Polisi wa Urusi waliozongwa na kazi, kukatishwa tamaa wanavyoacha kazi

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Olesya Gerasimenko
- Nafasi, BBC Russian
- Iliyochapishwa
Mnamo Januari 14 mwaka 2020, mwendo wa alfajiri mayowe yalisikika kwenye jengo la ghorofa katika eneo la Krasnodar kusini mwa Urusi.
Mkazi mmoja aliyekuwa na hofu alipiga simu polisi kuripoti kile kilichosikika kama shambulio dhidi ya mwanamke.
Lakini hakuna mtu aliyekuja.
Mayowe yaliendelea, sambamba na kishindo kikubwa na vilio vya kuomba msaada. Simu sita zaidi zilipigwa kwa huduma za dharura lakini hakuna maafisa wa polisi waliofika.
Majirani, waliokuwa wakihofia mabaya zaidi, waliamua kuchukua hatua mikononi mwao na kuingia ndani ya ghorofa hilo kwa kuvunja mlango.
Lakini walikuwa wamechelewa sana.
Mayowe yalikuwa yamekoma. Mwanamke huyo alikuwa amekufa.
Polisi hawapokei simu
Vera Pekhteleva alikuwa amedungwa kisu mara kadhaa, kupigwa na kunyongwa kwa kamba ya chuma na mpenzi wake wa zamani katika shambulio lililochukua saa tatu na nusu.

Chanzo cha picha, FAMILY HANDOUT
Wakati huo, polisi walisema hakukuwa na maafisa au magari ya doria katika eneo hilo. Lakini baadaye, maafisa watano walipatikana na hatia ya kusababisha kifo kwa uzembe na walihukumiwa kifungo cha miezi 18 jela, kusimamishwa kazi kwa miaka miwili.
Mahakama ilisema hukumu hizo, ambazo zilionekana na wengi kuwa nyepesi, zinafaa kwa sababu uhaba wa maafisa ulikuwa tatizo kwa "jeshi zima".
Urusi ina mojawapo ya vikosi vikubwa zaidi vya polisi duniani, ikiajiri zaidi ya maafisa 900,000 kuhudumia idadi ya watu milioni 146, kulingana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Urusi. Ina takriban maafisa 630 kwa kila watu 100,000 - zaidi ya mara mbili ya Marekani au Uingereza.
Lakini mwezi Agosti, Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Vladimir Kolokoltsev alisema nchi hiyo ina uhaba "muhimu" wa maafisa wa polisi, ambao unaweza kuchangia kupanda kwa viwango vya uhalifu.
Je, inawezaje kuwa hivyo, kwa kuzingatia idadi kubwa ya maofisa hao?
Mishahara duni, dhiki na rushwa
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ukubwa wa Urusi na ukosefu wa wafanyikazi wa usaidizi ofisini ni sehemu ya changamoto inayokabili jeshi la polishi nchini humo. Lakini matatizo ya hivi majuzi yanatokana na kupungua kwa idadi kubwa ya polisi - na wengi wanaoondoka ni maafisa wenye uzoefu.
Maafisa wengi wa zamani wa polisi wa Urusi wameiambia BBC kuwa wanaondoka jeshini na kujiunga na kazi zisizo na msongo wa mawazo ambazo zinalipa vizuri zaidi.
"Hawajarekebisha mshahara hata kidogo," afisa wa zamani kutoka Rostov, kusini magharibi mwa Urusi, alisema. "Baada ya mfumuko wa bei mshahara haukidhi mahitaji, hautoshi." Aliacha kazi kuwa dereva wa teksi.
Rafiki yake, ambaye pia alikuwa afisa wa polisi, sasa ni mjumbe.
Wote wawili wanapata mara mbili ya mshahara wao walipokuwa maafisa wa polisi.
"Nilifikia cheo cha meja. Lakini bado mtu anayefanya kazi katika duka kubwa alipata pesa nyingi zaidi kuniliko - kazi hatari sana. Ni mjinga tu ndiye atajiunga na polisi sasa," afisa wa zamani wa Rostov sema.
BBC imegundua kuwa vikosi vya polisi vilivyozidiwa sasa vinakataa kuwasilisha malalamiko rasmi, hata baada ya taarifa kutolewa.
"Kila mtu hupata siku 10 za kuchunguza taarifa, ikiwa kuna tano au 50, kwa hiyo ni wazi, ubora wa kazi unazorota," asema mpelelezi mmoja kutoka eneo la Siberia la Urusi.
"Ikiwa kuna msururu wa mambo 10 au zaidi wanapaswa kufanya - kuwaita majirani, kuwahoji mashahidi, kutembelea eneo la uhalifu - watafanya moja au mbili, na kuandika kwamba 'haiwezekani' kukamilisha mengine.
"Kisha wanakataa kufungua mashtaka - kwa hivyo hakutakuwa na uchunguzi," anasema.

Chanzo cha picha, EPA
Kadiri idadi ya maafisa inavyopungua, shinikizo kwa wale waliosalia huongezeka.
Maafisa wa zamani wameambia BBC kuwa hii inasababisha ufisadi.
"Maafisa wanawapiga watu na kuwalazimisha kukiri makosa, Kamata kamata inaongezeka, tunaona hii kila wakati," anasema mkuu wa polisi kutoka jiji la Tomsk.
"Hali itazidi kuwa mbaya. Kutakuwa na upotoshaji wa ushahidi, vipigo vilivyolengwa, hakutakuwa na wakati wa kuchunguza chochote ipasavyo.
"Una uongozi na unahitaji kuufukuza? Ni rahisi zaidi kumburuta mshukiwa wa kwanza hadi kituoni na kumpiga, kwa hivyo analaumiwa."
Maafisa wengine wanafungwa kwa kukiuka sheria - Hii inaathiri nguvu kazi.
Hali kama hii ilimpata Sergei, afisa wa zamani wa polisi wa miaka sita, aliyefungwa jela kwa kumpiga mlanguzi wa dawa za kulevya. Sergei anasema alihisi shinikizo la kumkamata mfanyabiashara huyo na kumpiga tu alipokuwa karibu kula dawa zake ili kuficha ushahidi.
Pia anaambia BBC kwamba rasilimali za polisi zimedorora sana ilibidi alipe mwenyewe mahitaji muhimu ya kazi. "Nilikuwa nikitumia gari langu mwenyewe, nilinunua karatasi yangu, vifaa vya kuchapisha makaratasi; kompyuta yangu, meza yangu, kiti changu, petroli yangu... Nilitengeza ofisi yangu mwenyewe, nikarekebisha kila kitu."
Afisa wa zamani kutoka Urusi ya kati anasema kuwa nafasi zilizoachwa wazi hazijajazwa kwa muda mrefu. "Kumekuwa na uhaba kwa miaka mingi. Nilianza 2015, na ni watu wawili tu wamejiunga na timu yetu katika miaka minane iliyopita, wakati 15 wameondoka."
Na kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya BBC, ikiwa ni pamoja na sajenti wawili na meja mmoja, Wizara ya Mambo ya Ndani ilifanya msako wa maafisa ambao walikuwa na uhusiano na mwanasiasa wa upinzani, Alexei Navalny, ambaye amekuwa akishikiliwa katika jela la mbali tangu 2021.
Maafisa wa muda mrefu, wenye uzoefu walifukuzwa kazi katika msako huo. Chanzo kimoja kilisema Huduma ya Usalama ya Shirikisho la Moscow ilikusanya orodha ya wafuasi wa Navalny kulingana na hifadhidata iliyodukuliwa ya anwani za barua pepe.












