Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: Claudette ambaye anakadiria kuwa na zaidi ya kilo 200 anaishi kwa huzuni kwa sababu ya unene
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Maisha ya kawaida kwa mtazamo wake Claudette Nyirangendo anasema ni kama kukwea mlima kila siku , hii inatokana na unene wa mwili wake ambao kwa sasa umelemaza shughuli ambazo zinaweza kuonekana za kawaida ila kwake ni mahangaiko kweli .Hajapima uzito wake hivi karibuni lakini kwa sasa anakadiria kuwa na zaidi ya 200 akiwa na miaka 43 mama huyu anaishi na huzuni huku akisema kwamba anatamani sana kupunguza uzito wa mwili.
"Maisha yanakuwa magumu sana kwangu , wakati mwengine inaweza kuchukua siku mbili au tatu sijatoka kitandani , hii inatokana na ugumu wa kutembea kutokana na uzito wa mwili wangu "anasema Claudette
Claudette ambaye ni mzaliwa wa Rwanda anazungumza kuhusu maisha ya utotoni na pia katika usichana wake kama yalikuwa mazuri, anakumbuka wakati huo hakuwa na unene wa mwili alionao sasa. Licha ya kwamba anasema anakula chakula asilia kutoka nchini mwake ambacho kinaliwa na watu wengine kwa mfano ndizi na mboga haelewi ni vipi mwili wake umezidi kunenepa hasa katika kipindi cha miaka 6 iliyopita.
Unene huu umemsababishia karaha mno hasa anapokumbuka kwamba mojawapo ya sababu za ndoa yake kufika ukingoni inahusiana na uzito wake.
Kulingana na mama huyu anadhani kwamba mume wake alichoka kuishi na yeye kutokana na uzito wake kwani anasema kwamba ni jambo alilokuwa analizungumzia kila wakati wakiwa kwenye ndoa hio
"Mimi nilikuwa mama na mke mwema , ila ndhani kwamba unene wangu ulikuwa ni kero kwa mume wangu , aliishia kuniacha na kuendelea na maisha yake. Sasa maisha ni mimi binti yangu ambaye ananisaidia kwa kila jambo hasa kwa kuwa sina uwezo wa kuinama" anasema Claudette.
Mwanamke huyu anasema kwamba alikuwa kwenye ndoa ya kwanza kwa miaka mingi lakini mume wake alifariki na akabaki mjane akiwa na watoto wanne.
Baada ya hapo aliingia kwenye mahusiano mengine yaliYoishia kwenye ndoa mpya , walijaaliwa mtoto mmoja kabla ya mume wake wa pili kumpa talaka.
Alipo sasa anaishi na mwanae na anasema kwamba maisha yamekuwa magumu kwake. Changamoto nyengine inatokana na kwamba anatembea kwa shida sana.
Eneo analoishi vyumba vya kujisaidia viko nje ya nyumba yake na ni vidogo kwake kuingia kutokana na unene wake , hali kadhalika hana uwezo wa kuinama.
''Inanipa huzuni sana kuona kwamba uzito wangu umenifikisha katika hali ya kwamba hata mambo ambayo ni ya kibinafsi sana, kwenye haja zangu nahitaji usaidizi wa mtu hapa namaanisha binti yangu ambaye huniaidia sana kwani siewezi kufika pale chooni , siwezi kutosha mlangoni na pia uzito wangu hauniruhusu kuinama "anasema Claudette
Mbali na hayo pia mwanamke huyu anasema kwamba usafi wa mwili wake wakati mwengine unakuwa na changamoto. Kuna wakati hawezi kwenda bafuni mara nyingi huoga kwa kujifuta.
Kwasasa anatafuta mbinu mbali mbali za kuanza kukata uzito wa mwili wake.
Anasema kwamba shughuli zake nyingi ambazo zinahitaji awe nje ya nyumba yake zimekwama na hajui afanye nini.
Sonona imekuwa sehemu kubwa ya maisha yake kwa kuwa na mawazo mengi ya unene wake hali kadhalika upweke wa kukaa nyumbani siku baada ya nyingine akiwa hawezi kutembea au kusimama kwa muda mrefu .
Claudette anatumai kwamba atapata suluhu ya jinsi ya kupunguza unene wa mwili wa mwili wake.
Je Unene wa mwili husababishwa na nini?
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani na mitandao ya afya, Unene wa kupindukia (kwa Kiingereza "obesity" hutokana na neno la Kilatini obesitas, linalomaanisha "gumu, nono au nene"
Hii ni hali ambapo mafuta ya ziada ya mwili hulimbikizana hadi kiwango kinachoweza kuathiri afya kwa kiwango kikubwa
Kipimo cha mwili kuwa mnene na mzito mno ni uwiano kati ya urefu wa mtu na uzito wake.
Watalam wa afya wanasema kuwa unene uliopitiliza ni hatari kwa afya na husababisha au kuongeza uwezekano wa magonjwa tofauti yakiwemo Shinikizo la juu la damu , Maradhi ya moyo na matatizo ya kupumua.
Unene wa kupindukia mara nyingi husababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo kula chakula kilicho na wanga nyingi,
Ukosefu wa mazoezi ya mwili, na urithi wa jini maalumu, ingawa visa vichache vina msingi wa jini pamoja na matatizo ya homoni.
Chakula bora na mazoezi ya mwili ndiyo njia kuu za kutibu unene wa kupindukia.