Vita vya Ukraine: Urusi ina matatizo makubwa- Biden

Iliyochapishwa

Rais wa Marekani Joe Biden amesema uamuzi wa Urusi kujiondoa katika mji wa Kherson wa Ukraine unaonyesha kuwa jeshi lake lina "matatizo ya kweli".

Bw Biden alisema alikuwa akitarajia hatua hiyo kwa "muda" na kwamba itaruhusu pande zote "kurekebisha misimamo yao" wakati wa msimu wa baridi.

Kherson ndio mji mkuu pekee wa Kiukreni kuanguka kwa vikosi vya Urusi.

Lakini mapema Jumatano, kamanda wa Urusi nchini Ukraine alisema haiwezekani tena kuudhibiti  mji huo.

Jenerali Sergei Surovikin, ambaye alipewa uongozi wa amri ya kijeshi wiki chache zilizopita, alitoa tangazo hilo akisindikizwa na maafisa wakuu wa jeshi kwenye runinga ya serikali ya Urusi. Alithibitisha kuwa wanajeshi wa Urusi watajiondoa kabisa kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Dnipro.

Ni pigo kubwa kwa matarajio ya kijeshi ya Urusi wakati inakabiliwa na uvamizi wa Ukraine.

Bw Biden alikuwa akizungumza kutoka Ikulu ya White House baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula ambapo chama chake cha Democratic kilionekana kuwa na uwezekano wa kupoteza udhibiti wa Baraza la Wawakilishi kwa chama cha upinzani cha Republican.

Wapinzani wa rais huyo wa kisiasa hapo awali waliapa kutathmini upya usaidizi wa kijeshi na kibinadamu wa Marekani kwa Ukraine, na Bw Biden aliona kwamba ilikuwa ya "kuvutia" kwamba Moscow "ilisubiri hadi baada ya uchaguzi" kutangaza kujiondoa.

Lakini alisema anatumai "mbinu ya pande mbili za kukabiliana na uchokozi wa Urusi nchini Ukraine" itaendelea.

Uamuzi wa kurudi nyuma katika eneo la Dnipro ulichukuliwa kwa tahadhari na Ukraine.

Rais Volodymyr Zelensky alisema Kyiv ilikuwa ikisonga "kwa uangalifu mkubwa" baada ya tangazo hilo.

"Adui hatupi zawadi, hafanyi 'ishara za nia njema', tunashinda yote," aliwaambia raia wake  katika hotuba yake ya usiku.

Baada ya tangazo la Urusi, raia ndani ya Kherson walisema askari wa Chechen kutoka jeshi la Urusi walikuwa katika jiji, kwenye mikahawa, na wakizunguka barabarani.

Na katika eneo la Kiukreni kwenye eneo la kuzunguka jiji, askari walisema adui anaweza kuwa anajaribu kuwavuta kwenye mtego na walikuwa wakiendelea kwa tahadhari.

Mji unaokaribia kudhibitiwa na utawala mwingine?

Na Paul Adams, mwandishi wa BBC wa masuala ya Kimataifa

Tangu Oktoba, baadhi ya wakazi wa Kherson waaminifu kwa Kyiv wamehisi mabadiliko yakija.

Huku maafisa walioteuliwa na Urusi wakianza kuwahamisha raia, ukombozi wa mji huo ulionekana kukaribia.

Wakati mmoja wa ishara - na labda wa wazi- ulikuja wakati timu ya Urusi iliwasili katika Kanisa Kuu la Karne ya 18 la St Catherine ili kuondoa mifupa ya Prince Grigory Potemkin, mtu aliyehusika na ukoloni kusini mwa Ukraine kwa niaba ya mpenzi wake, Catherine the Great.

Lakini kumekuwa na hisia inayoongezeka ya hofu pia. Ikiwa majeshi ya Urusi yangelazimika kuondoka, wangefanya nini watakapoondoka? 

Uvumi umeenea: kwamba Urusi inapanga kulipua bwawa la karibu la Nova Kakhovka; kwamba askari wa Urusi wamevaa nguo za kiraia na wamejificha katika nyumba za kibinafsi; au kwamba silaha za kivita za Urusi zitajaribu tu kusawazisha jiji kutoka ng'ambo ya Dnipro, baada ya wanajeshi kuondoka.

Chochote kitakachotokea, hii ni  kama wakati muhimu. Mji unaoonekana kama kito katika taji la uvamizi wa Urusi unaweza kuwa karibu kubadilishwa hadi kwa wadhibiti wapya .

Rais Vladimir Putin hakushiriki katika tangazo la kujiondoa.

Lakini washirika wake wawili wakuu - ambao hapo awali walikosoa juhudi za vita za Urusi - walikaribisha hatua hiyo.

Yevgeny Prigozhin, mwanzilishi wa kikundi cha mamluki cha Wagner na mshirika wa muda mrefu wa Putin, alisema kwamba ingawa uamuzi huo haukuwa "hatua ya ushindi" ni muhimu "kutoumia, sio kupata mshangao, lakini kufanya hitimisho na kufanyia kazi makosa.’

Kiongozi wa Chechnya Ramzan Kadyrov - ambaye Bw Putin alimchagua kutawala jamhuri hiyo inayojitawala mwaka 2007 - alisema Jenerali Surovikin alikuwa amechukua hatua  "kama jenerali wa kijeshi, bila kuogopa kukosolewa".

Ingawa kasi ya Ukraine imepungua  katika wiki za hivi karibuni, njia za usambazaji za Urusi katika eneo la Dnipro zilizidi kuwa ngumu baada ya madaraja machache kuvuka kuharibiwa na makombora ya Ukraine.

Kabla ya kujiondoa, Urusi iliwahamisha maelfu ya raia nje ya jiji hilo kwa boti, katika kile Ukraine ilichoeleza kuwa kufukuzwa.

Katika hatua nyingine, waandalizi wa mkutano wa G20 wiki ijayo wa viongozi wa dunia nchini Indonesia wameripotiwa kuthibitisha kuwa rais Putin hatahudhuria hafla hiyo.

Badala yake atawakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Sergei Lavrov, msemaji aliliambia shirika la habari la Reuters.