Diplomasia ya Uchumi: Je, Tanzania inaweza kusonga mbele bila washirika wa jadi?

Chanzo cha picha, URT
- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
"Mie sijali kama ni pesa ya ndani ama ya wahisani, me najali huduma nayopata."
Kauli hiyo ya Nafu Bakari, mkazi wa Mwanza, inaweza kuonekana ya kawaida. Lakini ndani yake kuna swali kubwa linalozungumziwa katika vyumba vya mikutano ya kimataifa, ofisi za serikali na taasisi za maendeleo; je, Tanzania inaweza kuendelea na safari yake ya maendeleo ikiwa washirika wake wa jadi watapunguza misaada na ushirikiano wao?
Kwa miaka mingi, Tanzania imejijengea taswira ya taifa linalofurahia mahusiano mazuri na jumuiya ya kimataifa. Mahusiano hayo yameisaidia kupata misaada, mikopo nafuu, uwekezaji, teknolojia na utaalamu uliosaidia kujenga sekta mbalimbali za maendeleo.
Hata hivyo, matukio ya vurugu za wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 yamezua mjadala mpya kuhusu mustakabali wa baadhi ya mahusiano hayo. Umoja wa Ulaya, mmoja wa washirika wakubwa wa maendeleo wa Tanzania, kupitia Bunge lake ulipendekeza kusitishwa kwa zaidi ya euro milioni 156 za ufadhili wa mwaka 2026 chini ya mpango wa NDICI–Global Europe. Marekani nayo ilitangaza kutathmini baadhi ya maeneo ya ushirikiano wake na Tanzania.
Ni mjadala uliokuja wakati serikali ikisisitiza kuwa Tanzania ya leo si Tanzania ya miaka ya nyuma.
"Mwaka huu (2025/26) bajeti yetu ni trilioni 56. Kati ya hizo trilioni 40 zinatokana na makusanyo yetu wenyewe. Misaada katika bajeti ni trilioni 1.07 tu," alisema msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa.
Kwa mujibu wa Msigwa, takwimu hizo zinaonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kujitegemea kifedha.
"Ukiangalia hizi takwimu unaona hatuwezi kushindwa. Kama trilioni 55 ni za kwetu, tutakwama wapi?" alihoji.
Lakini je, uwezo wa kuendesha bajeti bila misaada unatosha kuifanya Tanzania isitetereke endapo ushirikiano wa muda mrefu na baadhi ya washirika wa jadi utapungua?
Diplomasia ya uchumi imesaidiaje kujenga Tanzania?

Chanzo cha picha, Jamhuri
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa zaidi ya miongo sita, diplomasia ya maendeleo imekuwa sehemu muhimu ya safari ya Tanzania, kwa sera ya sasa itambue kama diplosasia ya uchumi. Kupitia mahusiano yake na Umoja wa Ulaya (UN), Marekani, Benki ya Dunia, Shirika la fedha la kimataifa (IMF), Benki ya Maendeleo ya Afrika na mashirika ya Umoja wa Mataifa, Tanzania imefanikiwa kuvutia mabilioni ya dola za misaada, mikopo nafuu na uwekezaji uliosaidia kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo.
Kwa mujibu wa TICGL Economic Research, kati ya mwaka 2010 na 2023 Tanzania ilipokea zaidi ya dola za Marekani bilioni 37 za Misaada Rasmi ya Maendeleo (ODA), wastani wa dola bilioni 2.7 kila mwaka. Mwaka 2023 pekee, misaada hiyo ilifikia dola bilioni 3.06, sawa na karibu asilimia 23 ya mapato ya serikali.
Fedha hizo zimeonekana katika maisha ya kila siku ya wananchi.
Mwanza ni mfano mmoja. Zaidi ya euro milioni 45 kutoka Umoja wa Ulaya zimeelekezwa katika miradi ya maji safi na mazingira inayolenga kuboresha maisha ya wakazi wa jiji hilo na kulinda mazingira ya Ziwa Victoria.
Kwa Nafu Bakari, matokeo ya ushirikiano huo yanaonekana wazi.
"Tulikuwa tunahangaika sana kupata maji safi, lakini mara nyingi yalikuwa hayapatikani au yalikuwa na changamoto za ubora. Sasa huduma imeboreshwa na maisha yamekuwa rahisi zaidi. Mie sijali kama ni pesa ya ndani ama ya wahisani, me najali huduma nayopata," anasema
Katika sekta ya afya, Marekani imeendelea kuwa mmoja wa washirika wakubwa zaidi wa Tanzania kwa zaidi ya miongo miwili, ikichangia mabilioni ya dola katika mapambano dhidi ya UKIMWI, kifua kikuu na malaria.
Katika sekta ya miundombinu, washirika wa maendeleo wamechangia maboresho ya viwanja vya ndege, barabara, huduma za maji na nishati.
Kwa mantiki hiyo, diplomasia ya uchumi imekuwa zaidi ya mahusiano ya kisiasa; imekuwa chombo cha kuleta huduma, fursa na maendeleo kwa wananchi.
"Ni kweli tunahitaji misaada, ni muhimu. Lakini si kwamba bila wao nchi hii hawezi kusonga," anasema Msigwa.
Tanzania ina nini cha kuziba pengo?

Chanzo cha picha, Getty Images
Swali la msingi kwa sasa si kama misaada inaweza kupungua. Swali ni kama Tanzania ina vyanzo mbadala vya kuendeleza kasi ya maendeleo, bila kutetereka.
Kwa miaka ya karibuni, Tanzania imeongeza makusanyo ya ndani kupitia mifumo ya kidijitali, matumizi ya mashine za EFD, malipo ya kielektroniki na juhudi za kuingiza biashara nyingi zaidi katika mfumo rasmi wa uchumi.
Kwa mujibu wa takwimu za serikali, makusanyo ya mapato ya ndani yaliongezeka kutoka shilingi trilioni 20.59 mwaka 2020/21 hadi shilingi trilioni 28.83 mwaka 2023/24. Aidha, makusanyo ya kila mwezi yaliongezeka kutoka shilingi trilioni 1.51 Novemba 2020 hadi shilingi trilioni 3.09 Machi 2025.
Zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya taifa sasa inatokana na vyanzo vya ndani, hatua ambayo serikali imekuwa ikiitaja kama ishara ya kuimarika kwa uwezo wa kujitegemea.
Mbali na kodi, Tanzania ina rasilimali nyingine nyingi zinazoweza kuongeza mapato ya taifa. Madini, gesi asilia, utalii, kilimo, uchukuzi wa kikanda, uchumi wa buluu na biashara kupitia bandari za Bahari ya Hindi ni miongoni mwa sekta zinazotajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuongeza mapato ya ndani.
Raphael Anthony, mtaalamu wa fedha, anaamini kuwa suluhisho la muda mrefu si kuongeza utegemezi wa misaada, bali kuongeza uwezo wa uchumi kuzalisha mapato yake yenyewe.
"Tanzania ina rasilimali nyingi. Kinachohitajika ni kuzibadilisha rasilimali hizo kuwa ajira, uzalishaji, kodi na mapato ya taifa. Hapo ndipo pengo la misaada linaweza kuzibwa kwa mafanikio," anasema.
Diplomasia ya uchumi inaweza kuziba Pengo?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pengine sehemu muhimu zaidi ya mjadala huu haipo kwenye misaada, bali kwenye diplomasia ya uchumi. Kwa uelewa, dhana ya diplomasia ya uchumi inaweza kuwa mahusiano ya mataifa mawili, kundi, kampuni ama watu wa mataifa mawili unaojikita katika mambo ya kiuchumi.
Katika miaka ya karibuni, Tanzania imekuwa ikitumia sera yake hii ya nje kuvutia uwekezaji, kupanua masoko ya biashara na kuitangaza nchi kimataifa.
Tangu aingie madarakani mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan ameifanya diplomasia ya uchumi kuwa moja ya nguzo muhimu za sera ya nje ya Tanzania.
Ziara zake katika mataifa mbalimbali duniani, mikutano ya kimataifa ya uwekezaji na juhudi za kuimarisha mahusiano ya kiuchumi zimekuwa sehemu ya mkakati wa kuvutia mitaji na teknolojia.
Filamu ya Royal Tour nayo ilitumika kama nyenzo ya kuitangaza Tanzania duniani, hasa katika sekta ya utalii, ambayo imeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato ya fedha za kigeni.
Katika kipindi hicho, Tanzania imeendelea kushuhudia ongezeko la uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati, madini, viwanda, huduma za usafirishaji na miundombinu.
Kwa mfano, mapato ya serikali kutoka sekta ya madini yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 624.61 mwaka 2021 hadi shilingi bilioni 788.82 mwaka 2025.
Katika utalii, mapato yaliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 700 mwaka 2020 hadi dola bilioni 3.9 mwaka 2024. Utalii wa ndani nao uliongezeka kutoka shilingi bilioni 46.3 mwaka 2021 hadi shilingi bilioni 209.8 mwaka 2024.
Miradi mikubwa kama reli ya kisasa ya SGR, maboresho ya bandari, uwekezaji katika nishati pamoja na maandalizi ya AFCON 2027 imeongeza matarajio ya ukuaji wa uchumi na kuvutia ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje.
Kwa mujibu wa wataalamu wa hesabu na uchumi, tofauti kubwa kati ya misaada na uwekezaji ni kwamba uwekezaji huongeza uzalishaji, huunda ajira na huongeza mapato ya muda mrefu.
"Misaada inaweza kupungua, lakini uwekezaji ukiongezeka unaweza kuziba sehemu ya pengo hilo. Uwekezaji hujenga uchumi unaozalisha badala ya kutegemea fedha za nje kwa muda mrefu," anasema Anthony.
Kwa mtazamo huo, diplomasia ya uchumi inaweza kuwa moja ya silaha muhimu zaidi ya Tanzania katika safari ya kupunguza utegemezi wa misaada.
Diplomasia, uwekezaji na somo la mataifa yaliyojitegemea

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Historia ya dunia inaonyesha kuwa kujitegemea hakumaanishi kujitenga. Botswana ilitumia mapato ya madini kujenga taasisi imara na kuongeza uwezo wa kugharamia maendeleo yake. Miongoni mwa mataifa yanayotajwa mara nyingi katika mjadala wa kujitegemea ni Rwanda.
Kwa mujibu wa mchumi mwandamizi wa International Growth Centre (IGC) Rwanda, Mphatso Kumwenda, mageuzi ya mifumo ya kodi yalikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya nchi hiyo.
"Rwanda iliwekeza katika matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti, mifumo ya ulipaji kodi kwa njia ya mtandao na huduma za kidijitali zilizorahisisha ulipaji na ukusanyaji wa kodi. Matokeo yake, mapato ya kodi yaliongezeka kutoka chini ya asilimia 10 ya Pato la Taifa mwanzoni mwa miaka ya 2000 hadi asilimia 17 mwaka 2018," anasema.
Anaongeza kuwa mafanikio hayo hayakutokana na kuongeza viwango vya kodi pekee, bali kujenga mfumo unaorahisisha ulipaji kodi na kuongeza uaminifu wa walipakodi.
Vietnam nayo ilitumia biashara, viwanda na uwekezaji wa nje kuondoka katika utegemezi mkubwa wa misaada na kujenga uchumi unaoongozwa na uzalishaji.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mifano hiyo inaonyesha kuwa mataifa yaliyofanikiwa kupunguza utegemezi wa misaada hayakukatiza mahusiano yao ya kimataifa. Badala yake, yalitumia diplomasia kuvutia biashara, teknolojia na uwekezaji zaidi.
Kwa Tanzania, mjadala wa sasa unaweza kuwa mtihani muhimu wa uwezo wake wa kutumia diplomasia kama nyenzo ya maendeleo. Wakati misaada ikibaki kuwa sehemu ya ushirikiano wa kimataifa, serikali inaonekana kuweka mkazo zaidi katika kuvutia uwekezaji, kupanua biashara na kuongeza thamani ya rasilimali zake.
Wachambuzi wanaamini kuwa mafanikio ya mkakati huo yatategemea uwezo wa nchi kuendelea kujenga imani kwa wawekezaji, kuimarisha mazingira ya uwekezaji, taasisi zake na kuongeza ushindani wa uchumi wake katika soko la dunia.
Kuhusu mazingira ya uwekezaji nchini, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema yameendelea kuboreshwa kupitia maboresho ya sheria, miundombinu na sera ya diplomasia ya uchumi, hatua inayolenga kuongeza imani ya wawekezaji, biashara na utalii nchini.
Je, diplomasia ya uchumi inaweza kuibadilisha Tanzania kutoka taifa linalopokea misaada kwenda taifa linalovutia zaidi uwekezaji, biashara na mitaji ya kimataifa? Jibu la swali hilo linaweza kuamua sura ya maendeleo ya Tanzania katika miongo ijayo.















