Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini shambulio kubwa na la nguvu lililotangazwa na jeshi la Ukraine dhidi ya Urusi halijaanza mpaka sasa?
Na Oleg Chernysh, BBC News Ukraine
Kwa karibu msimu mzima wa masika, raia wa Ukraine waliishi kwa matarajio makubwa kwamba kutafanyika mashambulizi makubwa yaliyotangazwa sana ya Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine. Tarehe maalum za mashambulizi hayo au "vita vya maamuzi" hazikutajwa, lakini uongozi wa kijeshi na kisiasa wa Ukraine ulisisitiza kuwa kila kitu kilikuwa "kimekamilika."
Baada ya mafanikio ya operesheni ya msimu wa vuli wa mwaka jana ya jeshi la Kiukreni katika mikoa ya Kharkiv na Kherson, ulimwengu wote ulisimama kwa kutarajia maendeleo makubwa zaidi.
Urusi na Ukraine zilikabiliana wakati wa msimu wa baridi kwa njia tofauti.
Kremlin ilirushwa makombora katika jaribio la kuharibu miundombinu ya nishati ya Ukraine.
Kyiv, kwa upande wake, ililenga kuimarisha safu za ulinzi, kutoa mafunzo kwa vitengo vipya vya kijeshi, kupata na kukusanya silaha za Magharibi.
Kufikia masika, pande zote mbili zilipaswa kujiandaa kwa "mapambano makali," kama Jenerali Kirill Budanov, mkuu wa Kurugenzi Kuu ya Ujasusi ya Wizara ya Ulinzi ya Ukraine, alivyoyaita.
Tangazo la 'shambulizi kubwa zaidi'
Idara ya Ujasusi (GUR) iligeuka na kuwa kama msemaji mkuu wa mamlaka juu ya tangazo lililotangazwa.
Mwezi Januari na Februari mwaka huu, mkuu wa idara hiyo, Jenerali Budanov, alitangaza "matukio muhimu" yaliyopangwa kwa msimu wa masika, na juu ya hatua za Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine katika kipindi hiki.
Mapema mwezi Machi, aliiambia USA Today kwamba "msimu wa masika utakuwa vita ya maamuzi kati ya Ukraine na Urusi, ambayo itaamua matokeo ya vita."
Kulingana na utabiri wake, ifikapo majira ya joto ya Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine pia vitapaswa kuingia Crimea ambayo ilitekwa na warusi tangu mwaka 2014.
Katikati ya Aprili, mkuu wa ujasusi wa kijeshi, katika mahojiano na waandishi wa habari wa Novoe Vremya, alisisitiza kuwa maandalizi ya shambulio hilo "yanakwenda kama lilivyopangwa."
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal aliiambia The Hill kwamba mashambulizi ya wanajeshi wa Ukraine yanaweza kuanza katika majira ya joto, si masika.
Mwanzo wa msimu wa masika, kulingana na wataalam wa kijeshi, kwa kweli haikuwa wakati mzuri kufanya shambulio kwa ufanisiwa kiwango kikubwa. Mnamo Machi na Aprili, mvua kubwa ilinyesha Mashariki na Kusini mwa Ukraine, ambayo ikawa kikwazo kwa harakati za magari makubwa na mazito ya kivita.
Wachambuzi wengine pia walieleza sababu nyingine ni kucheleweshwa kwa uwasilishaji wa mizinga kutoka Magharibi, mifumo ya ulinzi wa anga na mizinga kwa Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine.
Kwa kuongezea, katikati ya Aprili, kashfa ilizuka nchini Marekani juu ya uvujaji wa taarifa za siri za Pentagon. Faili nyingi zilikuwa na habari kuhusu mwendo wa vita ya Ukraine.
Ingawa taarifa maalum juu ya mwelekeo na wakati wa shambulio la Kiukreni haikufichuliwa, taarifa zilizovuja zilikuwa na habari nyeti kabisa juu ya mafunzo ya brigedi za Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine na silaha za Magharibi.
Pamoja na hayo, mwishoni mwa Aprili, katika mahojiano na RBC-Ukraine, Kirill Budanov alirudia tena kwamba Ukraine "inakaribia vita kali."
"Tupende tusipende, tunakaribia vita muhimu kwa historia ya sasa ya Ukraine. Huu ni ukweli, kila mtu anaelewa hili. Inapoanza ni siri. Lakini kila mtu anaelewa kuwa tunakaribia hii," alisema.
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Oleksiy Reznikov alisema mwishoni mwa mwezi Aprili na mapema Mei kwamba maandalizi ya mashambulizi hayo yamefikia tamati. Wakati huo huo, alihimiza kutoweka matumaini makubwa juu ya matokeo yake.
Rais Volodymyr Zelensky alisisitiza kuwa mashambulizi yataanza wakati Ukraine itapokea silaha zote zilizokubaliwa na washirika. Lakini wiki chache baadaye, Jenerali huyo huyo Budanov alitangaza kwamba Ukraine tayari ilikuwa na "idadi ya chini ya silaha zinazohitajika."
"Hatuwezi kupoteza muda zaidi. Tayari tuna kiwango cha chini kabisa cha silaha na vifaa vingine. Ninachoweza kusema ni kwamba hii [shambulio] litaanza siku za usoni," mkuu wa upelelezi wa kijeshi alisema katika mahojiano na vyombo vya habari vya Japan.
Maoni kuhusu iwapo Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine viko tayari kwa mashambulizi pia yamegawanyika. Mwishoni mwa mwezi wa Aprili, Kamanda Mkuu wa Muungano wa NATO wa Ulaya Jenerali Christopher Cavoli alisema Ukraine ilikuwa katika "nafasi nzuri" kwa shambulio hilo.
Lakini mkuu wa zamani wa kamati ya kijeshi ya NATO, na sasa Rais wa Czech Petr Pavel, aliitaka Kyiv isiharakishe.
"Itakuwa hatari sana kwa Ukraine ikiwa hatua hii ya kukabiliana na mashambulizi itashindwa, kwa sababu hawatakuwa na nafasi nyingine, angalau mwaka huu," Pavel aliiambia Guardian mnamo Mei 7.
Maafisa wa Urusi walijaribu kutozungumzia hadharani kuhusu mjadala wa Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine kutaka kufanya shambulizi la nguvu. Isipokuwa Mkuu wa kundi la Wagner PMC Yevgeny Prigozhin, ambaye alisema kwamba mashambulizi yangeanza kati ya Mei 9 na 15.
Andrey Yusov, msemaji wa GUR, alikataa kutoa maoni yake kwa BBC Ukraine juu ya kwa nini Wanajeshi wa Ukraine hayajaanza mashambulizi katika majira ya masika kama ilivyotangazwa. Alisema Wizara ya Ulinzi inaweza kuzungumza hilo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi Reznikov alisisitiza kwamba mashambulizi hayo yatawezekana zaidi kutekelezeka katika majira ya joto ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kufanikiwa.
Kwanini Mipango imebadilika?
Katika majira ya masika, mpango huo ulipaswa kbadilishwa kutokana na mazingira, mchambuzi wa kijeshi na mwanahistoria Mikhail Zhirokhov aliiambia BBC Ukraine. Ingawa hajaeleza chanzo cha taarifa zake.
Zhirokhov anabainisha kuwa taarifa zilizotolewa hazikutoa matokeo ambayo mamlaka ya Kiukreni yalikuwa yakitegemea.
"Ninaamini kwamba IPSO (taarifa na operesheni ya kisaikolojia) kuhusu mashambulizi yetu zilitangazwa mapema mno. Matokeo yake, matarajio ya jamii yetu na washirika wetu yaligeuka kuwa ya juu na makubwa sana," mtaalamu huyu anaamini hivyo.
Kulingana na Zhirokhov, mpango wa kwanza wa kukera ulikuwa na malengo ya kawaida na kuongeza: "Kupanga upya mpango wa uendeshaji, ikiwa ni pamoja na kufikia matokeo makubwa na kiwango kikubwa, ni mchakato mgumu sana".
Hasa, tunazungumza juu ya usambazaji wa silaha za ziada na mafunzo ya nguvu na njia za ziada.
Sababu nyingine ambayo ilipunguza kasi ya kufanyika kwa shambulio hilo la nguvu ni mashambulizi ya makombora ya Urusi, ambayo yaliendelea karibu kila siku mwezi wa Mei.
Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu anahakikishia kwamba wakati huu vikosi vya Urusi vilifanikiwa kuharibu maghala makubwa ya silaha ya vikosi cha Wanajeshi wa Ukraine huko Khmelnitsky, Ternopil na Nikolaev.
Mamlaka za Ukraine zinakanusha madai haya. Kulingana na wao, miundombinu na biashara za ndani ndizo zilizoathirika kutokana na makombora ya Kirusi.
Hata hivyo video nyingi za mlipuko mkubwa huko Khmelnytsky mnamo Mei 13, zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zinaonyesha kuwa ghala kubwa lililipuka, ambalo linatajwa kuhifadhi mizinga, makombora ya anga au makombora ya kutungua ndege.
Mikhail Zhirokhov anaamini kwamba mashambulizi kwenye maghala yalikuwa yenye ufanisi mkubwa, na jeshi la Kiukreni lilipoteza kiasi kikubwa cha silaha na kurudisha nyuma jitihada zao za kufanya shambulio la nguvu.
Mchambuzi huyu masuala ya kijeshi wa Ukraine, Mikhail Zhirokhov ana hakika kwamba kuna muda mchache sana uliosalia wa kuanza kwa mashambulio ya Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine. Vinginevyo, askari wa Urusi watafanya hivyo, wachukua hatua na kudhiviti na kuwashambulia Ukraine.
"Ikiwa shambulio la Kiukreni halitaanza wiki ijayo - mapema Juni - basi inaweza kuwa mbaya zaidi," mtaalam huyo anaamini.