Alaa Abdel Fattah, ‘mfungwa mashuhuri’ wa Misri ni nani?

Chanzo cha picha, AFP
Kesi ya mwanaharakati wa kisiasa wa Misri aliyefungwa,Alaa Abdel Fattah imevuta hisia za wengi ulimwenguni katika mkutano kuhusu hali ya hewa (COP27) unaoendelea katika mji wa Sharm El-Sheikh nchini Misri.
Familia ya Abdel Fattah, ambaye pia ana uraia wa Uingereza, imezitaka mamlaka za Misri kutoa ushahidi kuwa mwanaharakati huyo wa haki za binadamu kama bado yupo hai, kwani hawakuweza kuwasiliana naye tangu alipoongeza mgomo wake wa kula kwa miezi saba kwa kuacha kunywa maji Jumapili iliyopita, wakati mkutano wa kilele wa hali ya hewa ulipokuwa unaanza.
Haya yanajiri huku kukiwa na uvumi kwamba wakuu wa magereza wanamlazimisha kula kwa nguvu. Shinikizo la kimataifa kwa Misri kumwachilia Abdel Fattah limekuwa likiongezeka, hasa baada ya kuwasili kwa dada mdogo wa Abdel Fattah, Sana Seif, katika ukumbi wa mkutano na kutangaza kesi yake.
Miongoni mwa viongozi wa kimataifa ambao wametaka kuachiliwa kwake ni Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk.
Lakini Alaa Abdel Fattah ni nani hasa, ambaye hivi karibuni alikua mwanasiasa mashuhuri wa Misri
Familia ya wanaharakati

Chanzo cha picha, Getty Images
Alaa Abdel Fattah anachukuliwa kuwa mmoja wa wanablogu na wanaharakati mashuhuri wa Misri katika kipindi cha baada ya mwaka 2005. Kama mtaalamu katika masuala ya habari, amesaidia kukuza na kusimamia mifumo mingi ya kidijitali inayotaka uhuru wa kujieleza na uwazi katika maisha ya umma na kutoa hifadhi ya bila malipo - pamoja na ushauri - kwa wanablogu.
Alaa Abdel Fattah alizaliwa Novemba 1981 katika familia ya wanasheria. Baba yake ni mwanasheria maarufu wa mrengo wa kushoto na mwanaharakati Ahmed Seif al-Islam Abdel Fattah Hamad, ambaye alikamatwa zaidi ya mara moja wakati wa enzi za Marais wa zamani wa Misri Anwar Sadat na Hosni Mubarak.
Mama yake, Laila Souif, ni profesa wa Hisabati katika Chuo Kikuu cha Cairo na mwanaharakati wa kisiasa katika sekta ya mashirika ya kiraia. Alaa Abdel-Fattah ana dada wawili, Mona na Sana Seif, wote wanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu, na miongoni mwa wafuasi wakubwa wa kaka yao. Wanahamasisha juhudi za kufahamisha jumuiya ya kimataifa kuhusu kesi yake.
Sana amefungwa mara mbili: kwanza mnamo 2014 - aliachiliwa kupitia msamaha wa rais - na akafungwa tena mnamo 2020 kwa mwaka mmoja na nusu kwa tuhuma za "kueneza habari za uwongo".
Ni alama ya demokrasia na mageuzi

Alaa Abdel Fattah alikamatwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2006 na akiwa na watu waliokuwa wakishiriki maandamano ya kutaka uhuru wa mahakama - aliachiliwa baada ya siku 45.
Wakati huo, tovuti iliyokuwa ikitoa wito wa kuachiliwa kwake ilizinduliwa, ambayo baadaye ikawa na hashtag #FreeAlaa kwenye Twitter. Uzoefu wa kwanza wa kukamatwa kwa Abdel Fattah haukumkatisha tamaa kuendelea na shughuli zake.
Mnamo 2011, alikua mmoja wa watu mashuhuri wa vuguvugu la demokrasia, akitengeneza majukwaa ya mtandaoni ambayo yaliwezesha raia wa Misri kushiriki katika utayarishaji wa katiba. Ujumbe mwingi kupitia twitter pia zilifungua milango ya mijadala mingi kuhusu masuala kama vile dini na mageuzi ya kisiasa.
'Alaa aliteswa' na Yolande Knell

Chanzo cha picha, Getty Images
Abdel Fattah alionekana mwiba katika mapinduzi ya Januari 25. Ingawa hakuwa nchini Misri wakati wa maandamano hayo yakianza, alishiriki katika maandamano yaliyofuata yaliyopelekea kupinduliwa kwa Rais wa zamani Hosni Mubarak.
Kisha alisaidia kuandaa maandamano ya upinzani wakati wa utawala wa Baraza la Kijeshi la Wanajeshi, na alifungwa gerezani kwa kile kilichojulikana kama matukio ya Maspero mwishoni mwa Oktoba 2011 kutokana na kuhabarisha kuhusu mapigano kati ya waandamanaji wa Kikristo na vikosi vya usalama.
Mwendesha mashtaka wa kijeshi alimshutumu kwa uchochezi dhidi ya jeshi na kuvuruga amani na usalama wa umma. Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu alidai kuachiliwa kwake, na akaachiliwa mnamo Desemba mwaka huo huo.
Baada ya mageuzi

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Abdel-Fattah alikamatwa tena Novemba 2013, pamoja na watu wengine, aliposhiriki maandamano mbele ya bunge kupinga sheria ya maandamano na rasimu ya katiba ambayo ingepigiwa kura mapema 2014.
Alaa alishtakiwa na mamlaka ya usalama kwa "kuandamana bila kibali" na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela. Mahakama ya Misri iliidhinisha uamuzi huo mwaka 2017.
Wakati huu akiwa gerezani - kwa muda wake mrefu zaidi - baba yake Abdel Fattah alikufa na viongozi walimruhusu kuhudhuria mazishi yake.
Aliachiliwa Machi 2019 akiwa amemaliza kifungo chake, lakini alikamatwa tena Septemba mwaka huo huo na mnamo Desemba 2021 alifungwa kwa miaka mitano kwa "kueneza habari za uwongo".
Abdel-Fattah aliongeza mgomo wake wa kutokula Novemba 6, sambamba na kuanza kwa Mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa huko Sharm El-Sheikh, ambapo pia aliacha kunywa maji.
Afisa wa ngazi ya juu wa Marekani ameelezea wasiwasi wa Ikulu ya White House kuhusu "ripoti kuhusu hali ya afya ya Alaa Abdel Fattah", na kuongeza kuwa utawala wa Rais Joe Biden mara kwa mara umeibua "wasiwasi na serikali ya Misri kuhusu kesi ya mwanaharakati huyo na mazingira huko jela".













