Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
"Watoto wangu 9 niliojifungua wakiwa hai walifariki nikitizama"
Na Anne Ngugi
BBC Swahili
Anaposimulia matukio katika maisha yake utadhani anasimulia tamthilia au anakusimulia sinema fulani ya kustaajabisha. Lakini haya ndio maisha halisi ya Bi. Maggie Wanjobi, mwanamke kutoka Kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya.
Katika kipindi cha takriban miaka kumi na mitano mwanamke huyu alipitia uchungu usioelezeka kwani alikuwa anapata ujauzito, analea mimba hadi kufikia siku ya kujifungua, ila kati ya watoto wake kumi na wawili, kumi kati yao walifariki baada ya kuishi kati ya siku mbili na mwezi mmoja pekee.
“Imekuwa ni safari ndefu ya kutafuta kuitwa mama, niliolewa nikiwa msichana mwenye umri wa miaka 16 na nikapata ujauzito mara mmoja. Kwa miaka mingi nilifahamu tu uchungu kwa kuwa nilikuwa najifungua mtoto na baada ya siku anafariki. Sio kitu ambacho ninaweza kumtakia mama yeyote kwa kweli ”anasema Maggie.
Matukio ya kushangaza
Maggie hakufanikiwa kuingia shule ya sekondari baada kufaulu vizuri mtihani wake wa kumaliza shule ya msingi. Kulingana na mwanadada huyu wanawake wengi waliozaliwa katika jamii yao walikuwa wanapata mimba za utotoni au kuolewa mapema kwahiyo hakuwa na mfano mwema wa kuendelea na masomo yake.
”Kwetu kulikuwa na historia mbaya ya wasichana kupata ujauzito wakati wanapofanya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi, kwahiyo ni kana kwamba baba hakuwa tayari alidhani kwamba nitakuwa mjamzito wakati namalizia shule , ila kwangu ilikuwa tofauti sikupata mimba. Jamii yangu hawakunipeleka shule ya sekondari badala yake nilikwenda katika mkuu Nairobi kutafutia kazi za nyumbani ”anakumbuka Maggie.
Ulikuwa mwaka wa 2000 alipoanza kazi za kuwa mfanyikazi wa nyumbani akiwa katika pilkapilka hizo alikutana na mwanamume ambaye walianza uhusiano wa kimapenzi na hatimaye wakaingia kwenye uhusiano wa ndoa. Hata hivyo anasema kwamba yeye hakujua maana ya ndoa au mapenzi ni kitu gani haswa alipokuwa katia ndoa hiyo.
Alifunga ndoa akiwa na umri wa miaka 16, na anasema maisha ya mwanzo wa ndoa yalikuwa na changamoto kwani hakufahamu majukumu ya kuwa mke na jinsi ya kumtunza mume.
”Baada ya miezi mitatu ya ndoa siku moja niliamka asubuhi na nikawa na udhuru wa mwili, nilizimia nikiwa pale pale kwa nyumba ilibidi nisafirishwe hadi hospitalini kwa ambulensi , hakuna chochote ambacho nakumbuka, ila niliamka na uchungu mwingi mno kana kwamba nilikuwa nimefanyiwa upasuaji wa dharura ”, anasema Maggie.
Kulingana na mama huyu alikuwa tayari amepata ujauzito, ila mimba ilikuwa imeingia kwenye mrija unaounganisha mfuko wa mayai ua uzazi na mfuko wa uzazi (fallopian tube) na ilisababisha mshipa wake mmoja kupasuka, jambo ambalo lilimfanya azimie , na kwamba ilibidi afanyiwe upasuaji wa haraka wa kutoa kijusi kilichokuwa ndani ya tumbo lake kwa miezi mitatu. Mwanamke huyu anasema kwamba hakuwa na habari ya kuwa alikuwa mjamzito, kwa maana hakufahamu dalili na kwa hilo lilimshitua sana.
Kifo baada ya kifo
Maggie alirejea nyumbani na kuendelea kuuguza vidonda vya upasuaji , na kuanzia wakati huo alianza kupata mawaidha kuhusu ndoa, kupanga uzazi na na mawaidha mengine ya ndoa.
Hata hivyo ila ilichukua muda kabla ya kupata ujauzito mwingine. Yeye na mume wake waliamua kupata ushauri wa daktari na ndipo walipoambiwa kuwa kulikuwa na matatizo katika kizazi chake yaliyotokea baada ya kupata ile mimba ya kwenye mrija (fallopian tube )
Mwaka wa 2002 alipata ujauzito mwingine, na anasema mara hii alifuata ushauri wa kliniki, lakini asubuhi moja aliamka na uchungu mwingi ,kufika hospitalini alielezwa kwamba alikuwa katika hatari na alihitaji upasuaji wa dharura: ”Nilipoamka baada ya kufanyiwa upasuaji nilifahamishwa kwamba nilijifungua mtoto wa kike, ila madaktari walisema kwamba alikuwa na matizo ambayo yangemsababishia kifo. Lakini mimi niliamini kuwa wanangu angeishi. ”, anakumbuka Maggie.
Anasema kwamba baada yakuwa hospitalini kwa siku kadhaa, yeye na mwanae waliruhusiwa kurudi nyumbani. Hatahivyo hata baada ya kurejea nyumbani, mtoto wao alikuwa kiugua mara kwa mara, hali iliyowafanya waende watembelee hospitalini kwani matatizo ya kiafya ya mtoto yalikuwa mengi na hata wakati mmoja alilazimika kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi. Badala ya mwanaye kuongeza uzani wa mwili baada ya kuzaliwa aliendelea kudhoofika na kupungua uzito wake. Alizaliwa na uzito wa kilo moja nukta sita , lakini hadi alipofariki akiwa na umri wa miezi minne alikuwa na uzito wa gramu mia saba pekee yake, kulingana na Bi Maggie.
”Maisha yalibadilika sana baada ya kumzika mtoto wangu, watu walikuwa wameanza kuongea mengi kwa mfano, nilijifungua mtoto aliyekuwa na maumbile ya ajabu , na wengi walizungumza mengi kuhusu tukio hilo ”, Maggie anakumbuka.
Mwaka wa 2004 Maggie alipata ujauzito mwingine na mimba ikaendelea kukua hadi miezi minane, ambapo alishauriwa kufanyiwa upasuaji ili kuokoa maisha ya mtoto. Lakini mtoto aliishi kwa siku mbili pekee, akaaga dunia , anaongezea kuwa walifanya shughuli ya mazishi na akazikwa kama mtoto wapili katika shamba lao.
Mwaka wa 2005 alipata ujauzito wa tatu na akalea mimba hadi mwisho wake iliwadia wakati kujifungua na akafanyiwa upasuaji ila mtoto aliishi tu kwa wiki mmoja akaaga dunia...Maggie na jamaa zake walimbeba mtoto na kumzika.
Miaka ya 2006 hadi 2009 alipoteza watoto wengine watatu kila baada ya kujifungua walifariki katika njia za kutatanisha kambapo alielezwa kuwa alikuwa mtoto alikuwa mgonjwa au kwamba alichoka akiwa tumboni.
Mwisho wa ndoa
Hali ya kufiwa na watoto sita ilizua misukosuko katika ndoa yake, hasa anasema mengi yalizungumzwa huku wengi wakijiuliza iwapo Maggie ana uwezo wa kubeba mimba na kujifungua mtoto ambaye ataishi.
”Mengi yalizungumzwa ikiwemo kwamba nimebadilisha shamba letu kuwa la makaburi ya watoto , na kwamba haitakubalika tena nijifungue mtoto ili akajaze shamba na kaburi lingine , haikuchukua muda kwa mume wangu kuchoka na kuamua kwamba ilikuwa wakati nirejeshwe nyumbani kwetu kwanza ” Maggie anasema.
Mwanamke huyu anasema kwamba ndoa yake iliisha wakati mume wake pia alionyesha kuchoshwa na vifo vya kila mtoto wanayejaaliwa. Mume wake alimsihi Maggie arejee nyumbani kwao kwanza apone na pia kwa kuwa alikuwa na sonona atulize mawazo. Maggie alifahamu kwamba ilikuwa ni njia ya kiungwana ya kumfukuza kwenye boma yake .
Baada ya hapo mama huyu anasema kwamba mume wake alioa mke mwingine punde tu alipoondika nyumbani kwake.
Ndoa ya pili
Mwaka wa 2009 Maggie aliingia kwenye ndoa nyengine ambaye tayari alikuwa amemueleza mume wa pili kuhusiana na masaibu ya kupoteza watoto kutokana na vifo vilivyokuwa havieleweki. Na kwa hiyo waliingia kwenye ndoa hiyo na ikawa ni siri kati yake na mumewe.
Katika Ndoa ya pili alipata uzauzito mara tatu , mimba ya tisa aliyoipata mtoto aliaga dunia, ila mimba ya kumi aliyoipata mtoto aliishi na leo ana umri wa miaka 12.
Baada ya hapo aalipata mimba ya mapacha, mtoto mmoja aliishi baada ya kuzaliwa ila wa pili alifariki.
Kwa jumla Maggie ni mama ya watoto 12 ila ni watoto wawili pekee walio hai hii leo.
Vile vile anasema kwamba ndoa yake ya pili ilifika ukingoni , pale taarifa kwamba alikuwa kwenye ndoa ya kwanza na alikuwa amepoteza watoto wengi zilipowafikia jamaa wa mume wake .
Siri hio ilisababisha kizaazaa cha ndoa na ikawa kwamba hawawezi kuendelea na kuwa katika ndoa.
Maggie anasema kwamba safari ya kujifungua watoto na baada ya siku, wiki au miezi wanafariki haijakuwa nyepesi , imejaa majonzi,- hofu na kusimangwa sana katika jamii.
”Ilifika wakati nilianza kusikia baadhi ya watu wakisema kwamba ninawatoa watoto wangu kafara, na ikafika wakati ambapo kila mahali nilipokuwa napita wakinifahamu walikuwa wananinyooshea kidole cha lawama wakisema kwamba ni yule mama ambaye anazaa watoto wanafariki” Maggie anasema.
Ila anasema kwamba kadri siku zilivyokwenda alijikubali na kukubali hatma iliyowaangukia. Watoto wake walikifariki wakiwa wadogo ila anafarijika kwamba walau ana watoto wawili ambao wako hai na wanamkumbusha kwamba licha ya mahangaiko ya vifo anayo sababu ya kutabasamu kwa wanaoishi.
Maggie anatumia simulizi la maisha yake ya kuwapoteza watoto kuwaelimisha hasa wanawake , jinsi ya kukabiliana na mimba zinazosumbua au inapotokea kwamba mama atampoteza mtoto wake.