Tukio la kupewa sumu wanafunzi 650 wa kike nchini Iran, kilitokea nini?

Chanzo cha picha, IRNA
BBC imebaini kuwa takribani wasichana 650 wa shule waliotiwa sumu nchini Iran Afisa mkuu wa serikali hatimaye alikiri kwamba wasichana hao walikuwa wakilengwa makusudi.
Hakuna msichana wa shule aliyeuawa. Lakini watu kadhaa wamelazwa hospitalini wakiwa na matatizo ya kupumua, kichefuchefu, kizunguzungu na uchovu.
"Ni wazi kwamba baadhi ya watu wanataka shule zote, hasa za wasichana, zifungwe," Naibu Waziri wa Afya wa Iran Younes Panahi aliuambia mkutano na waandishi wa habari Februari 26.
Taarifa pekee rasmi iliyotolewa hadi sasa inasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameanzisha uchunguzi wa jinai kuhusu sumu hiyo na kwamba huenda kitendo hicho kilikuwa cha 'makusudi'.
Kwa muda wa miezi mitatu iliyopita, wasichana wa shule wameripoti kunusa machenza au samaki waliooza kabla ya kuugua.
"Kemikali zinazotumika si za daraja la kijeshi na zinapatikana kawaida.
Wanafunzi hawahitaji matibabu yoyote ya dharura. Ni muhimu kuwa watulivu," alisema Dk Panahi.
Baadaye, alisema kauli yake 'haikueleweka'. Ingawa hakuna wahusika ambao wametajwa hadharani, ni ishara ya mgawanyiko kati ya mamlaka juu ya jinsi ya kukabiliana na hasira ya umma.
Mji wa kidini wa Qom ndio kitovu cha tukio hili la sumu. Lakini tukio hili lilitokea katika miji minane kote Iran. Kero ya umma kuhusu hili inaendelea kuongezeka.
Mnamo Novemba 20, 2022, wanafunzi 18 wa kike kutoka Shule ya Ufundi ya Noor huko Qom walipelekwa hospitalini wakiwa na dalili za kupewa sumu. Hilo lilikuwa tukiola kwanza la sumu.
Tangu wakati huo, zaidi ya shule 10 za wasichana katika jimbo hilo zimekuwa zikilengwa.

Chanzo cha picha, IRNA
Katikati ya Februari, takribani watu 100 waliandamana nje ya ofisi ya gavana huko Qom.
"Nina mabinti wawili. Una deni kwangu kuhakikisha usalama wa watoto wangu! Mabinti wawili. Kitu pekee ninachoweza kufanya ni kutowapeleka shule," baba mmoja alifoka kwenye video iliyosambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii.
"Hii ni vita! Wanafanya hivi katika shule za sekondari za wasichana huko Qom ili kutufanya tukae nyumbani. Wanataka wasichana wabaki nyumbani," alisema mwanamke mmoja katika umati huo.
Baadhi ya wazazi wanaripoti kwamba watoto wao walikuwa wagonjwa kwa wiki kadhaa baada ya kupewa sumu.
Video nyingine iliyochukuliwa hospitalini inaonesha msichana akiwa amelala kitandani na mama yake.
Jamani akina mama mimi ni mama mtoto wangu amelazwa hospitali mikono na miguu imelegea, ninamfinya lakini hahisi chochote naomba msiwapeleke watoto shule,” anasema mama huyo mwenye huzuni. .
Hofu ya Wairani
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ilitokea katika mji wa Qom, nyumbani kwa viongozi wa kidini wa Uislamu wa Shia, uti wa mgongo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Lakini mamlaka ya viongozi wa kidini yametiliwa shaka tangu kifo cha Masa Amini, msichana wa Kikurdi ambaye aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi Septemba mwaka jana baada ya kudaiwa kushindwa kuvaa hijabu yake 'vizuri'.
Baadhi ya Wairani wanaamini kuwa shambulio dhidi ya wanafunzi hao wa kike lilitokana na ushiriki wao katika maandamano makubwa ya kuipinga serikali yaliyofuata. Mitandao ya kijamii imefurika picha za wasichana wa shule wakivua hijabu zao.
Wengi wanakisia kuwa mashambulizi hayo ni kazi ya watu wenye msimamo mkali ambao wanataka kutenda kama Taliban nchini Afghanistan na kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Boko Haram nchini Nigeria, wakiwatishia wazazi kuacha kuwapeleka wasichana wao shule.
"Je, Boko Haram Wamefika Iran?" Mohammad Ali Abdahi, Makamu wa Rais wa zamani wa Iran, aliuliza katika chapisho la Instagram.

Chanzo cha picha, Twitter
Mwanamageuzi na mwanasiasa huyo pia alionya kwamba "wenye msimamo mkali watachora mipaka ya serikali na dini kwa niaba yao."
Utawala wa Iran umekataa ukosoaji wa vikwazo kwa wanawake, kama vile hijabu ya lazima, na badala yake inajivunia idadi ya wanawake wanaojiunga na chuo kikuu.
Lakini ikiwa wasichana hawatamaliza shule, chuo kinakuwa ndoto tu.
Msichana wa shule alisema alilishwa sumu mara mbili katika mkutano na gavana wa Gome, akiangazia jinsi baadhi ya taarifa za mamlaka zilivyokuwa zisizoeleweka na zisizo sahihi.
"Walituambia (viongozi) kila kitu kipo sawa na tumekamilisha upelelezi. Lakini baba alipouliza shuleni kwangu, walisema, 'CCTV iko chini kwa wiki moja, hatuwezi kuchunguza hili. Samahani'," aliuambia mkusanyiko.
"Niliponyweshwa sumu kwa mara ya pili Jumapili, mkuu wa shule alisema, 'Ana ugonjwa wa moyo. Ndiyo maana yuko hospitalini'. Lakini sina ugonjwa wowote wa moyo!" Alisema mwanafunzi huyo.














