Kwa nini CCM imebadili msimamo wake kuhusu Katiba mpya?

Chanzo cha picha, Mpekuzi
Juni 22, 2022 Katibu wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka aliutangazia umma wa watanzania kwamba chama hicho tawala kimekubali mchakato wa katiba mpya uangaliwe kwa maslahi ya taifa.
Shaka amesema katika kikao cha Kamati kuu ya Halmashauri Kuu walichokaa wamekubaliana suala la Katiba mpya liangaliwe kwa maslahi mapana ya Taifa.
‘chama cha mapinduzi tunasisitiza umuhimu wa uwepo wa Katiba mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa na kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa katiba mpya kwa maslahi mapana ya taifa na maendeleo kwa ujumla,’ alisema Shaka.
Hii ni kauli ‘nzito’ na kubwa kwa siasa za Tanzania, ambayo wengi hasa kutoka upande wa upinzani hawakuitarajia, kutokana na mazingira ya siasa yaliyokuwepo kwa miaka 6 iliyopita, tangu utawala wa hayati Rais John Magufuli, ambapo chama hicho kilikuwa na msimamo tofauti, wa kuuweka kando mchakato wa katiba mpya uliokwama tangu mwaka 2014.
Lakini sasa CCM imekubali mchakato kuhuishwa kutokana na maslahi kwa taifa. Swali nini kimeifanya CCM kuja na mtazamo tofauti sasa?
Msimamo wa muda mrefu wa CCM kuhusu Katiba mpya
Hakuna ubishi kwamba CCM ilikua na msimamo wake kuhusu mchakato wa katiba mpya. Licha ya kutamkwa kwenye ilani ya chama hicho ya (2015-2020), lakini mchakato huo uliokwama miaka 8 iliyopita haukuendelezwa.
Rais John magufuli aliyeingia madarakani mwaka 2015, na ambaye alikuwa mwenyekiti wa CCM, aliweka wazi wakati wa utawala wake kwamba hakutakua na mchakato wa katiba mpya.
Ilani na matamko mengi ya viongozi wa CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020 na baada ya uchaguzi yaliashiria wazi kwamba, suala la katiba mpya halikuwa suala la kipaumbele.
Akaingia marakani Rais Samia Suluhu kufuatia kifo cha hayati Rais John Magufuli kilichotokea mwezi Machi 2021. Rais Samia ambaye alikuwa makamu wa rais katika utawala wa Rais Magufuli kuanzia mwaka 2015, yeye kuhusu katiba mpya alisema; ‘ naomba nipeni muda, nisimamishe nchi (kiuchumi), halafu tutashughulikia mengine’.

Chanzo cha picha, Twitter
Msimamo wa kuusubirisha mchakato wa katiba mpya ulionekana pia kupitia matamshi mbalimbali ya wanachama na viongozi wa chama hicho, akiwemo katibu mkuu Daniel Chongolo.
‘mimi nataka uniambie ni wapi umeona wananchi wamebeba mabango wanataka katiba mpya, tuombiane ukweli zaidi ya sisi wanasiasa’, alisema Chongolo mwezi Agosti mwaka jana na kuongeza; na sisi wanasiasa tunataka mambo mawili matatu, la kwanza tunataka tume huru ya uchaguzi, nambie tume huru ya uchaguzi mwananchi inampelekea unga? Inampelekea ugali? Chama kishaeleza msimamo wa chama mimi sirudii’, alisema.
Msimamo huu ulipigiliwa msumari mwezi Machi, 2022 na maoni ya kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini Tanzania ambacho kilipendekeza kwa Rais Samia, kwamba mchakato wa katiba mpya uanze baada ya uchaguzi wa 2025.
Kwa nini CCM imekuja na msimamo tofauti sasa?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Pamoja na msimamo uliokuwa wazi wa CCM kuhusu katiba mpya, mijadala iliendelea na inaendelea kila leo, huku msukumo zaidi ukitoka kwa wanasiasa wa upinzani na wanaharakati, mbali na wafuasi wenye itikadi tofauti na wenye misimamo mbalimbali.
Hakuna shaka kwamba CCM inafahamu umuhimu wa katiba mpya, na ndio maana walikubali kuanzishwa kwa mchakato wake chini ya Rais Kikwete, kulichokuwa kinaleta maoni tofauti kunatokana na mitizamo ya kiutawala.
Rais Magufuli alikuwa na msimamo tofauti, na sasa Rais Samia ana msimamo tofauti, kwa hivyo ni rahisi kuona kubadilika kwa misimamo.
Wadadisi wa kisiasa wanaona kwamba, maridhiano yanayoendelea na mazungumzo ndio msingi wa misimamo kubadilika na misimamo ya chama na watawala. Msimamo wa Rais Samia umeegemea kwenye maridhiano, kushirikiana, hatua iliyorahisisha mazungumzo mbalimbali na wapinzani na hata kuundwa kwa kikosi kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini humo
Mbali na wanasiasa wengine wa vyama mbalimbali vya siasa, Rais Samia alikutana na Tundu Lissu, mgombea urais wa Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, na mwanasiasa aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali, ambaye alinusurika kuuawa kwa risasi mwaka 2017, akiwa Dodoma kwenye shughuli za Bunge.
Amekutana pia na Mwenyekiti wa chama kikuu cha Upinzani, Freeman Mbowe, muda mchache tu baada ya Mbowe kutoka gerezani alikokaa kwa miezi minane kufuatia kesi ya Ugaidi iliyokuwa inamkabili.
‘Mazungumzo ya aina hii, ni msingi wa maridhiano na ni msingi wa kujenga umoja na mshikamano, naamini hili lilikuwa msingi wa CCM kuona umuhimu wa kuzungumza lugha moja na wengine,’ alisema Beatrice Kimaro, Mchambuzi wa siasa Tanzania.
Anachomaanisha mchambuzi huyu, kinaonekana katika maelezo ya Katibu wa itikadi na Uenezi, CCM Shaka aliyegusia suaa la maridhiano ya kisiasa linavyokwenda vizuri.
‘Ni imani yetu kwamba, maridhiano haya mwisho wa siku hayatawahusu wanasiasa tu, lakini hata nyinyi mnaozungukwa na jamii ni sehemu muhimu ya kufanikisha maridhiano haya’, alisema Shaka alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari, Juni 22, 2022 kuhusu yaliyokubalika kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM.

Chanzo cha picha, Twitter
Msimamo wa sasa wa CCM kuhusu katiba mpya, umepokelewaje?
Kuna hisia tofauti, miongoni mwa wananchi, wanasiasa na wanaharakati kuhusu Mchakato wa katiba mpya. Lakini wengi wamesifu msimamo huo, wakisema ni ukomavu na usikivu mkubwa wa kisiasa.
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe yeye alipongeza uamuzi huo wa CCM, akitafsiri majadiliano na maridhiano yameanza kuzaa matunda.
Hemed Salumu, yeye kupitia mtandao wake wa twitter aliunga mkono, akisema CCM imeona suala la haki.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Kwa upande wa Chadema, kupitia Salim Mwalimu, Naibu katibu Mkuu (Zanzibar), kimesema mbali na kukubaliana na CCM kwenye eneo la katiba kwamba lina umuhimu na maslahi mapana ya taifa, watakaa vikao na kutoa tamko kuhusu msimamo huo mpya wa CCM kuhusu Katiba mpya. Salimu alizungumza na Scolar Kisanga.












