Israel Gaza: 'Mama yuko wapi? Bibi yuko wapi? Walikwenda wapi?'

Chanzo cha picha, ANADOLU
Na David Gritten
BBC News
"Anaponiuliza kuhusu familia yake siwezi kumjibu. Badala yake, mimi huvuta pumzi na kujaribu kukwepa swali hilo kwa njia ya kitoto kwa kubadilisha mada."
Moein Abu Rezk ndiye jamaa pekee aliyesalia wa mpwa wake, Omar, mwenye umri wa miaka minne, ambaye yuko katika hali mbaya katika hospitali ya Al-Aqsa iliyopo katika eneo la Deir al-Balah, katikati mwa Ukanda wa Gaza.
Omar alilazimika kukatwa mkono wake wa kushoto na kubakia na jeraha kubwa lililo wazi kwenye mguu wake wa kulia, majeraha madogo kwenye kifua na usoni, na taya yake iligeuka kufuatia shambulio la anga la Israel ambalo Moein anasema liliwaua watu 35 wa familia yake, wakiwemo mama yake, baba na bibi (nyanya)yake.
Kufikia sasa, Moein ameamua kutomwambia Omar kuhusu vifo vyao, kwani anahofu itasababisha hali yake kuwa mbaya kabla ya kuhamishwa kwa matibabu kutoka Gaza kupitia Misri, wakiwa na matumaini kuwa mpango wa serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu na shirika la msalaba mwekundu la Emirates utatekelezwa. .
"Anahitaji kuambiwa taarifa hizo kwa njia maalum ili asipatwe na mshtuko au kuingia katika hali ambayo siwezi kuidhibiti," Moein aliambia BBC Arabic.
"Anajua kwamba hajamwona yeyote kati yao, na bado anahisi haja ya kuuliza: 'Mama yuko wapi? Bibi yuko wapi? Walienda wapi?'"
Hata hivyo, haijahakikishiwa kuwa gari la wagonjwa litamsafirisha Omar hadi kwenye mpaka wa Misri kwa sababu ya mapigano makali na mashambulizi makubwa ya mabomu yanayoendelea katika eneo linalojulikana kama Eneo la Kati la Gaza.

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Vikosi vya ardhini vya Israel tayari vimeigawa Gaza katika sehemu mbili, na kuuzingira kikamilifu Mji wa Gaza katika miezi miwili ya kwanza ya vita na Hamas - ambayo Israel, Uingereza na mataifa mengine yenye nguvu ya Magharibi yanaitaja kama kundi la kigaidi.
Vifaru na wanajeshi sasa wanaingia ndani kabisa ya mji wa kusini wa Khan Younis. Barabara kuu kutoka Deir al-Balah imetangazwa kuwa "uwanja wa vita", na kuwaacha watu katika eneo la Kati wakiwa na njia moja tu inayodaiwa kuwa salama ya uokoaji iliyopo kwenye pwani ya Mediterania.
Wapalestina wengi wanaoishi kaskazini mwa Gaza walitafuta hifadhi katika eneo la Kati baada ya jeshi la Israel kuwaamuru kuyahama makazi yao na kuelekea kusini mwa mto Wadi Gaza miezi miwili iliyopita.
Agizo hilo lilikuja mwanzoni mwa vita vilivyochochewa na mashambulizi ya kuvuka mpaka ya wapiganaji wa Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba ambapo watu 1,200 waliuawa na wengine wapatao 240 kuchukuliwa mateka.
Tangu wakati huo, zaidi ya watu 18,200 wameuawa huko Gaza kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas. Omar ni miongoni mwa watu wengine zaidi ya 49,000 walioripotiwa kujeruhiwa hadi sasa.
Jeshi la Israel linasema kuwa vikosi vyake vinafanya kazi kuwaondoa magaidi, kutafuta silaha na kuharibu miundombinu ya magaidi, na kwamba zaidi ya malengo 22,000 yamepigwa tangu kuanza kwa vita.

Chanzo cha picha, OEIN ABU REZK
Moein aliiambia BBC kwamba Omar na familia yake walikuwa wakitembelea nyumba ya nyanya yake katika kambi ya Nuseirat, kaskazini mwa Deir al-Balah, wakati ilipolipuliwa na walikuwa hawapewa onyo la awali na wanajeshi wa Israel kuhusu shambulio hilo.
"Hatujawahi kuona makombora kama hayo hapo awali. Kombora hilo huanguka na kuharibu eneo lote la makazi yaliyopo karibu," anakumbuka.
"Kwa bahati nzuri, nyumba ilikuwa na mwanya ambao [Omar] alianguka. Lakini mkono wake wa kushoto ulijeruhiwa [vibaya sana] kiasi kwamba ilibidi ukatwe mara moja. "[Siku ya Jumamosi], alipoteza takriban lita tatu za damu na hemoglobin ( kiwango cha seli nyekundu za damu kilishuka kutoka 9.5 hadi 7.4, kwa hiyo ilibidi ahamishiwe kwenye chumba cha ili kuongezewa damu ."
Moein alisema hali katika hospitali hiyo ni mbaya kiasi kwamba madaktari hawakuweza kumtafutia kitanda Omar licha ya majeraha yake kuwa makali, hivyo kumlazimu kusubiri kwenye huku madaktari na wauguzi wakimhudumia kadri walivyoweza.
"Vifaa vyote vya matibabu na zana ni vichache kwa kiwango ambacho tunalazimika kushughulika na hali hiyo kwa vitendo zaidi badala ya njia za kiafya za matibabu.
"Hakuna dawa za kutuliza maumivu kwa hivyo inabidi tufanye mzaha na kujaribu kumchekesha ili kumtuliza."
Moein alikubali kuwa njia hii ilifanya kazi kwa muda fulani tu lakini akaongeza: "Hatuna chaguo lingine lolote."
Alisema anatumai kuwa Omar atasafirishwa Alhamisi ijayo hadi kwenye kivuko cha mpaka cha Rafah na Misri na kisha kupelekwa hospitali kwa matibabu maalum.

Chanzo cha picha, NURPHOTO
Lena Shakora, mume wake na watoto watatu wa kiume hadi sasa wamenusurika katika shambulio la bomu la Israel, lakini anasema bado wanaishi "ndoto mbaya".
Walikimbia makazi yao katika wilaya ya Sheikh Radwan katika Mji wa Gaza na kwa sasa wanajihifadhi katika nyumba katika eneo la mashambani nje ya mji wa Deir al-Balah pamoja na jamaa zao.
"Ninaamka kila siku nikikumbuka kwamba tuko vitani [na] watu wana njaa. Ni mateso kuhamishwa kutoka katika nyumba yako na hakuna chakula," Lena aliiambia BBC Idhaa ya Kiarabu Jumapili usiku.
"Mimi na familia yangu tumekaa na watu 40 katika chumba kimoja na madirisha yote [yamelipuliwa]. Kimsingi tumekaa nje... na kuna baridi kali na watu wamefedheheshwa."
Lena anasema watoto wake walikuwa wameumia migongo yao kwa sababu wanabeba maji . Na mbaya zaidi, maji si safi kwa sababu mitambo ya kutibu na pampu hazifanyi kazi kwa kutokana na ukosefu wa mafuta.
Familia pia imekuwa ikilazimika kula chakula kichafu kwa sababu maduka yamebaki tupu na hawajapokea msaada wowote, aliongeza.
"Tumaini letu kuu ni kuwa na unga ili tuweze kuoka, na hata kama hatuwezi kuoka kwenye kuni [safi]."
"Watu huzunguka wakikusanya kuni zozote wanazoweza kupata. Lakini mkate unatoka ukiwa na uchafu kwa sababu umepikwa kwenye kuni kutoka eneo la lililolipuliwa," alielezea.
Umoja wa Mataifa ulisema Jumapili kwamba haukuweza kusambaza misaada nje ya mji wa kusini wa Rafah, kwenye mpaka na Misri, katika siku za hivi karibuni kwa sababu ya uhasama na vizuizi vya shughuli za utoaji wa misaada
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah












