Banderol: Lifahamu kombora jipya la Urusi lenye muundo wa droni

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Inaonekana Urusi imeanza kutumia kombora jipya linaloitwa Banderol kuishambulia Ukraine. Wataalamu wanasema ni "mseto wa ndege isiyo na rubani, bomu, na kombora."

Matumizi ya silaha hii mpya ya Urusi yaliripotiwa kwa mara ya kwanza mwezi Aprili na mtaalamu wa Ukraine, wa mifumo ya vita vya kielektroniki na mawasiliano, Serhiy Beskrestnov.

Kulingana naye, droni hizi ambazo zinaitwa "Banderol" zimekuwa zikishambulia eneo la Odessa kwa wiki kadhaa mfululizo.

Zina injini ya ndege na hufikia kasi ya takriban kilomita 400-500 kwa saa.

Mtaalamu anaelezea zinaweza kukaa hewani kwa muda mrefu, kuchunguza shabaha, badala ya kushambulia moja kwa moja kama vile Shahed.

Mapema mwezi Mei, Beskrestnov aliripoti kuhusu "Banderola" na akaiita droni ya masafa marefu, yenye kasi, na kichwa cha kombora cha takriban kilo 100.

Kulingana naye, ndege hii isiyo na rubani iliweza kuruka kilomita 200 ndani kabisa ya eneo la Ukraine.

Tunachokijua kuhusu Banderol

Mchambuzi mwingine wa Ukraine, wa masuala ya kijeshi, Oleksandr Kovalenko, baadaye alitoa taarifa zaidi kuhusu Banderol.

Aprili, droni nne ziligunduliwa katika anga juu ya Bahari Nyeusi, zikitembea kwa kasi ya wastani ya kilomita 500 kwa saa. Zilirushwa kutoka sehemu ya magharibi ya Crimea inayokaliwa na Urusi na kusafiri sehemu usawa wa takriban mita 500 kwenda juu.

Droni ziliruka masafa ya kilomita 140-150. Kulingana na Kovalenko, njia ya droni hiyo imenyooka, bila kwenda kulia na kushoto.

Hata hivyo, hali hii ilibadilika mapema Mei. Ilirekodiwa kwamba "Banderol" ina uwezo wa kuzunguka na inaweza kufikia kasi ya hadi kilomita 750-800 kwa saa.

Kovalenko aliripoti kwamba Mei 3, ndege isiyo na rubani iliruka kwa urefu wa mita 500, lakini ilipovuka ufuo, ilishuka chini hadi mita 100 ili isionekane na ulinzi wa anga.

Kurugenzi Kuu ya Ujasusi ya Ukraine ilithibitisha uvumi huu kwa kuchapisha picha ya "Banderola" na maelezo ya vipengele vyake Mei 12.

Ni kombora hatari

Kwa mwonekano na sifa, inafanana na ndege zisizo na rubani za Ukraine zinazoitwa "Peklo", "Palyanytsia.” Ni aina ya mseto wa ndege isiyo na rubani na kombora.

Zinaweza kurushwa kutoka ardhini na kutoka kwenye ndege.

Kulingana na ujasusi wa Ukraine, "Banderol" inarushwa kutoka ndege zisizo na rubani za "Orion" (pia inajulikana kama "Inokhodets"), na katika siku zijazo Urusi imepanga kuzirusha kutoka helikopta za Mi-28N.

Hii ni Orion ndege kubwa yenye uzito wa hadi tani 1, urefu wa mita 8 na urefu wa mabawa wa mita 16.3, ambayo inaweza kukaa angani kwa saa 24 na kupaa kwa urefu wa kilomita 7.5.

Chanzo cha BBC Ukraine katika Jeshi la Anga kilithibitisha matumizi ya "Banderola" na Warusi.

Waangalizi wa kijeshi wanasema droni hiyo inaweza kuwa hatari sana. Oleksandr Kovalenko anabainisha kuwa uwezo wa kuiendesha na kasi ya kombora hilo hufanya iwe vigumu kulidungua.

Jarida maalum la Defense Express linaamini kwamba Urusi inajaribu kutengeneza "kombora la bei nafuu" "kwa ajili ya mashambulizi dhidi ya Ukraine."

Urusi haijatoa taarifa kuhusu droni hiyo. Inaonekana silah hii bado ni ya majaribio. Vinginevyo, kungekuwa na taarifa zaidi kuhusu matumizi yake na vitu vilivyoshambuliwa.