Waridi wa BBC: ‘Sikuweza kutembea kwa miaka miwili baada ya kufungwa minyororo miguuni’

Iliyochapishwa

Phanice Favor alizaliwa na matatizo, miguu yake miwili ikiwa imejipinda (Clubbed feet ).

Kulingana na simulizi yake juhudi za wazazi wake kumpeleka katika hospitali kadhaa nchini Kenya wakati huo akiwa mtoto mchanga hazikufua dafu.

Na akaishi vivyo hivyo hadi wakati alipofikisha miaka 10 mwaka wa 1990 ndipo alipofikishwa hospitalini kufanyiwa upasuaji, anasema ilikuwa ni juhudi za wasamaria wema.

Wakati huo wote alikuwa anatembea kwa matatizo makubwa kwani miguu yake ilikuwa imejipinda upande wa ndani.

“Kabla ya upasuaji nilikuwa na shida kubwa ya kutembea, wakati huo sikuwa na viatu vya kuvaa, kwa hiyo wakati mwingi nilikuwa nakosa kwenda shuleni, japo tulijaribu kufanya marekebisho kwa viatu vinavyovaliwa, wakati wa mvua haikuwa rahisi nilijipata nikiwa na maambukizo mengi ya fangasi na malengelenge yenye uchungu,”anakumbuka Favor.

Maisha ya kunyanyapaliwa

Aidha mwanadada huyu anasema kuwa alipitia kipindi kigumu cha kunyanyapaliwa kila alipopita hasa miaka ya utotoni.

Anasema aligundua baadhi ya watu wakimtazama kama sinema na kumuita majina bandia japo sio wote.

Anakumbuka baadhi ya majirani wakinyanyapaa familia yake iliyoitwa majina ya kudunisha kwa mfano familia ya ‘viwete’ huku wengine wakisema kuwa jamii yao ilikuwa na laana .

Haya yote yalizua hali ya wasiwasi katika maisha yake Favor akijiuliza maisha ya usoni yatakuwaje?

“ Nilikuwa na mawazo mabaya kutokana na unyanyapaa huo, niliona kana kwamba sistahili kuishi. Nilimchukia sana Mungu, nilikuwa najiuliza je alikuwa na haraka ya kuniumba? na Nilitamani sana kuelewa ikiwa kweli nililaaniwa kwa sababu ni mimi pekee niliyekuwa na ulemavu,” anasema Favor.

Kufanyiwa upasuaji

Mwanamke huyu anasema wakati wa upasuaji hospitalini mguu wake wa kushoto ulichukua masaa 13 kurekebishwa, hii ni kutokana na kwamba mguu huo ulikuwa umepinda kabisa na mifupa kukomaa, siku iliyofuata akafanyiwa upasuaji uliochukuwa masaa 8 kurekebisha mguu wa kulia.

Ila athari za upasuaji alikabiliana nazo kwa miaka miwili iliyofuata.

Favor alikuwa hana uwezo wa kutembea kwani alikuwa amefungwa miguu yake na minyororo ili ipone.

Anasema kuwa kwa miaka miwli alikuwa akilala tu kitandani anakumbuka miguu yake ikiwa na vidonda, hakuwa anainuka wala kuketi, ni kulala tu kama njia ya kupatia miguu fursa ya kupona bila usumbufu.

‘’Haikuwa rahisi kuona minyororo kwenye miguu yangu kwa kipindi cha miaka miwili lakini nilivumilia’’.

Baada ya majeraha kupona, Favour alipewa kiti cha magurudumu na pia miguu yake kuwekwa plasta kama njia ya kuinyoosha irudi kuwa kawaida .

“Baada ya miezi 6 plasta ilitolewa na nikapewa viatu spesheli pamoja na magongo, niliendelea kufanya mazoezi ya kunyoosha miguu (physiotherapy), kisha baada ya muda fulani, nikawa na nguvu kidogo ya kutembea kwa kutumia magongo,’’ anakumbuka Favour .

Maisha baada ya upasuaji

Baada ya upasuaji yeye mwenyewe aligundua kuwa amepata nafasi ya kujiboresha na akaanza kubuni aina ya viatu vyake maalum vilivyomuwezesha kutembea na kuendesha shughuli zake za kila siku.

Favor alirejea akiwa amepoteza miaka mitatu nje wakati anatibiwa miguu yake na ikabidi arudi nyuma kimasomo.

Anajivunia kwamba licha ya kuchelewa kukamilisha masomo yake ya shule ya msingi alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliopata alama bora.

Alifaulu kuingia chuo kikuu cha Nairobi na kufuzu mwaka wa 2005 kwashahada ya kwanza katika sanaa ya elimu, kingereza na fasihi.

Amekuwa akifanya kazi kama mwalimu katika kaunti ya Kilifi hadi sasa pamoja na kuwa mtoa nasaha kwa wanafunzi wa shule za upili katika kaunti hiyo.

Favor ni Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari ya Moi Kadzonzo.

“Nimekuwa pia nikihubiri Injili, mwaka wa 2022 nilihitimu Shahada ya Uzamili ya Saikolojia ya Ushauri kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta na kwa sasa ninasomea PHD katika Saikolojia ya Ushauri Chuo Kikuu cha Methodist Kenya. Pia nilifanya Diploma ya Elimu na Diploma ya Juu ya Usimamizi wa Rasilimali Watu,’’ anasema Favor.

Anapotizama nyuma alikotoka anaishiwa na maneno hasa akikumbuka unyanyapaa na chuki nyingi nyakati za awali.

Pia mwanamke huyu ni mwandishi wa vitabu na hivi maajuzi ameandika vitabu 6, kwa sasa tayari amechapisha 2.

Kimoja cha ushairi wa shule ya upili, na kingine kikiwa na nukuu 1001 za hekima kwa maisha yenye mafanikio kwa wote.

Favor ni mama wa watoto watatu na ameolewa. Anasema licha ya mlemavu wake ameona Maajabu makubwa ya Mungu katika maisha yake.