Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mkakati wa Urusi baada ya kuongezeka kwa mashambulizi ya kombora huko Kyiv
Mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, umeshambuliwa mara kwa mara kwa makombora na ndege zisizo na rubani katika wiki za hivi karibuni. Mashambulizi mengi hutokea usiku.
Katikati ya jiji, Nataliya Lyashchenko amepoteza hesabu ya mara ambazo sauti za ving'ora, ndege zisizo na rubani na makombora zimemzuia kulala.
Anasimulia kwamba wakati wa shambulio la usiku miale angavu ya makombora katika anga yenye giza ilifanya ionekane "kama kwenye Star Wars."
Uvamizi kama huo unazidi kuwa wa kawaida.
Wataalamu wanaamini kuwa Urusi inabadilisha mbinu zake katika jaribio la kudhoofisha ulinzi wa anga wa Ukraine, lakini pia wanashuku kuwa, kwa kiasi fulani, inawashambulia raia wa Ukraine katika kukabiliana na vikwazo katika vita.
BBC Verify ilichanganua ripoti za vyombo vya habari vya ndani, akaunti za mashahidi, na taarifa za maafisa wa eneo hilo na jeshi la Ukraine ili kujenga picha ya ongezeko la mashambulizi haya ya anga huko Kyiv na kote nchini tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Mnamo Januari, Urusi ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya malengo tofauti nchini Ukraine kwa siku 3 pekee.
Mnamo Mei, idadi hiyo iliongezeka hadi siku 21. Pia kulikuwa na mashambulizi siku mbili za kwanza za Juni.
Mbali na kushadidisha mashambulizi hayo, Urusi inaonekana kubadili malengo yake makuu.
Dara Massicot, mtafiti mkuu wa sera katika Shirika la Rand, anasema lengo la mgomo huo ni kudhoofisha ulinzi wa anga wa Ukraine.
"Hivi sasa tunaona mashambulizi zaidi dhidi ya vituo vingi vya watu, jambo ambalo linaiweka Ukraine katika hali ambayo inalazimika kutumia viingilia kutetea miji yake," anasema.
'Interceptors' ni makombora ya kutoka ardhini hadi angani yanayotumiwa kurusha ndege zisizo na rubani au makombora.
Lakini kunaweza kuwa na sababu nyingine ya kuongezeka kwa mashambulizi, Masscot anasema.
Wakati wa vita hivi, Urusi imetumia makombora kuwaonesha wakazi wake kwamba inafanya jambo fulani, na kwa maana hii, Massicot anapendekeza kwamba mashambulizi ya hivi karibuni pengine ni majibu ya mashambulizi yaliyotokea ndani ya Urusi na kwamba Moscow inahusishwa na Ukraine. .
"Nadhani tunaona mchanganyiko wa zote mbili: kutambua kwamba wanahitaji kudhoofisha ulinzi wa anga wa Ukraine na kukabiliana na baadhi ya vikwazo ambavyo imekumbana nayo," anafafanua.
Mji mkuu, ulioathirika zaidi
Urusi imezidi kuelekeza mashambulizi yake katika mji mkuu, Kyiv.
Mwezi wa Aprili, mashambulizi 2 kati ya 7 ambayo Ukraine ilipokea yalikuwa katika mji mkuu, Mei imekuwa na mashambulizi 17 kati ya 21.
Na hii imesababisha athari ya kisaikolojia kwa wakazi wa jiji hilo.
Polina Karabach anaishi katika vitongoji, takribani kilomita tano au sita kutoka katikati ya Kyiv.
Mnamo Aprili 28, aliamka saa 4 asubuhi akisikia kelele kubwa kutoka nje.
"Nilikuwa na wasiwasi sana kwa sababu chaneli ya habari haikuwa ikifanya kazi kwa hivyo sikuweza kupata maelezo mengi," aliiambia BBC.
Ambacho hakujua wakati huo ni kwamba makombora ya cruise ya Kirusi yalikuwa yakiruka angani, na hatimaye kuharibiwa na ulinzi wa anga wa Ukraine.
Maafisa wa eneo hilo wanasema makombora yote au ndege zisizo na rubani zilizolenga Kyiv zilidunguliwa na kwamba uharibifu wowote unatokana na vifusi vinavyoanguka. Hili halijaweza kuthibitishwa.
Greg Bagwell, rais wa Shirika la Uingereza la Air and Space Power na kamanda wa zamani wa RAF, jeshi la anga la Uingereza, aliiambia BBC kwamba Kyiv inaonekana kuwa lengo la kimkakati zaidi kuliko la kijeshi.
"Kyiv ni kitovu cha serikali. Na hii inalingana na wazo la Urusi kujaribu kuunda hisia ya ushindi. Ni ishara zaidi kuliko athari halisi ya kijeshi," anaelezea.
Kuna pembe chache sana za Kyiv ambazo hazijahisi athari za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora.
Nataliya Lyashchenko aliiambia BBC kuhusu uzoefu wake wakati wa uvamizi huo, hasa ule wa Mei 4.
"Ilianza na ving'ora vya usiku na kisha kama dakika 15-20 baadaye vita vilianza," anasema.
Alikimbilia katika kituo cha treni ya chini ya ardhi umbali mfupi kutoka nyumbani kwake, akiwa amebeba tu pasipoti yake na paka wake.
"Sio mchezo. Ni vita," anasema.
"Tumepoteza kazi, nyumba, afya zetu, tuna changamoto kubwa mbele yetu, baada ya ushindi wetu, itachukua miaka 10 au 20, labda hata zaidi, kupona kiakili. Lakini nadhani tutapona, kwa sababu Waukraine wameonesha dhamira nzuri ya kuishi," anasema Natalia.