Polisi watafuta utambulisho wa wanawake 22 waliouawa

Iliyochapishwa

Na, Alice Cuddy, BBC News, Amsterdam

Polisi katika nchi tatu za Ulaya wanaomba usaidizi wa kuwatambua wanawake 22 waliouawa ambao majina yao yamesalia kuwa kitendawili.

Miili hiyo ilipatikana Uholanzi, Ubelgiji na Ujerumani kati ya 1976 na 2019.

Mauaji ambayo bado ni fumbo ya mwanamke mmoja huko Amsterdam, aliyepatikana kwenye pipa la magurudumu kwenye mto, yalichochea hatua ya polisi wa Interpol.

Ni mara ya kwanza kwa kundi la polisi wa kimataifa kujitokeza hadharani na orodha ya kutafuta habari kuhusu miili isiyojulikana.

Kile kinachosemekana kuwa tuhuma za uhalifu mkubwa haswa yaani "black notices", kama sehemu ya kampeni inayojulikana kama ‘Operesheni Nitambue’, kwa kawaida husambazwa ndani tu kati ya mtandao wa polisi wa Interpol duniani kote.

Mwanamke aliyepatikana kwenye pipa huko Amsterdam mnamo 1999 alikuwa amepigwa risasi kichwani na kifuani.

Afisa wa upelelezi Carina Van Leeuwen amekuwa akijaribu kutatua kitendawili hicho tangu alipojiunga na timu mwaka 2005 katika jiji hilo, iliyoshughulika na kesi ya kwanza ya uchunguzi wa makosa ya jinai ambao haujatatuliwa na umesalia wazi ukisubiri ugunduzi wa ushahidi mpya.

Polisi wa Uholanzi wanasema kesi inakuwa hivyo, inapobaki wazi na kutotatuliwa baada ya takriban miaka mitatu.

Baada ya kjfanyika kwa juhudi zote, yeye na mwenzake waliwasiliana na polisi katika nchi jirani za Ujerumani na Ubelgiji na kujua kuhusu kesi nyingi zaidi zinazowezekana kuwa za mauaji za wahasiriwa wanawake wasiojulikana.

Nchi hizo tatu zilikusanya orodha ya majina 22 ambayo walikuwa na wakati mgumu kupata ufumbuzi wa kesi hizo na kuwataka Interpol kuchapisha maelezo hayo.

Polisi wa Ubelgiji waliwasilisha kesi saba, Ujerumani sita na Uholanzi tisa.

Wengi wa waathiriwa walikuwa na umri wa kati ya miaka 15 na 30.

Bila kufahamu majina yao au ni nani aliyewaua, polisi wanasema ni vigumu kubaini mazingira halisi ya vifo vyao.

Orodha kamili - inayopatikana kwenye tovuti ya Interpol - inajumuisha maelezo kuhusu wanawake hao, picha za vitu vinavyoweza kuwatambulisha kama vile mavazi, vito na tattoo, na katika baadhi ya matukio, urekebishaji wa sura mpya na taarifa kuhusu kesi hizo.

Bi Van Leeuwen anasema kupata majibu katika visa kama hivyo ni muhimu. "Ikiwa huna jina, huna simulizi. Wewe ni nambari tu. Na hakuna nambari," anaelezea.

Nchini Uholanzi, karibu miili yote isiyojulikana ya wanawake inaonekana kuwa kesi za mauaji, huku - wanasema polisi - wanaume wasiojulikana walifariki katika mazingira mbalimbali.

Katika sehemu hiyo ya Ulaya, watu wanaweza kwenda kati ya nchi kwa urahisi sana kwa sababu kuna mipaka ya wazi.

Ongezeko la uhamiaji duniani, na biashara haramu ya usafirishaji binadamu, kumesababisha watu wengi zaidi kuripotiwa kupotea nje ya mipaka ya nchi zao, anasema Dk Susan Hitchin, mratibu wa kitengo cha DNA cha Interpol.

Inaweza kufanya utambuzi wa miili kuwa na changamoto zaidi, na wanawake "wanaathiriwa isivyo sawa na unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa majumbani, unyanyasaji wa kingono, na usafirishaji haramu wa binadamu," anasema.

"Operesheni hii inalenga kuwarejeshea wanawake hawa majina yao."

Mwathiriwa nambari moja

Mwili wa mwanamke huyo uliopatikana kwenye pipa hilo sasa uko kwenye makaburi katikati mwa Amsterdam.

Kaburi lake limewekwa karibu na njia ya treni na nyuma ya safu za kaburi yenye maandishi yaliyochongwa na maua mapya yaliyokatwa yamewekwa.

Yuko katika eneo la wale ambao majina yao hayajulikani. Makumi ya mabamba madogo ya kumbukumbu huwekwa kutokeza nje ya udongo yakiwa na maneno "wafu wasiojulikana".

Mwanamke huyo alipatikana wakati mwanamume wa eneo hilo, Jan Meijer, alipotoka nje kwa mashua yake na kuchukua pipa la magurudumu ambalo jirani yake aliliona likielea kwenye mto unaopita karibu na nyumba yake nje kidogo ya mji mkuu wa Uholanzi.

Lakini alipolipiga pipa kwenye boti aliona lilikuwa zito zaidi kuliko vile alivyotarajia na, kadiri lilivyozidi kuenea juu ya maji, aliweza kunusa "kitu cha kutisha".

Kama zima moto, Jan aliwahi kuwa karibu na maiti hapo awali. Lakini uvundo huu ulikuwa si wa kawaida. Ulimrudisha kwenye tukio la utoto wake, alipopata mzoga uliooza wa kondoo aliyechinjwa.

Alipochunguza kwa makini, aligundua kuwa pipa lilikuwa limefungwa.

Alilivuta hadi kwenye sitaha yake na kuwaita polisi.

Wakati pipa hilo lilifunguliwa na kuwa wazi, maafisa walipata mifuko ya sabuni ya unga ikiwa imerundikwa juu yake.

Waligeuza pipa juu chini na mwili ukaanguka sakafuni. Mkono mmoja ulikuwa umefungwa kwa zege kwa sehemu.

Afisa mmoja aliyekuwa pale ananiambia mwili ulikuwa wa kijivu na ulionekana kama "mchongo wa mchanga".

Ilikuwa vigumu kutambua kama mtu huyo alikuwa mwanamume au mwanamke, anasema.

Uchunguzi wa wakati huo uligundua kuwa mwanamke huyo labda alikuwa katikati ya miaka ya 20 na "akionekana kuwa na asilia nusu ya Ulaya ya Magharibi na kwa kiasi fulani, kutoka Asia".

Uchunguzi wa hivi karibuni zaidi wa kisayansi, kwa kutumia uchanganuzi wa isotopu, umeelekeza zaidi mahali alipozaliwa ama kuwa holanzi, Ujerumani, Luxemburg au Ubelgiji.

"Yote yanahusiana na chakula unachokula na maji unayokunywa, lakini pia hewa unayopumua," Bi Van Leeuwen anasema kuhusu mbinu hiyo.

Wiki chache baada ya kugunduliwa kwake, polisi walitoa maelezo ya ukubwa wa nguo na viatu vyake na alichokuwa amevaa, lakini bado hawakuweza kumtambua.

Viatu vyake vyeusi vyenye kamba na soli ya bapa havikuwa miguuni mwake bali vilikuwa vimewekwa kwenye pipa pamoja na mwili wake.

Taarifa za kilichopatikana na mwili huo zimetolewa na kundi la Interpol ikiwa ni sehemu ya ‘Operesheni ya Nitambue’.

Alikuwa amevaa saa ya rangi ya dhahabu kwenye mkono wake wa kulia na mfuko wa ngozi ya nyoka pia ulipatikana kwenye pipa.

Nguo za mwanaume pia zilipatikana kwenye pipa - polisi wanaamini kuwa ni za mhalifu. Ni pamoja na koti lenye alama nyekundu ya mviringo iliyoshonwa ndani yake. Jitihada za kutambua chochote zaidi hazikufaulu.

Hakuna mshukiwa aliyewahi kuhojiwa au kukamatwa kuhusiana na kesi hiyo, na hamu ya awali ya vyombo vya Habari kutaka kujua zaidi ikafifia baada ya muda mfupi.

Lakini kwa waliokuwepo siku ile mwili ulipopatikana, haikuwa rahisi kumsahau mwanamke huyo ambaye hakufahamika jina lake. Bado wanashangaa alikuwa nani - na ni nani anayeweza kuwa anamtafuta.

'Wote walikuwa na mtu ambaye anatamani kuwaona'

Wakati mpelelezi Carina van Leeuwen alipotembelea kaburi la mwathiriwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2007 alihisi kushtushwa na kuhuzunishwa na matukio ya watu kujikuta katika vifo vya aina hii.

Mmiliki wa kaburi alimuuliza mpelelezi alipanga kufanya nini kuhusu "wengine wote".

Hapo ndipo alipogundua ukubwa wa tatizo la miili isiyojulikana.

Kutambua waliofariki ndio ikawa utaalamu wake na ameendelea kubaini watu 41 waliofariki kutokana na sababu mbalimbali.

Miili yote ambayo ameitambua ilikuwa na kitu kimoja sawa.

"Haijalishi ilichukua muda gani kuwatambua, wote walikuwa na mtu ambaye anatamani kuwaona," anasema.

"Hata ikiwa ni miaka 25 baadaye, watu wanafurahi sana kuwa na kitu ambacho wanaweza kuzika na kutoa heshima zao."

'Operesheni Nitambue’

Ni miili minne pekee ambayo Carina amesaidia kutambua nchini Uholanzi walikuwa watu kutoka nchi hiyo, ndiyo maana anaamini kufanya kazi na vikosi vya polisi kuvuka mipaka, na ufahamu mpana wa umma, ni muhimu sana.

Mojawapo ya kesi za ‘Operesheni Nitambue’ ni mwanamke aliyepatikana nchini Ubelgiji akiwa na tattoo ya kipekee ya ua jeusi lenye majani ya kijani na "R'NICK" iliyoandikwa chini yake.

Alipatikana akiwa amelala kwenye mwamba kwenye mto huko Antwerp mwaka wa 1992.

Polisi walisema aliuawa kikatili, lakini hawajawahi gundua jina lake kamwe.

Katika kisa kingine cha mwaka 2002, mwili wa mwanamke ulipatikana katika klabu mji wa Bremen nchini Ujerumani, ukiwa umefungwa kwenye zulia na kufungwa kwa kamba.

Interpol inasema inatumai kuwa kutoa orodha hadharani ya wanawake hawa waliouawa ambao bado hawajatambulika kutasaidia kuharakisha kumbukumbu na kuhimiza watu kujitokeza na taarifa zozote wanazoweza kuwa nazo.

"Labda watatambua hereni au nguo maalum ambayo ilipatikana kwa mwanamke ambaye hajatambulika," anasema Dk Susan Hitchin wa Interpol.

Katika baadhi ya kesi 22, vikosi vya polisi vinatumia teknolojia ambayo haikuwepo wakati miili hiyo ilipatikana ili kuongeza uwezekano wa utambuzi.

Usanifu mpya wa uso wa mwanamke aliye kwenye pipa huko Amsterdam umetayarishwa na Dk Christopher Rynn, msanii wa uchunguzi huko Scotland.

Carina anasema ingawa angependa kutatua kesi hiyo na kumtafuta mhusika. Kwake yeye "yote yanahusu utambulisho wa [mwanamke], ili tu kumrudisha kwa familia".

Anasema "hatakata tamaa kamwe" kwa mwanamke aliyepatikana kwenye pipa akiwa ameuawa, au wengine anaowachunguza.

"Wewe ni mtu, una jina, una historia, na historia inapaswa kuzungumziwa hadi mwisho, hata kama mwisho ni wa kusikitisha kiasi gani."