Kwa nini Uturuki iliwazawadia viongozi wa NATO bastola zenye risasi sita?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, aliwashangaza viongozi wa NATO kwa kuwapa kila mmoja bastola iliyokuwa na risasi sita kama zawadi mwishoni mwa mkutano wa muungano huo uliofanyika Ankara.

Kila bastola ilikuwa imechongwa jina la kiongozi aliyepokea zawadi hiyo pamoja na jina la nchi yake. Hata hivyo, baadhi ya viongozi hawakuweza kuondoka nazo kutokana na sheria za nchi zao kuhusu silaha za moto.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, alilazimika kuiacha bastola hiyo mikononi mwa maafisa wa Uingereza nchini Uturuki kwa sababu sheria za Uingereza haziruhusu kuingiza silaha za moto nchini humo.

Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, na Waziri Mkuu wa Uholanzi, Dick Schoof, pia hawakuzichukua zawadi zao.

Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, alipoulizwa alifikiria nini alipoiona zawadi hiyo, alisema kwa utani kuwa hakuwahi hata kuifungua na kusisitiza kuwa hapendi kuwa karibu na silaha.

"Nataka kuwahakikishia Wakanada kwamba silaha iliwekwa mbali nami."

Aliongeza kuwa zawadi hiyo haikuwa kile alichotarajia. "Nadhani, ikilinganishwa na sharubati ya maple niliyokuwa nimetoa kama zawadi… iwe ilikuwa bastola ya kalibu .357 au kitu kama hicho, haikulingana na haikuwa zawadi inayofaa."

Sharubati ya maple, inayotengenezwa kutokana na utomvu wa mti wa maple, ni kitamu cha asili kinachotumika kama kiungo cha kuongeza utamu wa vyakula na vinywaji.

Aliongeza kuwa, "Jambo lingine lililonijia akilini ni kwamba hiki ni kitu ambacho kingefaa kuhifadhiwa katika makumbusho ya vita, au makumbusho ya Jeshi la Canada, au mahali pengine pa aina hiyo, ambako kingekuwa cha kuvutia na pia chenye umuhimu katika kuelezea historia na nafasi ya NATO kwa ujumla."

Baadaye Carney alisema bastola hiyo imekabidhiwa kwa Polisi wa Farasi wa Kifalme wa Canada na imeondolewa uwezo wa kutumika, kwa kuwa haikidhi masharti ya kisheria ya kumilikiwa nchini humo.

Waziri Mkuu wa Canada aliongeza, "Kwa kweli, haikuwa zawadi niliyotarajia."

Viongozi walisemaje kuhusu zawadi ya bastola?

Viongozi wengine pia walishangazwa na zawadi hiyo.

Waziri Mkuu wa Ubelgiji alifahamu kuhusu bastola hiyo baada ya ndege yake kutua Brussels na akaikabidhi mara moja kwa polisi wa uwanja wa ndege.

Pia Ofisi za mawaziri wakuu wa Uholanzi na Uswidi zilisema bastola walizopewa zimehifadhiwa katika balozi za nchi zao mjini Ankara. Bastola ya Uholanzi ilitarajiwa kuondolewa uwezo wa kutumika, huku ile ya Uswidi ikisubiri kukamilishwa kwa taratibu za kuingizwa nchini humo.

Kwa upande wa Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, bastola yake tayari imehifadhiwa katika Palazzo Chigi, makao makuu ya serikali ya Italia, pamoja na zawadi nyingine rasmi za serikali.

Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, alikusudia kuizawadi bastola yake kwa makumbusho ya kijeshi, huku Waziri Mkuu wa Ugiriki akipanga kuiwasilisha katika Makumbusho ya Vita jijini Athens.

Mbali na mijadala ya kisiasa na usalama, mkutano wa NATO mjini Ankara ulivutia pia mjadala kutokana na zawadi hiyo isiyo ya kawaida iliyotolewa kwa viongozi waliohudhuria.

Nia ya Uturuki ilikuwa ipi?

Zawadi hiyo ya bastola iliwekwa ndani ya kisanduku cha mbao chenye mpangilio wa rangi nyeusi. Kisanduku hicho kilikuwa na bendera ya Uturuki, nembo ya NATO na kibao kilichoandikwa kwa Kituruki na Kiingereza: "Gumusay, bastola ya kwanza ya aina ya revolver kutengenezwa nchini mwetu."

Kupitia zawadi hiyo, vyanzo nchini humo vilisema Rais Recep Tayyip Erdogan alinuia kuonesha mafanikio ya sekta ya ulinzi ya Uturuki, ambayo imekuwa moja ya bidhaa muhimu za mauzo ya nje na chombo cha sera ya nje ya nchi hiyo.

Picha zilizochapishwa na baadhi ya viongozi wa dunia zilionyesha kuwa silaha hiyo ilikuwa bastola ya aina ya Gumusay .357 Magnum, bastola ya risasi sita ambayo ilitengenezwa na kampuni ya silaha ya Uturuki MKE katika miaka ya tisini.

Ndani ya kisanduku hicho pia kulikuwa na risasi sita halisi pamoja na hati maalumu iliyoziondoa silaha hizo katika masharti ya kawaida ya udhibiti wa usafirishaji wa silaha nje ya Uturuki.

Kwa mujibu wa Small Arms Survey, taasisi huru ya utafiti yenye makao yake Geneva, Uturuki ilikuwa nchi ya tatu kwa ukubwa duniani katika usafirishaji wa silaha ndogo kati ya mwaka 2019 na 2024, nyuma ya Marekani na Italia. Katika kipindi hicho, thamani ya mauzo ya silaha hizo ilifikia takribani dola za Marekani bilioni 3.

Jukumu la Uturuki katika NATO mpya

Mkutano wa kilele wa NATO, ambao Uturuki inauandaa tena baada ya miaka 22, unafanyika huku kukiwa na vita vinavyoendelea barani Ulaya na Mashariki ya Kati, na kuangazia tena umuhimu wa kimkakati wa Ankara kwa muungano huo.

Uturuki ina jukumu muhimu katika miundombinu ya uendeshaji wa NATO kupitia vituo hivi:

  • Vituo vya anga vya Incirlik, Konya na Erhac,
  • Mitambo ya rada ya Korjik na Kisejik,
  • Kamanda wa Vikosi vya Ardhi vya Washirika wa NATO huko Izmir,
  • Vituo vya pamoja vya operesheni za anga katika miji tofauti,
  • Kituo cha majini cha Aksaray, pamoja na bandari za Taşucu na Iskenderun, ambazo zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kijeshi ikihitajika,

Wakati wa vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran mwaka huu, kuzuiwa kwa makombora yaliyorushwa kutoka Iran kuelekea Uturuki kwa kutumia mifumo ya ulinzi ya NATO kulionyesha umuhimu wa vitendo wa miundombinu hii na nafasi ya Uturuki katika masuala ya usalama wa muungano huo.

Mkutano kati ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Rais wa Marekani Donald Trump, uliopangwa kufanyika Ankara mnamo Julai 7, pia unachukuliwa kuwa mmoja wa mikutano muhimu zaidi ya kidiplomasia katika kuamua mwelekeo wa baadaye wa uhusiano wa Uturuki na Marekani katika enzi hii mpya.

Bado haijafahamika jinsi uhusiano wa Marekani na NATO utakavyochagiza miaka miwili na nusu ya mwisho ya urais wa Donald Trump.

Hata hivyo, baada ya Vita Baridi na enzi za baada ya Vita hivyo, NATO sasa inaingia katika enzi mpya.

Lengo la mtindo mpya ni kupunguza mzigo wa kijeshi na kifedha wa Marekani kwa NATO na kuhamisha uongozi na jukumu la msingi la ulinzi kwa nchi za Ulaya.

Ikiwa mustakabali wa NATO utaundwa kwa kuzingatia mtindo huu, Uturuki ina uwezo wa kuchukua nafasi muhimu sana katika viwango vya kimkakati na kiutendaji, kutokana na umiliki wake wa moja ya majeshi yenye nguvu zaidi katika muungano huo, pamoja na uwezo wa sekta yake ya ulinzi.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid