Silvio Berlusconi : 'Mfalme' wa kujinasua kutoka kashfa moja hadi nyingine ambaye aliongoza Italia mara nne

Iliyochapishwa

Katika ulimwengu wa siasa za Italia, Silvio Berlusconi alikuwa mjasiriamali mwenye haiba kubwa - mtu ambaye aliweza kuunganisha biashara na maisha yake ya siasa zaidi ya mtu mwingine yeyote.

Mbwembwe zake ziliwavutia wapiga kura wa Italia, ambao waliendelea kumuunga mkono licha ya madai ya ufisadi na kashfa kashaa zilizomzunguka.

Alikuwa waziri mkuu mara nne, na kila wakati iliponekana kana kwamba taaluma yake ya kisiasa ilikuwa imekwisha, alifanikiwa kuwachanganya wakosoaji wake na kurejea ulingoni.

Miaka tisa baada ya kupigwa marufuku ya kishikilia ofisi ya umma kwa ulaghai wa kodi, alirejea bungeni, akachaguliwa kuwa Seneta waa Italia kabla ya kutimiza umri wa miaka 86 mwezi Septemba 2022.

Lakini mara nyingi maisha yake ya kibinafsi - kupenda kujizunguka na wasichana warembo, na kashfa za ngono zilizofuata - ambazo ziligonga vichwa vya habari kote duniani.

Berlusconi, ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 86, alikuwa gwiji wa vyombo vya habari, mmiliki wa klabu ya soka na mfanyabiashara bilionea ambaye hakukata tamaa katika siasa - na alisaidia kuunda sura ya Italia kwa miongo kadhaa.

Nyota wa Milan

Silvio Berlusconi alizaliwa katika familia ya tabaka la kati huko Milan mnamo 29 Septemba 1936 na alikulia katika kijiji kilichokuwa viungani mwa jiji wakati wa Vita Vikuu vya pili vya dunia.

Kuanzia wakati alipokuwa mwanafunzi, alionyesha uwezo wa kupata pesa. Alipokuwa akisoma sheria katika chuo kikuu, alicheza gita katika bendi ya wanafunzi - na kujizolea sifa kama mwimbaji, akifanya kazi katika vilabu vya usiku vya burudani na kwenye meli za kitalii.

Mara ya kwanza alifanikiwa kutumia haiba yake ya asili katika biashara ni wakati alipokuwa kama muuzaji wa vifaa vya kusafisha nyamba na kuuza makala maalum zilizoandikwa kwa wanafunzi wenzake.

Baada ya kuhitimu, alianza ujenzi na kampuni yake mwenyewe, Edilnord, akijenga jumba kubwa la ghorofa pembezoni mwa Milan - ingawa chanzo cha ufadhili wa mradi huo ni fumbo ambalo halijawahi kupata jibu.

Mnamo 1973, mfanyabiashara huyo alizindua kampuni ya televisheni ya cable inayoitwa Telemilano kutoa huduma za televisheni kwa mali yake.

Miaka minne baadaye, alimiliki vituo viwili zaidi na studio kuu ya Milan. Mwishoni mwa muongo huo, alikuwa ameunda kampuni inayomiliki, Fininvest, kusimamia upanuzi wa haraka wa umiliki wake wa biashara.

Hatimaye, ilimiliki Mediaset - himaya kubwa zaidi ya vyombo vya habari nchini Italia na mmiliki wa stesheni kubwa zaidi za kibinafsi nchini - na shirika kubwa la uchapishaji la Italia, Mondadori.

Kufikia wakati wa kifo chake, alikuwa mmoja wa watu tajiri zaidi wa Italia, na familia yenye utajiri wa mabilioni ya dola. Watoto wake - Marina, Barbara, Pier Silvio, Eleonora na Luigi - wote wameshiriki katika uendeshaji wa himaya yake ya biashara.

Baadhi ya utajiri huo ungetumika kutimiza maslahi yake binafsi - ikiwa ni pamoja na kuokoa klabu yake ya soka ya AC Milan dhidi ya kufilisika mwaka 1986.

Uwekezaji huo ungelipa miongo mitatu baadaye mwaka wa 2017, alipoiuza klabu hiyo kwa wawekezaji wa China kwa £628m (€740m).

Hakukata tamaa katika soka pia, baadaye alinunua klabu ya soka ya Monza na kufurahia kupanda kwake hadi kwenye ligi kuu ya Serie A kwa mara ya kwanza katika historia yake.

Nguvu za kisiasa na uchunguzi wa ufisadi

Uwezo wa ajabu wa Berlusconi wa kukabiliana na mahakama mara kwa mara - na kudumisha umaarufu wake katika siasa - haukuwa na kifani.

Mara kadhaa alilalamikia kudhulumiwa - haswa na waendesha mashtaka katika mji wake wa kuzaliwa wa Milan - wakati mmoja akidai kuwa alifika mahakamani mara 2,500 katika kesi 106 zilizomkabili kwa miaka 20.

Mashtaka yaliyomkabili kwa miaka kadhaa yalijumuisha ubadhirifu, ulaghai wa kodi na uhasibu wa uwongo, na kujaribu kuhonga hakimu. Aliachiliwa au hukumu zake zibatilishwa mara kadhaa.

Kashafa zake zilikuwa dhahiri na zilikuwa mambo ya kawaida katika maisha yake yote ya kisiasa. Mnamo Februari 2023 aliondolewa hatia ya kuwahonga mashahidi ili kusema uwongo kuhusu karamu za "bunga bunga" ambazo alikuwa amezifanya katika jumba lake la kifahari kama waziri mkuu.

Alikuwa ameanzisha chama chake cha kisiasa miaka 30 mapema mwaka 1993 na ndani ya mwaka mmoja, aling'olewa madarakani.

Akiongeza shauku yake kwa soka, alikiita chama chake kutokana na wimbo wa wafuasi - Forza Italia (Nenda Italia). Wakati huo, upungufu wa mamlaka ulikuwa umeibuka kutokana na kashfa iliyoathiri mrengo wa kulia wa kati wa Italia - na Berlusconi alitoa njia mbadala kwa wale wapiga kura ambao hawakuwa wa mrengo wa kushoto.

Kampeni kubwa ya utangazaji kwenye vituo vyake vya Televisheni ilimsaidia kupata ushindi katika uchaguzi wa 1994.

Hata hivyo, hamu yake mpya ya siasa ilionekana kama nia ya kuepuka kuhusishwa na mashtaka ya ufisadi yeye binafsi, baada ya biashara zake kadhaa kuhusishwa katika uchunguzi huo.

Lakini alitupilia mbali madai hayo. "Sihitaji kuingia ofisini kwa ajili ya mamlaka. Nina nyumba duniani kote, boti za kifahari, ndege nzuri, mke mzuri, familia nzuri. Ninajitolea."

Mara tu alipokuwa madarakani, serikali ya Berlusconi ilipitisha sheria iliyompa yeye, na viongozi wengine wakuu wa umma, kinga ya kutoshtakiwa akiwa madarakani, lakini baadaye ikatupiliwa mbali na mahakama ya kikatiba.

'Mfalme' wa kujinasua kutoka kwenye kashfa

Muungano wa kwanza wa Berlusconi ulidumu kwa miezi michache tu - kwa kiasi fulani kutokana na mvutano kati ya pande tofauti ndani yake, na kwa kiwango fulani kutokana na mashtaka dhidi ya Berlusconi kuhusiana na madai ya ulaghai wa kodi yaliyofikishwa mbele ya mahakama ya Milan.

Alishindwa katika na mrengo wa kushoto katika uchaguzi wa 1996 - lakini maisha yake ya kisiasa ndiyo mwanzo yalikuwa yanaanza.

Mnamo 2001, Berlusconi alirejea kama waziri mkuu, akiwa mkuu wa muungano mpya unaojulikana kama House of Freedoms. Ujumbe mkuu wa kampeni yake ya uchaguzi ulikuwa ahadi ya kurekebisha uchumi wa Italia, kurahisisha mfumo wa ushuru na kuongeza pensheni.

Lakini thamani ya sarafu ya Italia ilidorora kutokana na hali mbaya ya uchumi wa dunia, na Berlusconi hakuweza kutimiza ahadi zake. Alidhindwa na Mrengo wa Kushoto mnamo 2006 - lakini akarejea tena madarakani mwaka 2008.

Alisalia kuwa mshiriki katika siasa za Italia hadi 2011, ambayo ingedhihirisha kuwa wakati mgumu sana katika safari yake ya siasa.

Gharama za kukopa za Italia zilipanda wakati wa mzozo wa deni la kanda ya euro. Waziri Mkuu alilazimika kujiuzulu baada ya kupoteza wingi wake wa ubunge.

Mwaka huo huo, mahakama ya kikatiba ilitupilia mbali sehemu ya sheria iliyompa yeye na mawaziri wengine wakuu kinga ya muda.

Kufikia mwisho wa 2011, alikuwa likuwa ameondolewa mamlaka. Mnamo Oktoba 2012, alihukumiwa kifungo cha miaka minne kwa ulaghai wa ushuru na kuzuiwa kuhudumu katika ofisi ya umma. Berlusconi alitangaza kutokuwa na hatia na alizungumzia "mapinduzi ya mahakama".

Lakini kufikia wakati huo, alikuwa na umri wa zaidi ya miaka 75 na badala yake alikabidhiwa huduma ya jamii. Alifanya kazi kwa saa nne kwa wiki na wagonjwa wazee wenye changamoto za kiakili katika nyumba ya utunzaji ya Wakatoliki karibu na mji wa Milan.

Pia alipigwa marufuku ya kushikilia ofisi ya umma - marufuku ambayo ilidumu kwa miaka kadhaa kabla arejee tena ulingoni.

Sherehe za Bunga-bunga na maisha ya kibinafsi ya umma

Mbali na siasa, Berlusconi aligonga vichwa vya habari katika maisha yake ya kibinafsi, ambayo mara nyingi aliyaweka hadharani.

Waziri mkuu huyo mwenye mbwembwe nyingi hakuficha harakati zake za kujihusisha kimapenzi na wanawake wachanga.

Alizidi umri mpenzi wake wa hivi karibuni, mwenzake wa chama Marta Fascina, kwa zaidi ya miaka 50. Alijulikana kutumia upandikizaji wa nywele na kufanya upasuaji wa urembo ili kujifanya kuwa mdogo.

Alikutana na mke wake wa pili, Veronica Lario, baada ya kucheza bila nguo katika mchezo wa kuigiza. Lakini baadaye aliekuelezea jinsi alivyofadhaika hadharani kutokana na tabia ya mume wake ya kujihusisha kimapenzi na wasichana zaidi ya mara moja.

Aliomba talaka baada ya mumewe kupigwa picha kwenye sherehe ya miaka 18 ya kuzaliwa kwa mwanamitindo Noemi Letizia.

Kashfa yake dhidi yake zaidi ilitokana na madai katika sherehe za "bunga bunga" zilizoandaliwa katika jumba lake la kifahari, na kuhudhuriwa na wasichana wa maonyesho - hadithi ambayo iliishia katika hatia ya kumlipa kahaba wa umri mdogo kwa ajili ya ngono.

Hatimaye iliibuka kuwa mwaka wa 2010, Berlusconi, akiwa waziri mkuu, alipiga simu kituo cha polisi na kuomba kuachiliwa kwa Karima "Ruby" El Mahroug mwenye umri wa miaka 17, aliyepewa jina la utani la Ruby Heart-Stealer, ambaye alikuwa akishikiliwa kwa wizi. Pia aliripotiwa kuwa mgeni wa sherehe za "bunga bunga".

Vyombo vya habari vya Italia viliripoti kwamba waziri mkuu alidai msichana huyo alikuwa mpwa au mjukuu wa rais wa Misri, na alikuwa akijaribu kukwepa tukio la kidiplomasia.

Berlusconi alipatikana na hatia ya kumlipa ili kustarehe naye na kutumia vibaya mamlaka yake mwaka 2013 - lakini uamuzi huo ulibatilishwa mwaka uliofuata.

Kwa upande wake, Berlusconi kila mara alikataa madai kwamba alikuwa amemlipa mwanamke yeyote kwa ajili ya kustarehe naye, akisema kufanya hivyo ni "kukosa raha ya ushindi". Lakini pia alikiri kuwa "si mtakatifu".