Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ballon d'Or: Karim Benzema ashinda tuzo ya mchezaji bora wa soka duniani kwa mara ya kwanza
Mshambuliaji wa Real Madrid na Ufaransa Karim Benzema ameshinda tuzo ya Ballon d'Or - tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka huu - kwa mara ya kwanza.
Benzema alifunga mabao 44 katika michezo 46 alipoisaidia Real kushinda Ligi ya Mabingwa na La Liga msimu wa 2021-22.
Lionel Messi (saba) na Cristiano Ronaldo (tano) walikuwa wameshinda tuzo hiyo mara 12 kati ya 13 zilizopita.
Sadio Mane wa Bayern Munich, ambaye alikuwa Liverpool msimu wa 2021-22, alikuwa wa pili mbele ya Kevin de Bruyne wa Manchester City.
Alexia Putellas wa Barcelona alihifadhi tuzo ya Ballon d'Or ya Wanawake, iliyotolewa kwa mwanasoka bora wa kike wa 2022.
Mshindi wa England Euro 2022 na mshambuliaji wa Arsenal Beth Mead alikuwa wa pili.
Mabingwa wa Premier League Manchester City, ambao walikuwa na wachezaji sita walioteuliwa kwenye sherehe hizo, walitunukiwa Klabu Bora ya Mwaka mbele ya Liverpool.
Tuzo ya Ballon d'Or hutunukiwa mwanasoka bora wa mwaka, kulingana na utendaji wake katika msimu wa 2021-22.
Mfaransa wa kwanza kushinda tuzo tangu 1998
Sherehe za Jumatatu mjini Paris zilishuhudia dereva wa F1 Mfaransa Esteban Ocon akiwasili katika ukumbi wa Theatre du Chatelet akiwa na kombe la Ballon d'Or katika gari la mbio za langalanga.
Benzema ni Mfaransa wa kwanza kushinda tuzo hiyo ya heshima tangu Zinedine Zidane mwaka 1998. Zidane alikuwa kwenye hafla hiyo kumkabidhi mchezaji huyo tuzo hiyo.
“Tuzo hii iliyo mbele yangu inanifanya nijivunie sana,” alisema Benzema. “Nilipokuwa mdogo, ilikuwa ndoto ya utotoni, sikukata tamaa, lolote linawezekana.
"Kwa kweli ninajivunia safari yangu hapa. Haikuwa rahisi, ilikuwa wakati mgumu kwa familia yangu pia."
Benzema ndiye aliyepewa nafasi kubwa kushinda tuzo ya mwaka huu.
Mabao yake 44 yalijumuisha hat-trick katika dakika 17 za kipindi cha pili dhidi ya Paris Saint-Germain kwenye Ligi ya Mabingwa, na lingine ugenini kwa Chelsea katika mechi ya robo fainali ya kwanza.
Pia alifunga mabao matatu zaidi katika mechi mbili za nusu fainali dhidi ya Manchester City.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34, ambaye amekuwa Real Madrid tangu 2009, anatarajiwa kuwa na jukumu muhimu kwa Ufaransa kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar litakaloanza tarehe 20 Novemba.
Tuzo ya Ballon d'Or inapigiwa kura na wanahabari 100 kutoka kote ulimwenguni.
Mapokezi mazuri kwa Haller
Mshambulizi wa zamani wa Borussia Dortmund na West Ham, Sebastien Haller, ambaye hivi majuzi alifanyiwa matibabu ya uvimbe kwenye tezi dume, alipigiwa makofi na watazamaji alipopanda jukwaani kumpa tuzo ya Yashin Trophy Thibaut Courtois wa Real Madrid kama kipa bora.
Alisson wa Liverpool alikuwa wa pili, huku Ederson wa Manchester City na Edouard Mendy wa Chelsea akiwa wa tatu na wa nne mtawalia. Hugo Lloris wa Tottenham alikuwa wa 10.
Kombe la Kopa, lililotunukiwa mchezaji aliyefanya vizuri zaidi chini ya umri wa miaka 21, lilikwenda kwa kiungo wa Barcelona na Uhispania, Gavi, ambaye alitimiza miaka 18 mnamo Agosti.
Kiungo wa kati wa Borussia Dortmund Jude Bellingham, 19, aliorodheshwa katika nafasi ya nne na mwenzake wa Uingereza naye fowadi wa Arsenal Bukayo Saka, 21, alikuwa wa nane.
Mshambulizi wa Barcelona Robert Lewandowski alishinda Kombe la Gerd Muller lililotunukiwa mshambuliaji bora baada ya kufunga mabao 57 akiwa na Bayern Munich na Poland mnamo 2021-22.
Tuzo ya kwanza ya Socrates, tuzo ya kibinadamu, ilienda kwa Mane kwa kazi yake ya hisani.
Ronaldo mshindi mara tano katika nafasi ya 20
Messi na Ronaldo wametawala tuzo hiyo katika miaka ya hivi karibuni, mbali na mwaka wa 2018 ambapo kiungo wa kati wa Croatia Luka Modric alishinda tuzo hiyo.
Messi alikuwa tayari ameshinda kombe hilo mara nyingi zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote na mafanikio yake ya saba mwaka 2021 yalikuja baada ya kushinda 2009, 2010, 2011, 2012, 2015 na 2019.
Hata hivyo, hakuteuliwa wakati huu baada ya msimu wa kwanza kutofanya vizuri katika klabu ya Paris St-Germain.
Ronaldo wa Manchester United, ambaye alishinda tuzo hiyo mara ya mwisho mwaka wa 2017, aliwekwa katika nafasi ya 20 kati ya wachezaji 30 walioteuliwa, ikiwa ni nafasi ya chini kabisa ya mchezaji huyo wa Ballon d'Or wa Ureno tangu 2005.
Matokeo ya Ballon d'Or
1. Karim Benzema (Real Madrid, France).
2. Sadio Mane (Bayern Munich, Senegal).
3. Kevin de Bruyne (Manchester City, Belgium).
4. Robert Lewandowski (Barcelona, Poland).
5. Mohamed Salah (Liverpool, Egypt).
6. Kylian Mbappe (Paris St-Germain, France).
7. Thibaut Courtois (Real Madrid, Belgium).
8. Vinicius Junior (Real Madrid, Brazil).
9. Luka Modric (Real Madrid, Croatia).
10. Erling Haaland (Manchester City, Norway).
11. Son Heung-min (Tottenham Hotspur, South Korea)
12. Riyad Mahrez (Manchester City, Algeria).
13. Sebastien Haller (Borussia Dortmund, Ivory Coast).
14. Fabinho (Liverpool, Brazil) alikuwa sawa na Rafael Leao (AC Milan, Portugal).
16. Virgil van Dijk (Liverpool, Netherlands).
17. Luis Diaz (Liverpool, Colombia) alikuwa sawa na Dusan Vlahovic (Juventus, Serbia) na Casemiro (Manchester United, Brazil).
20. Cristiano Ronaldo (Manchester United, Portugal).
21. Harry Kane (Tottenham Hotspur, England).
22. Trent Alexander-Arnold (Liverpool, England) alikuwa nafasi sawa na Phil Foden (Manchester City, England) na Bernardo Silva (Manchester City, Portugal).
25. Joao Cancelo (Manchester City, Portugal) alikuwa sawa na Joshua Kimmich (Bayern Munich, Germany), Mike Maignan (AC Milan, France), Antonio Rudiger (Real Madrid, Germany), Darwin Nunez (Liverpool, Uruguay) na Christopher Nkunku (RB Leipzig, France).