Vita ya Marekani na Iran yaipa thamani gesi asilia Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Alfred Lasteck
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 9
"Madereva wanaotuma vyombo vya moto vinavyotumia gesi asilia (CNG) huwa hawalalamiki hata ukimwambia nauli uliyo nayo haitoshi tofauti na wale wanaotumia nishati ya mafuta, hivi karibu wamekuwa wakali na hawakubebi kama hauna nauli tosha, yote ni kupanda kwa bei ya mafuta kufuatia mgogoro unaoendelea kati ya Marekani na Iran, " anasema Mariam Simbachaweni ambaye mkazi wa Manzese jijini Dar es Salaam.
Kauli ya Mariam inakuja wakati vita kati ya Marekani na Iran ikiendelea kuyumbisha soko la nishati duniani, ambapo bei ya mafuta imepanda kutokana na hofu ya kuvurugika kwa usalama na usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango bahari wa Hormuz, njia muhimu inayobeba sehemu kubwa ya mafuta ya dunia.
Hali hiyo inatajwa kuathiri mataifa mengi ya Afrika ambapo bei za mafuta zimepanda na hivyo kuongezeka kwa gharama za usafiri, bidhaa na huduma. Lakini nchini Tanzania, watumiaji wanasema uwepo wa gesi asilia, umeme katika sekta ya usafiri umepunguza baadhi ya changamoto.
Dar es Salaam hadi Dodoma, mabasi ya abiria hadi pikipiki za magurudumu matatu 'bajaji', gesi asilia imekuwa mbadala unaotoa nafuu wamiliki wa vyombo vya moto na wananchi wakati soko la mafuta duniani likikabiliwa na misukosuko isiyotabirika.
Bei elekezi ya gesi asilia kwaajili ya magari nchini Tanzania ni shilingi 1,550 za kitanzania (Dola za Kimarekani 0.59). Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ndilo linalodhibiti ubora na kupanga bei ya nishati hiyo.
Kipato cha uhakika
Bahati Peter, ambaye ni dereva wa basi linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Morogoro anasema kuwa posho anayopata ni nzuri kuliko wakati akiedesha gari lililokuwa likitumia mafuta ya dizeli.
Peter anasema, "Toka nianze kuendesha gari la gesi, sioni nikirudi kule kwenye mafuta, kwa siku ninapata posho mpaka shilingi 50,000 (dola 19.2. Sasa wakati nikiendesha gari la mafuta nilipata shilingi 30,000 na wakati huo mafuta yalikuwa bei ndogo, najiuliza kwa mafuta haya ningekuwa napata kitu kweli? …
"…gesi asilia imebadili maisha yangu, nasomesha, nimejenga," anaeleza Peter ambaye ni mkazi wa Morogoro. Mji wa Morogoro unapatikana mashariki mwa Tanzania, kilometa takribani 190 kutoka jiji la kibiashara la Dar es Salaam.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Peter anasema, vita viavyoendelea kati ya Marekani na Irani, vinaonesha jinsi gani gesi ni fursa kwa wamiliki wa vyombo vya moto kwani ni salama, bei rahisi na rafiki kwa mazingira.
" Kilo moja ya gesi asilia ni shilingi 1,550 (dola 0.59) ukitumia unaenda mwendo mrefu kuliko lita moja ya mafuta ambayo sasa yanazidi shilingi 4,000 (dola 1.53). Fikiria hata kabla ya mgogoro wa Irani mafuta hayakuwahi kufikia bei ya gesi," anaeleza Peter.
Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude aliiambia BBC kuwa kadiri muda unavyokwenda na matumizi ya gesi kuongezeka na kutengeneza fursa za ajira na kusukuma maendeleo kutokana na urahisi wa nishati hiyo.
"Kama tutaamua kwenda katika mfumo wa gesi na kufanya uwekezaji wa kutosha, nafikiri hata migogoro inapotokea nje, haitatuathiri kwa kiwango kikubwa kwani tuna gesi ambayo inaweza kusukuma uchumi kwenye viwanda, matumizi ya majumbani na hata kwenye magari," anasema huku akieleza kuwa gesi ya Tanzania kwa siku za mbele pia inaweza kuuzwa nje na kuongeza fursa.
Mkude anasema, katika miji kama Nairobi (Kenya), Kampala (Uganda) na Kigali (Rwanda), matumizi ya gesi asilia kwenye magari bado ni madogo, au hakuna kabisa hali ambayo ni tofauti na Dar es Salaam ambako magari ya teksi 'bajaji' na mabasi yanatumia gesi hivyo kuwa sehemu ya kusukuma uchumi.
Zaidi ya vyombo vya moto 20,000 vinatumia gesi asilia
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati nchini Tanzania, hadi Machi mwaka huu zaidi ya vyombo vya usafiri 20,000 nchini vilikuwa vinatumia gesi asilia sambamba serikali pia imewezesha ujenzi wa vituo 18 vinavyotoa huduma huku vingine nane vikiwa katika hatua za ujenzi.
Kwa madereva wengi wanaotoa nishati ya gesi jijini Dar es Salaam, wanasema wanapata nafuu na hivyo wanafuraha kazi yao.
Dereva wa teksi, Johanes Mrindoko katika eneo la Mbezi Beach jijini alisema kabla ya kubadili mfumo wa gari lake alikuwa akitumia zaidi ya Sh 60,000 (dola 23) kwa siku kununua petroli, lakini iwapo angekuwa anatumia nishati hiyo mpaka sasa angekuwa ananunua mpaka sh 100,000 ( sawa na dola 40) lakini sasa anatumia chini ya Sh17, 000 (dola 6.5) kwa gesi asilia huku akifanya safari zilezile.
"Nikijaza gesi kwenye gari langu nahudumia kwa siku nzima. Ni tofauti kubwa kama ningekuwa natumia mafuta. Tena katika kipindi hichi ingekuwa balaa zaidi," Mrindoko aliiambia BBC
Mmoja wa wamiliki wa 'teksi', Miraji Athumani anasema kuwa matumizi ya gesi kwa muda mrefu yamechangia kuwa na mahusiano bora na madereva wake kwa kile walichokubaliana huwa kinatimizwa.
" Niseme tu, huwa sigombani na madereva wangu kwasababu hawaniletei visingizio labda mafuta yako juu au vipi. Magari yangu yote yanatumia gesi ambayo ni bei ndogo sana, hivyo wananiletea stahiki zangu vizuri, sidhani kama wengi wanaoendesha magari ya mafuta kwasasa kama wanaweza kupeleka fedha kama zamani. Na pia sidhani kama wanapata posho. Gesi imeniokoa kwa kweli," anasema Athumani
Meneja wa mradi wa kuunganisha mfumo wa gesi asili katika magari (CNG) katika Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Dkt Esebi Nyari anasema watumiaji wengi wa gesi asilia nchini huokoa kati ya asilimia 40 hadi 60 ya gharama walizokuwa wanatumia kwa petroli au dizeli.
"Faida ni kubwa ya kutumia gesi, ni nafuu, ni salama na inapatikana kwa wingi. Unaweza kubadili mfumo wa gari au kuagiza gari la gesi na ni njia bora ya kupunguza gharama," anasema Dkt Nyari.
Kuna kiasi gani cha gesi asilia nchini Tanzania?

Wakati nchi nyingi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiendelea kutegemea kwa kiwango kikubwa mafuta yanayoagizwa kutoka nje, Tanzania ina faida ya ziada kwa kuwa na akiba kubwa ya gesi asilia inayopatikana ndani ya nchi.
Kiwango hicho cha gesi kunaifanya Tanzania kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kujikinga dhidi ya misukosuko ya bei za mafuta duniani kuliko baadhi ya nchi jirani ambazo hazina rasilimali kubwa za gesi.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati nchini Tanzania, anayeshughulikia masuala ya Mafuta na Gesi Asilia, Dkt James Mataragio alisema kuwa asilimia 10 gesi asilia iliyogundulika na ambayo haijaendelezwa Afrika inapatikana Tanzania.
Dkt Mataragio aliyasema hayo April mwaka huu alipohudhuria maonesho katika Wiki ya Nishati yaliyofanyika katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.
Alieleza kuwa gesi iliyogundulika na ambayo haijaendelezwa Afrika inafikia futi za ujazo trilioni 550, ambapo Tanzania ina futi za ujazo trilioni 57 ambayo ni asilimia 10 ya gesi hiyo iliyogundulika Afrika.
"Tanzania sasa ina jukumu la kuongeza kasi ya matumizi ikiwemo uzalishaji wa umeme, kuongeza kasi ya matumizi ya gesi katika kuendesha viwanda, vyombo vya moto na kutumika katika nishati safi ya kupikia ambapo ifikapo mwaka 2034, asilimia 80% ya Watanzania watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia," alisema.
Kadiri migogoro ya kimataifa inavyoendelea kusababisha bei za mafuta kubadilika mara kwa mara, Tanzania inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya gesi asilia kwa lengo la kuongeza matumizi yake kwenye usafiri, viwanda na majumbani.
Mwezi Mei akiwa London nchini Uingereza wakati akiwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania kwenye Kongamano la Nishati Afrika, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, alisema kuwa sekta ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania ina fursa kubwa na zenye mvuto kwa uwekezaji.
Alisema kuwa utekelezaji unaendelea wa miradi mbalimbali katika mkondo wa juu wa petroli, ikiwemo mradi wa uchimbaji wa visima vya uzalishaji wa gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linalosimamia miradi ya gesi asilia linaendelea kufanya shughuli za utafiti wa mafuta na gesi asilia kwenye vitalu vya Lindi–Mtwara, Eyasi-Wembere, Mnazi Bay Kaskazini na Songo Songo Magharibi.
Gesi kusambazwa mikoa mingine ya Tanzania, Uganda na Kenya
Hivi karibuni, Waziri wa Nishati wa Tanzania, Deogratius Ndejembi katika kuhakikisha kuwa usambazaji wa CNG unafikia maeneo mengi ya nchi, Serikali kupitia TPDC ipo katika hatua za ununuzi wa vituo vitano (5) vya gesi vinavyohamishika (Mobile CNG stations).
Waziri Ndehembi alipokuwa akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake alisema vituo hivyo vinatarajiwa kuwekwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma kwa awamu ya kwanza na mikoa ya Arusha, Tanga na Kilimanjaro kwa awamu ya pili.
Pia alisema katika kuhakikisha kuwa gesi asilia inafika maeneo mbalimbali ya nchi yaliyo mbali na miundombinu ya gesi kwa sasa.
Serikali kupitia TPDC kwa kushirikiana na Sekta Binafsi imewezesha ujenzi wa vituo 18 vya CNG ambavyo vinaendelea kutoa huduma, na vituo vingine nane (8) vipo katika hatua za ujenzi.
Vilevile, hadi Machi, 2026 zaidi ya kampuni binafsi 86 za ndani na nje ya nchi zilikuwa zimepewa idhini ya kuwekeza katika mnyororo wa thamani wa gesi asilia nchini.
Katika kuhakikisha huduma inasambazwa nje ya mipaka Tanzania, Aprili mwaka huu, Wizara ya Nishati ya nchi hiyo ililieleza bunge kuwa Machi mwaka huu Tanzania na Uganda zilisaini mkataba ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Tanzania hadi Uganda.
Sambamba serikali ilisema hatua za mradi wa kusafirisha gesi hiyo kutoka Dar es Salaam (Tanzania) hadi Mombasa (Kenya) ziliendelea na tayari wataalamu wanaendelea kuboresha nyaraka za maridhiano kwa ajili ya kuidhinisha nyaraka muhimu za kumpata mshauri mwelekezi atakayefanya upembuzi yakinifu wa mradi.
Nishati nafuu ya kupikia majumbani
Mbali na kutumika kwenye magari, gesi asilia pia usambazwa majumbani, shuleni na taasisi binafsi kama mbadala wa kuni na gesi lakini pia hutumika katika kuzalisha umeme.
Gesi hutumika kwenye makazi na viwandani katika uendeshaji wa mitambo kwa kuwa inatajwa kuwa nafuu kuliko matumizi ya umeme.
Kwa mijibu wa Wizara ya nishati, kiwango cha Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia kimeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025.
Mafanikio hayo yanatajwa kuwa miongoni mwa makubwa zaidi barani Afrika katika kipindi cha miaka michache iliyopita huku wengi wakitumia gesi asilia, gesi inayohifadhiwa kwenye mitungi (LPG) na wengine umeme.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, mtandao wa usambaji wa gesi asilia upo katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Sallaam.
Kupitia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, Serikali ya Tanzania inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Bei ya gesi dhidi ya mafuta Afrika Mashariki
Licha ya unafuu wa gesi asilia kuonekana kunufaisha Tanzania, nchi zingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilinaendelea kuathirika kutokana na bei ya mafuta kuwa juu huku raia wakilalamika gharama za maisha kupanda.
Bei elekezi ya gesi asilia kwaajili ya magari nchini Tanzania ni shilingi 1,550 za kitanzania (dola 0.59). Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ndio wanaodhibiti ubora na kupanga bei ya nishati hiyo.
Katika taarifa zinazotolewa mara kwa mara na wadhibiti bei ya nishati ya mafuta kwa mataifa ya Jumuiya, inaonesha kuwa pertoli na dizeli zinauzwa hadi dola mbili za kimarekani kwenye baadhi ya mataifa yake kama Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (EWURA), bei ya lita moja ya petroli jijini Dar es Salaam mwezi Juni 2026 ilifikia shilingi za kitanzania 4,086 ( dola 1.57) wakati dizeli inauzwa shilingi 4,333 (sawa na dola 1.66).
Nchini Kenya, mamlaka ya nishati ya Kenya, EPRA ilitangaza bei ya lita moja ya petroli Nairobi kufikia takribani shilingi za Kenya 214 (dola 1.66) kwa lita wakati dizeli iliuzwa kwa shilingi 232.86 (dola 1.8)
Uganda inauza petrolilita moja katika jiji la Kampala kwa shilingi za Uganda 6, 499 sawa na dola 1.75) wakati dizeli inauza wastani wa dola 1.80.
Kutokana na bei hizo kuongezeka kutokana na mzozo baadhi ya viongozi wa Jumuiya wamechukua hatua mbalimbali ikiwemo kupunguza tozo mbalimbali na pia kushauri watendaji wa Serikali kupunguza matumizi ya magari mengi kwenye misafara.
Mwezi April, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu alitangaza kupunguza idadi ya magari kwenye misafara yake mbalimbali ya kikazi ikiwa ni moja ya mkakati wa kupunguza matumizi makubwa ya mafuta serikalini.
Uchumi wa Tanzania na uhitaji wa mafuta

Chanzo cha picha, AFP
Licha ya jitihadi kupunguza matumizi na pia kutumia nishati mbadala kwenye magari kama gesi na umeme, bado kuna uhitaji mkubwa wa mafuta kweye shughuli mbalimbali za kiuchumi
Waziri Ndejembi anasema, "Wastani wa matumizi ya mafuta kwa siku nchini umeendelea kuongezeka na kufikia lita milioni 6.28 kwa petroli na lita milioni 8.42 kwa dizeli ikilinganishwa na lita milioni 5.45 kwa petroli na lita milioni 7.61 kwa dizeli zilizotumika kila siku kwa mwaka 2024/25…
"… ongezeko hilo ni sawa na asilimia 15.23 kwa petroli na asilimia 10.64 kwa dizeli ambalo linaashiria kuendelea kuongezeka kwa mahitaji ya mafuta kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi na kijamii nchini zikiwemo kilimo, ujenzi, usafirishaji, migodi na maendeleo ya viwanda," anaeleza Waziri huyo.















