Alex Soros: Mfahamu mrithi wa utajiri wa bilionea George Soros

Iliyochapishwa

Bilionea Mmarekani George Soros ameamua kuwa mwanawe Alex atasimamia himaya yake kifedha na hisani yenye thamani ya dola bilioni 25.

Bw Soros, 92, mwenye asili ya Hungary, alisema katika mahojiano na Wall Street Journal kwamba mtoto wake "alistahili".

Tangu miaka ya 1990, sehemu ya utajiri wa familia hiyo imeenda kusaidia ujenzi wa demokrasia katika nchi kadhaa. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, George Soros amekuwa mlengwa wa njama dhidi ya Wayahudi na makundi ya mrengo wa kulia kwa mujibu wa msemaji wa bilionea huyo akithibitisha maelezo ya mahojiano yaliyochapishwa Jumapili kwa BBC.

Wasifu wa mrithi

Alex Soros, 37, ana shahada katika historia na ndiye mwana wa mwisho wa ndugu watano.

Yeye ndiye mwanafamilia pekee kuhudumu katika kamati ya uwekezaji ya Usimamizi wa Mfuko wa Soros, ambayo inasimamia dola bilioni 25 na msingi wake wa hisani, kulingana na Wall Street Journal.

Baba yake mzaliwa wa Hungary George Soros aliishi katika enzi za Nazi wakati wa Vita vya vya pili vya Dunia. Familia yake ilificha utambulisho wao wa Kiyahudi ili kuishi.

Baada ya vita, aliondoka Hungary na kuhamia London, kisha New York, ambako alipata mabilioni kupitia biashara zake.

Soros alikuja kujulikana nchini Uingereza baada ya kushinda kamari ya dola bilioni 1 kwenye anguko la pauni mwaka wa 1992.

Wakati Ukuta wa Berlin ulipoanguka, na kufungua njia ya kuanzishwa kwa serikali za kidemokrasia katika kambi ya zamani ya Soviet, aliunda Wakfu wa Open Society (OSF) kusaidia mchakato huo.

Leo, OSF inatoa kiasi cha dola bilioni 1.5 kila mwaka kwa mashirika ya elimu na haki za binadamu katika zaidi ya nchi 120.

Uhusiano na siasa

George Soros ni mmoja wa wafadhili wakubwa wa Chama cha Democratic nchini Marekani.

Mwanawe Alex, ambaye ana maoni mapana ya kisiasa kama baba yake, aliambia Wall Street Journal kuwa "anaegemea siasa zaidi" na atafanya kampeni dhidi ya azma ya Donald Trump ya kuwania muhula wa pili kama rais wa Marekani.

"Kama vile ningependa kuchukua pesa kutoka kwa siasa, mradi tu upande mwingine unafanya, lazima tufanye hivyo," alisema Alex Soros, ambaye anahusika na "super PAC" ya baba yake, mfumo unaotoa fedha kwa vyama vya siasa nchini Marekani.

Kulingana na mwanawe, Open Society Foundations itafuata malengo sawa na babake, kama vile uhuru wa kujieleza, mageuzi ya haki ya jinai, haki za wachache na wakimbizi, na uungwaji mkono kwa wanasiasa huria.

Lakini pia anataka kujumuisha mipango ya kupiga kura, utoaji mimba na usawa wa kijinsia, huku akitaka kuzingatia ajenda inayozingatia zaidi Marekani.

Baadhi ya sababu zake zimechochewa na haki, kama vile vita dhidi ya ubaguzi wa rangi katika mfumo wa haki wa Marekani.

OSF ilihamisha ofisi yake ya oparesheni za kimataifa kutoka Budapest hadi Berlin mnamo 2018 baada ya serikali ya Hungary iliyoongozwa na Viktor Orban kuendesha kampeni ya wazi dhidi ya Soros na dhidi ya kazi ya taasisi yake.

Alex Soros ni shabiki wa hip-hop na timu ya soka ya New York Jets. Anajulikana pia kwa kuishi maisha hadhi ya juu, akihudhuria karamu za watu mashuhuri huko Cannes na Hamptons.

Pia amesafiri hadi maeneo ya mbali ya Amazon na kuketi kwenye bodi ya shirika la kutetea haki za binadamu la Global Witness.

"Kambi yetu inahitaji kuwa ya kizalendo na jumuishI zaidi," aliambia Wall Street Journal.

"Kwa sababu tu mtu anampigia kura Trump haimaanishi kuwa amepotea au ni mbaguzi."