Kutoka vita hadi mazungumzo: Safari ngumu ya amani kati ya Wahouthi na Saudi Arabia

.

Chanzo cha picha, Reuters

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Kulingana na gazeti la Axios, Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, amemwomba Rais wa Marekani Donald Trump kuunga mkono uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Wahouthi, baada ya kuzuka kwa tuhuma kwamba ndege ya Iran ilijaribu kusafirisha silaha na wataalamu wa kijeshi kwenda kwa kundi hilo kupitia Uwanja wa Ndege wa Sanaa.

Ripoti hiyo ilieleza kuwa uwanja huo wa ndege ulishambuliwa kwa mabomu, huku Wahouthi wakijibu kwa kuushambulia Uwanja wa Ndege wa Abha nchini Saudi Arabia.

Hilo ndilo shambulio la kwanza lililotangazwa dhidi ya Saudi Arabia tangu kuanza kwa makubaliano yasiyo rasmi ya kusitisha mapigano mwaka 2022.

Matukio haya yameibua maswali kuhusu mustakabali wa usitishaji huo wa mapigano na uwezekano wa hali ya usalama kuzorota kwa mara nyingine.

Wahouthi ni kina nani?

Kundi la Wahouthi, inayojulikana pia kama Ansar Allah, ina mizizi yake katika mkoa wa Saada, kaskazini mwa Yemen.

Kundi hilo lilianzishwa na Hussein Badreddin al-Houthi, mwana wa mwanazuoni mashuhuri wa madhehebu ya Zaydi, Badreddin al-Houthi.

Katika miaka ya 1970 na 1980, Badreddin al-Houthi alijitokeza kama mpinzani mkubwa wa itikadi ya Kisalafi, akipinga kile ambacho Wahouthi walikitaja wakati huo kuwa ni kuenea kwa "Uwahabi wa Saudi" nchini Yemen. Kwa mujibu wa simulizi la Wahouthi, msimamo huo ulimfanya akabiliwe na shinikizo na mateso ya kisiasa.

Harakati hiyo ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 wakati Hussein Badreddin al-Houthi alipoingia katika siasa na kuanzisha chama cha upinzani cha Al-Haq, kilichowajumuisha viongozi wa kisiasa na wa kidini.

Katika uchaguzi wa bunge wa mwaka 1993, Hussein al-Houthi alichaguliwa kuwa mbunge wa kuwakilisha Mkoa wa Saada kupitia chama hicho.

Mapambano ya kwanza ya moja kwa moja ya kijeshi kati ya Wahouthi na Saudi Arabia

Operesheni iliyopewa jina la "Operation Decisive Storm" mwaka wa 2015 haikuwa mapambano ya kwanza ya kijeshi kati ya Saudi Arabia na kundi la Wahouthi, linalojulikana kama Ansar Allah.

Mwezi Novemba tarhe 5, mwaka wa 2009, wapiganaji wa kundi hilo waliingia katika kijiji cha mpakani cha Al-Khoba kilichoko katika eneo la Jazan nchini Saudi Arabia, kama sehemu ya jaribio la kudhibiti Mlima Dukhan kwa kile kilichojulikana kama "Vita vya Sita" kati ya Wahouthi na serikali ya Yemen iliyoongozwa na aliyekuwa Rais Ali Abdullah Saleh.

Rais wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh, aliuawa mwaka wa 2017

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh, aliuawa mwaka wa 2017

Saudi Arabia ilijibu kwa kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya mamia ya wapiganaji wa Wahouthi waliokuwa wamewashambulia walinzi wao wa mpakani. Siku tatu baadaye, Saudi Arabia ilitangaza kuwa ilikuwa imerejesha udhibiti wa Mlima Dukhan.

Mapigano yaliendelea hadi mwezi Februari mwaka wa 2010. Baada ya kipindi hicho, Riyadh ilianza kuwaona Wahouthi kama tishio linaloweza kuhatarisha usalama katika mpaka wake wa kusini.

Kuanzia mapinduzi ya Arab Spring hadi kutekwa kwa Sanaa

Mwaka wa 2011, Yemen ilishuhudia maandamano makubwa ya wananchi kama sehemu ya matukio ya Arab Spring, ambayo yalimalizika kwa kujiuzulu kwa Rais Ali Abdullah Saleh mwezi Februari mwaka wa 2012 chini ya Mpango wa Nchi za Ghuba.

Mpango huo ulielekeza kufanyika kwa uhamisho wa madaraka kwa njia ya amani kwenda kwa makamu wake, Abd Rabbuh Mansur Hadi, kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, pamoja na kumpa Saleh kinga dhidi ya mashtaka kwa sharti la yeye kuachia madaraka.

Wahouthi walitumia udhaifu wa serikali na msukosuko wa kisiasa kupanua ushawishi wao wa kijeshi na kisiasa kaskazini mwa Yemen. Hatimaye, walitwaa udhibiti wa mji mkuu, Sanaa, mwezi Septemba mwaka wa 2014.

Hatua hiyo ilifanyika wakati Wahouthi walikuwa na ushirikiano usiotangazwa rasmi na aliyekuwa Rais Ali Abdullah Saleh, ambao uliwapa uungwaji mkono wa kisiasa na kijeshi uliowawezesha kudhibiti taasisi muhimu za serikali.

Maamuzi

Baada ya Rais Abd Rabbuh Mansur Hadi kukimbilia Saudi Arabia, Riyadh ilianzisha "Operation Decisive Storm" mwezi Machi mwaka wa 2015, ikiongoza muungano wa nchi za Kiarabu kwa lengo la kuiunga mkono serikali ya Yemen.

Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Ulinzi, alisimamia operesheni hizo za kijeshi.

Muungano huo ulijumuisha Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Kuwait na Qatar kabla ya Qatar kujiondoa mwaka 2017 kufuatia mgogoro wa nchi za Ghuba, pamoja na Misri, Jordan, Morocco na Sudan.

Ingawa Pakistan ilijadili uwezekano wa kushiriki katika muungano huo mwanzoni, bunge lake lilipiga kura mwezi Aprili mwaka wa 2015 na kuamua nchi hiyo ibaki katika msimamo wa kutofungamana na upande wowote katika mzozo huo.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Makombora, ndege zisizo na rubani na mzozo wa kibinadamu

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kipindi cha vita, Wahouthi walitumia makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani kushambulia viwanja vya ndege, miundombinu ya mafuta na miji ya mpakani ndani ya Saudi Arabia.

Mashambulizi yaliyogonga vichwa vya habari zaidi ni lile lililolenga vituo vya Aramco katika Abqaiq na Khurais mwezi Septemba mwaka wa 2019, shambulio ambalo Washington na Riyadh ziliishutumu Tehran kwa kulipanga au kuliunga mkono.

Wakati huo, Saudi Arabia na Marekani ziliishutumu Iran hadharani kwa kuwasambazia Wahouthi silaha, makombora, ndege zisizo na rubani na utaalamu wa kijeshi. Kwa upande wake, Riyadh iliona ushawishi wa Iran kupitia Wahouthi kuwa tishio la moja kwa moja kwa usalama wake na mipaka yake ya kusini.

Kwa kujibu, muungano ulioongozwa na Saudi Arabia ulianzisha mashambulizi makubwa ya anga ndani ya Yemen. Mashambulizi hayo yalizua ukosoaji mkali kutoka kwa mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu na wataalamu wa Umoja wa Mataifa kutokana na athari kubwa za kibinadamu zilizosababishwa na vita hivyo.

Ripoti za Umoja wa Mataifa za wakati huo zilionyesha kuwa takriban Wayemeni milioni 17 walikuwa wanahitaji kwa dharura msaada wa chakula, huku karibu watu milioni 7 wakiwa katika hatari ya kukumbwa na njaa kali. Aidha, mlipuko wa kipindupindu ulisababisha vifo vya karibu watu 2,000.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Wasiwasi wa Riyadh na hatua ya kujaribu kupunguza mvutano

Katika kipindi cha vita, wasiwasi mkuu wa Saudi Arabia ulikuwa uwezekano wa Wahouthi kuwa na nguvu ya kudumu ya kijeshi katika mpaka wake wa kusini, kuongezeka kwa uwezo wao wa kutumia makombora, matumizi ya Wahouthi na Iran kama chombo cha kuongeza shinikizo la kikanda, pamoja na tishio kwa usalama wa usafiri wa majini katika Bahari Nyekundu na Mlango wa Bahari wa Bab al-Mandab.

Mwezi Aprili tarehe 1, mwaka wa 2022, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa, Hans Grundberg, alitangaza kuwa pande zote mbili zilikuwa zimekubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa miezi miwili, huku makubaliano hayo yakiwa yanaweza kuongezwa muda. Usitishaji huo wa mapigano ulianza kutekelezwa mwezi Aprili 2, mwaka wa 2022.

Makubaliano hayo yalielekeza kusitishwa kwa operesheni zote za mashambulizi kupitia nchi kavu, baharini na angani.

Ingawa usitishaji wa mapigano ulimalizika rasmi baadaye, hali ya utulivu isiyotangazwa rasmi iliendelea, huku mawasiliano ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili yakianza.

Maridhiano kati ya Saudi Arabia na Iran

.

Chanzo cha picha, Wana News Agency/Reuters

Baada ya usitishaji wa mapigano, Saudi Arabia na Iran zilirejesha uhusiano wao wa kidiplomasia kupitia upatanishi wa China mwezi Mei mwaka wa 2023. Aidha, Riyadh ilifanya mazungumzo ya moja kwa moja na Wahouthi katika juhudi za kufikia makubaliano ya kudumu ya amani.

.

Chanzo cha picha, Saba News Agency/Reuters

Mnamo Septemba 2023, ujumbe wa Wahouthi ulifika Riyadh katika ziara ya kwanza ya wazi ya aina hiyo tangu kuanza kwa vita. Mazungumzo hayo, yaliyosimamiwa na wapatanishi wa Oman, yalidumu kwa siku tano na kuzaa makubaliano ya kumaliza mgogoro huo.

Hata hivyo, matukio ya hivi karibuni yanayohusiana na viwanja vya ndege vya Sanaa na Abha yameleta tena mjadala kuhusu kile kinachoweza kuitwa "udhaifu" wa usitishaji wa mapigano ambao umekuwa ukidumu tangu mwaka 2022.