COP27: Mradi wa mafuta unaoitwa dhambi

Wanasiasa wanapokutana kujadili jinsi ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, vizazi vya wakazi wa kwanza wa Kusini mwa Afrika wanaibua wasiwasi kuhusu mradi wa utafiti wa mafuta na gesi.
Viongozi wa kidini pia wamezungumza, huku mmoja akisema mradi huo ni dhambi, na kutoa wito kwa wajumbe wa COP27 kudhibiti shughuli za makampuni ya mafuta.
Katika nchi za Kusini mwa Afrika Botswana ni mojawapo ya delta kubwa zaidi za bara duniani, mandhari ambayo Umoja wa Mataifa umeitaja kuwa "ya kipekee" na "nadra" kwa uzuri wake.
Okavango Delta ni chemichemi inayopatikana katikati ya Jangwa la Kalahari. Eneo hilo ni makazi ya baadhi ya wanyama walio hatarini kutoweka duniani, kama vile faru weusi, ndege, samaki, na wanyama wanaoishi hapa wanafanya mfumo asilia wa eneo hili kuwa dhaifu.
Ni eneo lenye thamani sana ndiposa imeteuliwa kuwa Urithi wa Dunia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini kuna hofu kwamba eneo hili linakabiliwa na tishio la kuharibiwa, kwa sababu lina kadiriwa kuwa nishati ya mafuta.
Kampuni ya Reconnaissance Energy Africa (ReconAfrica), kutoka Canada, inaamini kunaweza kuwa na utajiri wa mafuta na gesi chini ya ardhi kaskazini mwa Botswana na nchi jirani ya Namibia.
Ina leseni za uchunguzi wa eneo la kilomita za mraba 34,325 linalozunguka mpaka wa nchi hizo mbili. Visima vitatu vya majaribio tayari vimechimbwa nchini Namibia.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Mradi huo ni dhambi, na ni mbaya," Askofu wa zamani wa Kanis ala Kianglikana aliyestaafu hivi karibuni wa Namibia ananiambia.
Luke Pato alitumia miezi ya mwisho ya muda wake nchini Namibia kufanya kampeni dhidi ya mradi huo na kundi la viongozi wengine wa kidini.
Tunapoketi kwenye bustani ya nyumba yake huko Johannesburg, ananiambia kwa nini.
"Yesu alisema, 'Nimekuja ili wawe na uzima kisha wawe nao tele.' Asingewahi kuwa upande wa kitu chochote chenye uwezo wa kuharibu maisha, kuharibu mazingira ambayo watu wanaishi. Sina shaka kwamba Yesu angepata njia ya kuvuta zulia chini ya miguu ya wale ambao bado wanataka kushiriki katika utafutaji wa nishati ya mafuta."Ningependa kuchimba visima kusitisha, kampuni hii ichukue mashine zake na kuondoka."
Askofu Pato ana wasiwasi kuhusu athari ambayo uchimbaji wa visima nchini Namibia unaweza kuwa nayo kwenye mabwawa ya maji yaliyo chini ya ardhi ambayo yanaunganishwa na Mto Okavango.
Mto huo unapita kando ya mpaka wa Namibia kaskazini mwa maeneo ya kuchimba visima, ukipeleka maji kwenye delta katika nchi jirani ya Botswana.
ReconaAfrica inasema uchunguzi wake hauna madhara kwa mazingira.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanyengwa Shapwanale, mkuu wa mawasiliano wa kampuni tanzu ya ReconAfrica ya Namibia anasema kampuni hiyo inafanya kazi na serikali ya Namibia "kuhakikisha kwamba sio tu tunaendana na kile kinachotarajiwa kutoka kwetu kulinda mazingira, haswa maji, lakini pia kuhakikisha kuwa tunakwenda hatua ya ziada."
Lakini Askofu Pato pia ana wasiwasi mwingine: anafikiri uchunguzi wa maliasili za Kiafrika na kampuni inayomilikiwa na Canada ni sawa na "wimbi jipya la ukoloni."
Anataka wajumbe wa COP27 nchini Misri kuweka mbele "azimio ambalo lingeambia makampuni kwamba wanachimba visima nje ya nchi zao wasifanye hivyo."
Serikali ya Namibia ilikataa ukosoaji wake, ikiambia BBC kuwa ina jukumu la kuendeleza maliasili ya nchi hiyo kwa manufaa ya watu wake.
"Kupuuza jukumu hilo itakuwa ni kutojali, kwa hiyo kama nchi huru ya kidemokrasia, Namibia itachunguza na kuendeleza maliasili yake kwa uendelevu," ilisema.
Ilisema kwamba uzalishaji wa gesi chafuzi nchini Namibia "haukuwa na maana ikilinganishwa na ule wa mataifa yaliyoendelea".
Afrika kwa ujumla inawajibika kwa chini ya 4% ya uzalishaji wa hewa chafu duniani.

Suala la iwapo nchi za Afrika zinapaswa kuendelea kutumia nishati ya mafuta linaibuka kama hatua ya mgawanyiko katika COP ya mwaka huu.
Idadi kubwa inasema wanapaswa kuwa huru kutumia amana za mafuta na gesi, ili kukuza uchumi wao na kumaliza umaskini wa nishati. Lakini Askofu Pato bado hajashawishika.
"Wakati kuna uwezekano wa vyanzo safi vya nishati, kwa nini uchukue hatua ya kurudi kwenye nishati ya kisukuku?" anauliza.
Nchini Botswana wasiwasi huo unaungwa mkono na vizazi vya wakazi wa kwanza wa Kusini mwa Afrika: Wasan.
Kwa maelfu ya miaka jimii ya Wasan iliishi eneo ambalo sasa ni Kusini mwa Afrika, wakiishi maisha ya uwindaji.
Sasa watu wa jamii hiyo waliosalia wanadhaniwa kuwa karibu 90,000 wanaopatikana Botswana, Namibia, Afrika Kusini na Zambia.
Msingi wa mifumo ya tamaduni na imani zao ni kuishi kwa amani na asili. Msimamo wa kiroho wa Wasan inahusishwa kwa kiasi kikubwa na uhusiano wao na ardhi, mimea na wanyama.
"Hatutaki mradi huu ufanyike," anasema Diphetogo Anita Lekgowa, mwanaharakati wa Jamii ya San kutoka Botswana ambaye anahudhuria COP27 nchini Misri kama mwanaharakati wa haki za watu wa kiasili.
"Tunajali mazingira na ulinzi wa maliasili zetu, kwa sababu mara [uchimbaji visima unapoanza] kutakuwa na mabadiliko mengi.
Wanyama watahama, na tunahofia kupoteza mimea yetu ya kiasili." Serikali ya Botswana ilikataa maombi kadhaa ya mahojiano, lakini Waziri wa Rasilimali Madini, Lefoko Moagi, amewahi kusema kwamba "masharti ya leseni yanahitaji ReconAfrica kuhifadhi mazingira asilia kadiri inavyowezekana [na] kupunguza ... uharibifu wa asili na rasilimali za kibiolojia."

Chanzo cha picha, DIPHETOGO ANITA LEKGOWA
Serikali pia imesisitiza kwamba hakuna uchimbaji unaopangwa kwa sasa nchini Botswana - uchunguzi utafanywa kwa njia zisizo za uvamizi.
Lakini Anita anahofia kwamba iwapo uwepo wa mafuta au gesi utathibitishwa, hatimaye uchimbaji wa visima utaongezeka sana.
Askofu Pato ana wasiwasi kuhusu nini kinaweza kutokea. Yeye ni kutoka kwa watu wa Mto San, ambao wanaamini walipewa mto Okavango na miungu, kwa sababu haukauki kamwe.
Alipokuwa akikulia katika kijiji cha Khwai kwenye ukingo wa delta, heshima waliyokuwa nayo wazee wake kwa mto huo ilifumwa katika maisha yao, anasema.
"Wazazi wetu wangeenda kwenye mto ili kucheza, wakiungana na miungu, wakishukuru miungu. Utamaduni wetu, namna yetu ya maisha, roho yetu inaunganishwa na mto huu." Ikiwa mto huu na mandhari yake yatadhuriwa, Anita anasema, "itawaangamiza watu kihisia".
"Kwa nini serikali yetu inavutiwa na mafuta wakati kuna mambo mengine yanaweza kufanywa ambayo yanaweza kuleta mapato?"














