Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi mamluki wa Urusi alivyotoroka hadi Norway
Andrey Medvedev alipokuwa akikimbia kuelekea mpaka wa Urusi na Norway, aliweza kusikia sauti ya mbwa wa kushambulia nyuma yake.
Kuwasili kwao kulimaanisha kwamba wanaume waliokuwa wakimwinda walikuwa wakikaribia. Lakini mpaka - na ulimwengu wa Magharibi – vilikuwa karibu.
Miezi miwili mapema, kijana huyo wa miaka 26 alikuwa amejitenga na mamluki wa Urusi, Kundi la Wagner. Alikuwa karibu kuwa askari wao kwa kwanza kuhamia Magharibi.
Baada ya kuanzishwa mnamo 2014, Kundi la Wagner linaendeshwa na mfanyabiashara Yevgeny Prigozhin. Inaaminika kuwa linachukua takriban 10% ya vikosi vya Urusi nchini Ukraine, na limefanya operesheni huko Syria, Libya na Mali.
Kundi hilo, na mbinu zake mara nyingi zisizo za ubinadamu, sasa linajulikana kimataifa. Lakini habari kuhusu jinsi linavyofanya kazi - na jinsi linavyofadhiliwa - imebaki siri. Kutoroka kwa Medvedev kunaweza kuruhusu maofisa wa ujasusi wa Magharibi kulifahamu kundi hilo.
Kwa nini alichagua kuhama kupitia Norway haijulikani. Tundra iliyoganda ambapo Urusi inakutana na Nato ni mojawapo ya maeneo ya mpakani yenye ulinzi mkali zaidi duniani.
Minara ya ulinzi, yenye askari-jeshi, yana taa kali za kutafuta ili kupenya giza la majira ya baridi kali la Aktiki. Timu za pande zote mbili huweka doria za mara kwa mara.
Lakini katika video iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Urusi Gulagu.net, kamanda huyo wa zamani wa Wagner anakumbuka akiipita minara hiyo kisiri. Wakati wote huo, anadai, askari wa Urusi wanaomwinda walikuwa wanakaribia.
Mnamo saa 2 asubuhi kwa saa za ndani siku ya Ijumaa, Medvedev anasema hatimaye alivuka waya wenye miiba unaolinda mpaka wa Norway huku walinzi wa Urusi wakikaribia.
Alipokuwa akipanda, anasema aliweza kusikia mbwa nyuma yake. Na, mwangaza wa minara ya walinzi ulipomumulika, molio mikali wa risasi za urusi ilisikika.
Baada ya kuvuka waya, Medvedev alikimbia kuelekea msitu - msitu wa Norway - kwa matumaini ya kupata mtu wa kumsaidia.
Akiwa anasogea katika pori hilo, Medvedev anasema aliona taa kutoka kwa makazi madogo kwa mbali – karibu umbali wa kilomita mbili. Alikimbia kwenda kwa taa hiyo.
Aliogopa sana kutazama nyuma yake, anasema, aliogopa mbwa wanaomfuata pia walikuwa wamevuka ua.
Aligonga mlango wa kwanza aliofikia. Baada ya kuwasihi wenyeji kwa Kiingereza kisichoeleweka vizuri kuwaita mamlaka, alizuiliwa na walinzi wa mpaka wa Norway.
Safari yake - kutoka kwa askari wa uvamizi wa kikatili wa Urusi kwa Ukraine, hadi usalama wa Magharibi - ilikuwa imefika mwisho.
Kabla ya kuwasili kwake, na kujitenga kutoka Ukraine, Medvedev hakuwa ameishi maisha ya kawaida sana.
Baada ya kutumikia kwa muda mfupi katika jeshi la Urusi - kama takriban vijana wote wenye umri wa miaka 18 wanapaswa - alifungwa kwa muda mfupi karibu 2017, mwanzilishi wa Gulagu.net Vladimir Osechkin aliiambia BBC. Kosa lake halijajulikana, ingawa baadhi ya ripoti zinasema ni wizi.
Lakini uvamizi mkali wa Urusi dhidi ya Ukraine ndio uliobadilisha maisha yake.
Vita vilipokaribia kukwama, na Urusi ilijaribu kujaza mapengo yaliyotokana na kuongezeka kwa majeruhi, Kundi la Wagner lilianza kuajiri kwa wingi.
Medvedev, ambaye huenda alichochewa na matarajio ya mshahara wa kutosha, alitia saini mkataba wa miezi minne tarehe 6 Julai hadi 6 Novemba. Waajiriwa wa Wagner wanaripotiwa kulipwa karibu $10,000 kwa mwezi, zaidi ya mshahara wa kawaida wa Urusi.
Kama mtu aliye na uzoefu wa kijeshi hapo awali, Medvedev aliteuliwa kuwa kamanda wa kitengo katika mkoa wa mashariki wa Donbas.
Bw Osechkin aliambia BBC kwamba Wagner walimpatia Medvedev takriban wanajeshi 30-40 kwa wiki, wengi wao wakiwa wafungwa waliosajiliwa kutoka magereza ya Urusi.
Mengi ya mapigano makali zaidi nchini Ukraine katika kipindi cha miezi sita iliyopita yametokea Donbas, na Wagner wanaaminika kuhusika pakubwa katika vita viwili vya umwagaji damu zaidi - huko Soledar na Bakhmut.
Wakili wa Medvedev nchini Norway, Brynjulf Risnes, aliiambia BBC kwamba Medvedev alishuhudia uhalifu mwingi wa kivita - ikiwa ni pamoja na kuona "wale wanaokataa kupigana wakiuawa" na idara ya usalama ya ndani ya Wagner Group.
Naye Bw Osechkin alisema Medvedev aliamua kuhama Wagner baada ya kushuhudia "mbinu za kigaidi" za kundi hilo.
"Alinipa ushuhuda kuhusu kile alichokiona katika vita," alisema, "na jinsi vikosi maalum vya Wagner Group vinavyowaua Warusi ambao hawataki kupigana dhidi ya Ukraine."
Mnamo Novemba 2022, Medvedev aliambiwa kwamba, licha ya kukamilisha kandarasi yake ya miezi minne, kikundi kiliamua kwa upande mmoja kuongeza huduma yake. Haikuwa wazi kwa muda gani.
"Kwa kifupi alihisi kusalitiwa na alitaka kuondoka haraka iwezekanavyo," Bw Risnes aliambia BBC.
Baada ya kutoroka Ukraine na kurejea Urusi, Medvedev aliingia katika kituo cha kuandikisha waajiri cha Wagner katika jiji la Urusi la St Petersburg ambako alirudisha vitambulisho vyake vya mbwa. Hii ilionekana kuvutia umakini wa kikundi.
"Alipoondoka Wagner Group, afisi ya usalama ya Wagner ilifanya mambo mengi kumtafuta na alikuwa katika hatari ya kufa," Bw Osechkin alisema.
Huku maajenti wa usalama wakimtafuta, Medvedev alilazimika kujificha ili kuepusha aina ya adhabu ya kikatili ambayo aliona kundi hilo likiwawekea watu waliotoroka nchini Ukraine.
Ilikuwa ni wakati huu ambapo alienda kwa Gulagu.net - shirika la haki za binadamu lililo uhamishoni - kwa msaada.
"Alipokuwa katika hatari ya kufa, rafiki yake aliandika barua kwa Gulagu na kwangu, kusaidia kuokoa maisha ya Andrey," aliongeza. "Tulifanya kitu wakati huo kumsaidia kuondoka Urusi."
Baada ya kujaribu kuvuka mara mbili hadi Finland, Medvedev alisafiri hadi kaskazini ya mbali ya Urusi na kuvuka mpaka wa Norway.
Hadithi hiyo ilipoibuka Jumatatu, mkuu wa Wagner Bw Prigozhin alitoa taarifa ya kejeli akidai Medvedev ni raia wa Norway ambaye aliongoza kitengo kisichokuwepo kutoka taifa la Scandinavia.
Picha ya pasi ya kusafiria ya Medvedev iliyosambazwa na BBC ilionyesha kuwa hakika yeye ni raia wa Urusi kutoka kijiji kimoja katika jimbo la kati la Tomsk.
Bw Risnes aliiambia BBC kuwa anaamini kuwa mamluki huyo wa zamani alikuwa amechukua ushahidi wa uhalifu wa kivita hadi Norway, na kwamba ana nia ya kutoa habari zake na makundi yanayochunguza uhalifu wa kivita.
Uzoefu wake, na sehemu yake katika uvamizi wa umwagaji damu wa Urusi, inaweza kusaidia kutoa ufahamu juu ya shughuli za kikundi kote ulimwenguni.
Lakini kwa sasa, Medvedev anaendelea kuzuiliwa katika eneo la Oslo, akisubiri kusikia matokeo ya ombi lake la hifadhi – mbali kabisa na mzozo uliobadilisha maisha yake, na jina lake kugonga vichwa vya habari.