Familia inayosafiri ulimwengu mzima kabla ya watoto wao kupoteza uwezo wa kuona

Chanzo cha picha, Family Picture
Je inamaanisha nini kuwa na ulemavu wa macho? Mtoto wa miaka mitano Laurent aliwauliza wazazi wake.
Yeye na ndugu zake wawili , Mia na Colin hatimaye watapoteza uwezo wao wa kuona kutokana na ugonjwa usio wa kawaida unaothiri retina ya macho.
Wakati watoto hao walipogunduliwa kuwa na ugonjwa huo, mtaalamu alipendekeza kuwaonesha picha nyingi zaidi , kupitia vitabu, ili kuweza kuvirekodi katika ubongo wao , Picha za maeneo, wanyama na kazi za sanaa….
Lakini wazo hili halikumshawishi mama yao.
‘’Nilijiambia mwenyewe: Sitawaonesha picha hizo kupitia vitabu . Nitawatembeza kuona ndovu na twiga moja kwa moja’’ , alisema Edith katika mahojiano na BBC.
Ni kutokana na hilo ndiposa família hii ya Canada ilianza ziara kote duniani kwa kipindi cha mwaka mmoja ili watoto wao waweza kujionea vitu tofauti duniani.

Chanzo cha picha, Family Picture
Ugonjwa huo
Edith anaeleza kwamba ugonjwa wa watoto wake unaowaathiri polepole , unaitwa retinitis pigmentosa, ambapo husababisha chembe za retina kufa polepole.
Baada ya muda, Laurent, Mia na Colin wataishia kuwa na ulemavu wa macho, hadi wawe hawaona kabisa.
Wakikabiliwa na utabiri huu mbaya, Edith na mumewe, Sébastian, hawakusita kufunga virago vyao na kuanza safari pamoja na watoto hao ambayo, hadi sasa, tayari imewapeleka kutembelea nchi sita katika mabara matatu.
“Ndiyo, tunataka kujaza kumbukumbu zao za kuona, lakini pia tunataka watoto wetu wawe na nguvu kidogo kwa sababu katika maisha yao yote watahitaji ustahimilivu huu,” anasema mama huyo.
Lengo ni kwamba watoto warudi nyumbani wakiwa na zana zote za kihisia wanazohitaji ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
Edith hataki watoto wake waone ugonjwa wao adimu "kama laana, au kama kitu kibaya", lakini waelewe kwamba "hii ndiyo njia yao maishani".
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kufikia sasa, hali hiyo imewafanya ndugu hao wanne kupata kujionea maeneo ya mbali yenye thamani yanayovutia sana.
"Wakati niliopenda zaidi ulikuwa siku yangu ya kuzaliwa kwa sababu niliruka kwa puto ya hewa moto," Laurent aliambia BBC, huku kaka yake Leo akikumbuka kwa upendo wa pekee siku waliyokaa pamoja wakicheza katika mawimbi huko Bali (Indonesia).
Miongoni mwa matukio haya yote, pia kuna nafasi ya muda wa kutafakari, ambayo wazazi wanasimulia katika blogu ya kibinafsi kwenye Facebook inayoitwa "Le monde plein leurs yeux" ("Dunia machoni mwao"):
"Laurent aliuliza tu swali la uchungu: 'Ina maana gani kuwa kipofu?'
Licha ya kuhisi kitu kilichokwama katika koo langu na moyo wangu kuzama kifuani mwangu, ninaendelea kutabasamu, nikijaribu kujibu maswali yake kwa kawaida iwezekanavyo.
'Kwa nini hatuwezi kuponya? Nitavukaje barabara? Je, mke wangu atakuwa kipofu pia?'
Usiku wa leo moyo wangu ni umekatika vipande vipande, kuruhusu maumivu kwenda mbali. Kesho tutakusanya vipande hivyo, tunyanyue videvu vyetu na kuendelea kukabiliana na maisha."












