yetu katika uwezo wake wa kutoa huduma za msingi wakati huu ambapo, unajua, nchi imegawanyika sana kuhusiana na suala la vita," alisema Braun.
Wataalamu waliongeza kuwa kuna uwezekano kwamba wadukuzi wa Iran siku moja huenda wakafanikiwa kuhatarisha mifumo ya usambazaji wa maji nchini Marekani.
Vitendo hivyo vya uhalifu vinaweza kusababisha usambazaji hatari wa kemikali, kukatika kwa maji, au kuharibu mitambo, Wright alidokeza.
Cisa na Shirika la Kulinda Mazingira la Marekani (EPA) kwa pamoja zimesema kuwa mashambulizi ya mtandaoni ni "chanzo cha wasiwasi mkubwa" kwa mashirika ya huduma za maji.
Marekani ina mifumo 152,000 ya umma ya maji ya kunywa na zaidi ya vituo 16,000 vya kusafisha maji taka.
"Angalia, kama unataka kuilemea nchi na kuifanya ipige magoti, unalenga mambo mawili: unalenga nishati ya umeme na maji," alisema Wright.
Je hili lingeweza kuzuiliwa?
Vifaa vingi vinavyotumika katika mifumo ya maji na maji taka vinakabiliwa na tishio la kushambuliwa, kutokana na kuwepo kwa miundombinu ya zamani au teknolojia ya kizamani, alisema Wright.
Wataalamu waliozungumza na BBC walionya kuwa bila kuboresha usalama wa mifumo hii, Marekani itaendelea kukabiliwa na tishio hili la usalama wa taifa.
Mashirika mengi ya huduma za maji nchini Marekani yanaendeshwa na serikali, tofauti na miundombinu mingine muhimu.
Hivyo, ni jukumu la serikali kuchukua hatua, wataalamu walisema.
CISA imependekeza maboresho mbalimbali kwa serikali kote Marekani kwa lengo la kupunguza tishio hili.
Ili kuzuia jaribio la udukuzi, shirika hilo lilipendekeza kuwa mifumo ya maji iondolewe kwenye mtandao haraka iwezekanavyo na manenosiri yabadilishwe.















