Mauaji ya mateka wa shule mwaka 2004 ambayo yalifichua udhaifu wa Putin

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Sarah Rainsford
- Nafasi, BBC
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Siku ambayo mji wa Beslan ulianza kuzika wapendwa wake, kulikuwa na magari mengi yakiwa yamepakia majeneza kuelekea makaburini. Katika mji mdogo wa Caucasus, kila mtu alikuwa amepoteza jamaa au alijua mtu aliyeuawa katika shambulio la School No.1.
Shambulio hilo lilifanywa na wapiganaji wenye silaha nzito, hasa kutoka Chechnya, na lilidumu kwa siku tatu. Watu mia tatu na thelathini na wanne walikufa; 186 kati yao walikuwa watoto.
Ni miaka 20 leo tangu School No. 1 kuzingirwa na kutokea milipuko yenye uharibifu, lakini huzuni bado imetanda kwa watu wa Beslan.
Alina mwenye umri wa miaka 11, amezikwa kwenye ua mbele ya nyumba yao, huku wanasesere wake wakiwekwa kando yake.
Tukio lenyewe

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 2004, mkasa wa Beslan ulisababishwa na makumi ya wanaume na wanawake waliovamia shule hiyo, wakifyatua risasi hewani na kuwachukua mateka mamia ya watu.
Waliwakusanya akina mama walio na watoto na puto, na wasichana wadogo waliokuwa na vibanio vya nywele kichwani. Familia zilikuwa zikisherehekea siku ya kwanza kurudi shuleni. Wanamgambo hao walijaza vilipuzi kwenye jumba la mazoezi na kuanza kuwauwa mateka wa kiume.
Wakati wa majira ya joto, vita vya kikatili vya Vladimir Putin dhidi ya wanaotaka kujitenga huko Chechnya - vilivyoanza miaka minne mapema - tayari vilikuwa vimevuka mipaka ya jamhuri ya kusini mwa Urusi.
Siku moja kabla ya kuzingirwa kwa Beslan, watu 10 waliuawa pale mwanamke wa Chechnya alipojilipua nje ya kituo cha treni ya chini ya ardhi huko Moscow.
Kabla ya hapo, washambuliaji wa kujitoa mhanga walilipua ndege mbili kutoka angani na kulikuwa na shambulio baya kwenye tamasha la muziki.
Putin na shambulio hilo

Chanzo cha picha, Getty Images
Ilichukua miaka 20 kwa Putin kutembelea magofu ya School No. 1. Hata hivyo, hakujiunga na hafla za ukumbusho na familia. Alisafiri kwenda huko wiki mbili zilizopita, akiwa peke yake.
Kuta chache za shule zilizovunjwa ziliachwa zimesimama kama ukumbusho, na hufunikwa kwa sanda yenye rangi ya dhahabu na kuning'inizwa picha za waliouwawa.
Katikati ya ukumbi wa mazoezi ambapo mateka hao walishikiliwa, Putin aliweka maua chini ya msalaba wa mbao.
Lilikuwa shambulio baya zaidi la kigaidi kuwahi kutokea nchini Urusi. Mara tu baada ya mzingiro kuisha, aliruka kwa ndege usiku sana kutembelea hospitali. Aliwaambia watu wa Beslan kwamba Urusi yote inaomboleza pamoja nao lakini jua lilipochomoza alikuwa tayari ameondoka.
Nambari na uwongo

Chanzo cha picha, Getty Images
Wiki mbili zilizopita, mama watatu kutoka Beslan, walipelekwa kukutana na Putin.
"Ni kitendo cha kutisha ambacho kiligharimu maisha ya watu 334," Putin alieleza kuhusu mkasa huo, mbele ya kamera ya runinga ya serikali.
"Kati ya idadi hiyo, 136 walikuwa watoto."
Lakini watoto waliouwawa hasa ni 186 huko Beslan. Ni nambari iliyoandikwa kwenye akili ya kila mtu katika mji huo. Ni jambo moja wasilosahau.
Miongo miwili iliyopita, aliwaambia Warusi, kuwa amepigana na kushinda vita dhidi ya ugaidi. Na sasa anawaambia kuwa anapigana na "Wanazi mamboleo" na “maadui Magharibi” huko Ukraine, na ameapa atashinda vita hivyo pia.
Mafunzo kwa Putin

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza nini kingetokea kwa serikali ya kidemokrasia ya Magharibi baada ya shambulio ambalo lilimalizika kwa mateka wengi kuuawa, kuliko magaidi.
Nadhani itakuwa vigumu kustahimili uchunguzi rasmi usioepukika, au uchaguzi ujao. Lakini Vladimir Putin hakuwa na wasiwasi kuhusu hilo.
Mwaka 2017, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilisema, Urusi ilishindwa katika jukumu lake la kuwalinda mateka na ilitumia nguvu kupita kiasi. Kesi hiyo ililetwa na akina mama waliokata tamaa, waliofiwa, wakitafuta haki.
Lakini hakukuwa na uchunguzi mpya nchini Urusi. Hakuna maafisa wakuu waliowajibika.
Wakati akina mama watatu wa Beslan walipolalamika kwa Putin kuhusu hilo mwezi Agosti, katika mkutano wao, alionekana kushangaa na akaahidi kuliangalia.
Mwaka 2004, Putin alitangaza kufuta uchaguzi wa moja kwa moja wa magavana katika mikoa ya Urusi, akidai hilo lingesaidia kuimarisha usalama. Hakukuwa na uhusiano wowote na shambulio la Beslan.
Wakati bunge lilipokusanyika kupiga kura juu ya hatua hiyo, wanasiasa wa upinzani walikaa nje ya jengo hilo wakionya juu ya udikteta unaoenea.
Miongo miwili baadaye, hakuna upinzani tena. Vyombo vya habari vya serikali vimedhibitiwa kikamilifu. Demokrasia imekandamizwa.
Somo kuu ambalo Putin alichukua kutokana na kuzingirwa kwa Beslan, lilikuwa ni kuhusu kuongeza udhibiti.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












