Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini Ukraine imewaondoa wanajeshi wake katika taifa hili barani Afrika?
Takriban wanajeshi 250 wa Ukraine waliokuwa sehemu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamerejea nchini mwao kusaidia katika vita dhidi ya jeshi la Urusi.
Ilipotangazwa mwezi Machi kuwa Jeshi la Wanahewa la Ukraine linaondoka nchini humo, wanadiplomasia walionya kwamba vikosi vya kulinda amani vinavyofanya kazi nchini DRC vinaweza kukabiliwa na uhaba wa ndege za kivita.
Vikosi vya Ukraine ambavyo sasa vimeondoka nchini humo vilikuwa na jukumu muhimu katika vita dhidi ya waasi hao walioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ndege nane za kivita za Ukraine zilikuwa sehemu ya theluthi moja ya ndege za kivita za ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.
Tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwezi Februari, Ukraine imeondoa wanajeshi wake kutoka kwa ujumbe mwingine wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani uliotumwa huko.
Jacques Ndjoli, mjumbe wa kamati ya ulinzi ya bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, aliambia BBC kwamba kujiondoa kwawanajeshi wa Ukraine ni suala zito.
Aidha amesema vikosi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vina jukumu la kuleta amani nchini humo.
Wakati wanajeshi wa Ukraine walipoondoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kamanda wa vikosi vya Brazil katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa, Jenerali Marcos da Costa, alisema "tunashukuru sana kwa hatua yao katika miaka 10 iliyopita".
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Monusco, unakabiliwa na shinikizo kutoka ndani ya nchi hiyo.
Umekosolewa vikali kwa kuchelewa kukabiliana na ukosefu wa usalama mashariki mwa DRC ambako makundi yenye silaha yamekuwa yakisababisha ubakaji, mauaji na uporaji wa rasilimali kama vile madini ya dhahabu na almasi katika eneo hilo.
Mwezi Julai, watu 36, wakiwemo walinda amani wanne wa Umoja wa Mataifa, walikufa baada ya makundi ya watu kushambulia majengo ya Umoja wa Mataifa katika miji ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Baada ya miaka 22 ya vikosi hivyo nchini DRC, inatarajiwa kupungua kwa operesheni hiyo lakini haijaelezwa ni lini operesheni ya kulinda amani itakamilika.
Kwa sasa Monusco ina takriban wanajeshi 18,000 nchini humo, wakiwemo zaidi ya wanajeshi 12,000 kutoka Pakistan, India na Bangladesh. Inachukuliwa kuwa Umoja wa Mataifa utapunguza idadi ya vikosi hivi ingawa tarehe haijabainishwa.
MONUSCO ilichukua nafasi ya Ujumbe wa awali wa Umoja wa Mataifa ulioiongoza nchi mwaka 2010.
Mapigano yameongezeka huko yakihusisha makundi kadhaa yenye silaha ikiwa ni pamoja na vuguvugu la M23 na Democratic Forces.
Ni mojawapo ya misheni kubwa na ya gharama kubwa zaidi kati ya misheni 12 za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.