Mwanajeshi wa Israel ahukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa tuhuma za kufanyia Iran upelelezi
Mahakama ya kijeshi nchini Israel imemhukumu askari kifungo cha miaka mitano jela kwa madai ya kutoa taarifa nyeti kwa "wakala wa Iran" ili kupata malipo.
Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama, askari huyo—ambaye jina lake halijatolewa hadharani—alituma video zinazoonyesha kukatizwa kwa makombora mawili kwa "wakala wa Iran" wakati wa vita vifupi vilivyotokea mwaka jana kati ya Israel na Iran.
Mamlaka za mahakama nchini Israel zilikuwa zimeomba adhabu kali zaidi kwa askari huyo, lakini mahakama ilitoa hukumu hafifu zaidi ikizingatia kuwa alisitisha kwa hiari uhusiano wake na "wakala wa Iran," kisha akatoa taarifa kwa makamanda wake na kukiri kosa la upelelezi.
Mbali na kifungo cha miaka mitano jela, askari huyo pia alihukumiwa kulipa faini na kushushwa cheo hadi askari wa kawaida.









