Walibadilishwa baada ya kuzaliwa : Namna wanawake wawili walivyobaini kuwa tofauti na walivyofikiri

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Na Jenny Kleeman

Mtangazaji, The Gift

Familia mbili katika eneo la West Midlands nchini Uingereza zinagojea kulipwa fidia katika tukio la kwanza rasmi kwenye kumbumbu za hospitali, la watoto kubadilishwa baada ya kuzaliwa katika historia ya hospitali za umma (NHS).

Ilichukuliwa kama namna ya kipekee ya shauku ya kutaka kufahamu suala fulani wakati wa majira ya mvua – kakini matokeo ya kushtua ya vipimo vya vinasaba yaliwaazimisha wanawake wawili na familia zao kutathimini upya kuhusu kila kitu walichokifahamu juu yao.

Wakati marafiki wa Tony walipomnunulia vifaa vya kipimo cha DNA akiwa nyumbani wakati wa Kristmas 2021, aliviacha vifaa hivyo jikoni na kuvisahau huko kwa miezi miwili.

Hakuviona tena hadi siku moja mwezi February. Tony alikuwa nyumbani akiwa mpweke kwa sababu hakuweza kwenda kucheza golf sababu ya mvua. Alitema mate katika chombo cha sampuli, na kukitoa mahali pale, na hakukifikiria kwa majuma kadhaa.

Matokeo yalikuja Jumamosi jioni. Tony alikuwa akizungumza na mama yake, kwenye simu, Joan, wakatika ujumbe wa barua pepe ulipoingia.

Kila kitu kilionekana sawa mwanzoni, kila kitu kilionekana kama kilivyotarajiwa. Kipimo kilionesha sehemu huko Ireland ambako familia ya wazazi ilikotokea. Binamu alikuwemo katika mfumo wa familia. Dadada yake alikuwemo pia.

Lakini alipotazama jina la dada yake, halikuwa sahihi. Badala ya Jessica, mtu anayeitwa Claire aliorodheshwa kama ndugu yake kamili (Jessica na Claire si majina yao halisi - wote wamebadilishwa, kulinda utambulisho wa wanawake).

Tony ndiye mkubwa wa watoto wanne wa Joan. Baada ya watoto wa kiume watatu, alitamani binti. Hatimaye alipata matakwa yake Jessica alipozaliwa mwaka 1967.

“Ilikuwa hisia nzuri sana, hatimaye kuwa na msichana,” Joan ananiambia.

Hata hivyo, mara moja alikuwa na wasiwasi aliposikia kwamba kulikuwa na jambo lisilotarajiwa katika matokeo ya DNA ya Tony. Alikuwa, pia, lakini alijaribu kutoonesha. Miaka kumi baada ya kifo cha baba yake, mama wa Tony alikuwa katika miaka yake ya 80 na akiishi peke yake. Hakutaka kumtia wasiwasi.

Asubuhi iliyofuata, alitumia kituo cha ujumbe cha kibinafsi cha kampuni ya kupima DNA kuwasiliana na Claire, mwanamke ambaye ilidai alikuwa dada yake.

"Halo," aliandika. “Naitwa Tony. Nimefanya kipimo hiki cha DNA. Umekuja kama ndugu kamili. Nadhani ni kosa. Je, unaweza kutoa mwangaza wowote kuhusu suala hili?”

Claire alikuwa amepewa chapa sawa ya kipimo cha DNA miaka miwili iliyotangulia, kama zawadi ya siku ya kuzaliwa kutoka kwa mwanawe.

Matokeo yake pia yalikuwa ya kushangaza - hakukuwa na uhusiano wowote na wazazi wake walipozaliwa, na alikuwa na kiungo cha maumbile na binamu wake wa kwanza ambaye hakujua na hakuweza kuelezea.

‘Nilijiona kama mdanganyifu’

Kisha, baadaye 2022, alipokea taarifa - kaka yake kamili alikuwa amejiunga na familia yake.

Ilikuwa taarifa ya kutatanisha. Lakini kwa njia moja, ilikuwa na maana. Alipokuwa akikua, Claire hakuwahi kuhisi kama mtu wa famili hiyo.

“Nilijihisi kuwa mdanganyifu,” asema. "Hakukuwa na kufanana, kwa sura au tabia," ananiambia. "Nilifikiri, 'ndiyo - nimeasiliwa."

Katika mfululizo wa kwanza wa The Gift, Jenny Kleeman aliangalia ukweli wa ajabu ambao unaweza kufichuliwa wakati watu wanafanya vipimo vya DNA nyumbani kama vile Ancestry na 23andMe.

Kwa mfululizo wa pili, Jenny anaingia ndani zaidi katika matokeo yasiyotarajiwa - mitetemeko ya baadaye - iliyowekwa wakati watu wanaunganishwa kwenye kanzidata kubwa ya kimataifa ya DNA.

Wakati Clare na Tony walipoanza kubadilishana ujumbe na maelezo yasiyoepukika yalianzan kujitokeza – wawili hao watoto wa kike walikuwa wamebadilishwa wakati wa kuzaliwa, miaka 55 iliyopita, na walikuwa wamelelewa na kukua katika familia mbili tofauti.

Ukweli ni kuwa matukio ya watoto waliobadilishwa kwa bahati mbaya kwenye wodi za uzazi hazisikiki ndani ya Uingereza. Katika kujibu maombi ya ya uhuru wa kupata taarifa ya mwaka 2017, NHS ilisema kwamba kwa mujibu wa kumbukumbu zake hapakuwepo tukio la watoto kupelekewa nyumbani kwa wazazi tofauti na wale haliasi.

Tangu miaka ya 1980 watoto wachanga wana pewa utambulishi maarufu kama radio frequency identification (RFID) tags mara tu baada ya kuzaliwa, ambao unaowezesha kufuatiliwa nakufahamika mahali walipo. Kabla ya hapo, wodi za uzazi zilitegemea utambulisho wa kuandikwa kwa mkono.

Kadiri walivyojaribu kupuuza Habari hii, iliwabidi Claire na Tony kuamua jambo la kufanya.

“Mawimbi yatokanayo na hili yatakuwa makubwa”, Tony alimwandikia Claire. “ Iwapo unataka kuliachia hapa, basi nitakubaliana nawe, na hatutasonga nalo mbele kabisa.”

Bla kusita, Claire alifahamu kuwa alihitaji kukutana na Tony na mama yao mzazi.

“Nilihitaji kuwaona, kukutana nao, kuzungumza nao na kuwakumbatia,” alisema.

Tony alipomwambia Joan kuhusu matokeo ya kipimo cha DNA, alishtushwa na majibu. Hili jambo liliwezekanaje?

Usiku wa barafu mwaka 1967

Kumbukumbu za Joan za usiku ambao binti yake alizaliwa ni wazi. Alikuwa ajifungulie nyumbani, lakini kwa sababu alikuwa na shinikizo la damu, aliongezewa uchungu katika hospitali ya West Midlands.

“Walinikaribisha siku ya Jumapili,” alisema. "Kulikuwa na theluji siku hiyo."

Mtoto alizaliwa karibu 22:20. Joan alimshikilia binti yake aliyemtamani sana kwa dakika chache tu - anakumbuka akitazama uso mwekundu wa mtoto mchanga.

Kisha mtoto alipelekwa kwenye chumba cha watoto kwa usiku ule ili mama yake apumzike. Hii ilikuwa jambo la kawaida katika miaka ya 1960.

Saa chache baadaye, baada ya saa sita usiku, Jessica alizaliwa katika hospitali hiyo hiyo.

Asubuhi iliyofuata, Joan alikabidhiwa Jessica badala ya binti yake wa kumzaa, Claire.

Mtoto huyu alikuwa na nywele tofauti na familia nyingine, ambao wote walikuwa na nywele nyeusi - lakini Joan hakufikiria chochote. Kulikuwa na shangazi na binamu wenye rangi zinazofanana.

Mume wake alipofika hospitali kukutana na mtoto Jessica, walikuwa wamefurahishwa sana na ujio wao mpya na kuwa na shaka yoyote.

Miaka 55 baadaye, Joan alitamani sana kujua Claire alikuwa na maisha ya aina gani. Je, alikuwa na furaha?

Lakini kabla ya kupata majibu, ilibidi yeye na Tony wamwambie Jessica habari hiyo, ambaye alikuwa ameishi maisha yake yote akiamini Joan ndiye mama yake, na Tony alikuwa kaka yake.

Tony na Joan walisafiri hadi nyumbani kwa Jessica ili kumwambia ana kwa ana. Joan anasema alimhakikishia kuwa daima watakuwa mama na binti, lakini tangu wakati huo, anasema uhusiano wao haujawa sawa. Jessica hakutaka kuhojiwa kuhusiana na hadithi hii.

‘Nilihisi ni sawa tu’

Siku moja baadaye - na siku tano tu baada ya Tony kupata matokeo yake ya DNA - Claire alisafiri umbali mfupi kati ya nyumba yake na ya Joan.

Kwa miaka mingi, alikuwa akiendesha gari katika kijiji cha Joan akienda na kurudi kazini, bila kujua kwamba huko ndiko mama yake mzazi aliishi.

Tony alikuwa akimsubiri barabarani. "Halo dada," alisema. “Njoo ukutane na mama.”

Claire anasema tangu alipomwona Joan, ilionekana kana kwamba walikuwa wakifahamiana siku zote: “Nilimtazama, na kusema, ‘Mungu wangu, nina macho yako! Tuna macho sawa. Ee Mungu wangu, ninafanana na mtu fulani!’”

"Nilihisi sawa," Joan asema. "Nilifikiria, alionekana kama nilivyokuwa katika siku zangu za ujana."

Walitumia mchana kuchungulia picha za familia. Claire aliwaambia Tony na Joan kuhusu mpenzi wake, watoto wake na wajukuu. Walimweleza yote kuhusu baba mzazi ambaye hatawahi kukutana naye.

Lakini swali lilipohusu iwapo alikuwa na maisha ya utotoni yenye furaha, Claire alikwepa.

"Nisingeweza kusema ukweli wakati huo," anasema. “Wazazi wangu walitengana nilipokuwa mdogo sana. Sikumbuki wakiwa pamoja. Nililelewa katika umaskini mtupu, ukosefu wa makazi, mara nyingi nilikuwa na njaa, na yote hayo yanahusu. Ulikuwa utoto mgumu sana.”

Claire anasema kumjulisha mama aliyemlea lilikuwa jambo gumu zaidi ambalo amewahi kufanya.

Anasema alijitahidi kuwahakikishia wazazi wote wawili aliokua nao, kwamba hakuna kitakachobadilika katika uhusiano wao. Mama yake alifariki mapema mwaka huu.

Pamoja na kukubaliana na utambulisho mpya wa maumbile, kulikuwa na athari za vitendo kwa Claire, pia. Kwa sababu alikuwa amezaliwa kabla ya saa sita usiku, aligundua kwamba alikuwa na umri wa siku moja kuliko vile alivyofikiria hapo awali: "Cheti changu cha kuzaliwa si sahihi, pasipoti yangu, leseni yangu ya kuendesha gari - kila kitu si sawa."

‘Kosa la kutisha’

Majuma machache baada ya kufanya ugunduzi huo, Tony aliiandikia taasisi ya NHS trust ambayo inasimamia hospitali ambayo Claire na Jessica walibadilishwa, akielezea kile vipimo vya DNA vya nyumbani vilivyobaini.

Taasisi hiyo ilikubali makosa hayo - ingawa miaka miwili na nusu baadaye, kiwango cha fidia bado hakijakubaliwa. Tony na Joan wanasema waliambiwa ingekamilika mwaka jana.

Tuliwasiliana na NHS Resolution ambayo inashughulikia malalamiko dhidi ya NHS. Ilisema ubadilishaji wa watoto ulikuwa "kosa la kutisha" ambalo ilikuwa imelikubali kisheria.

Hata hivyo, ilisema kwamba ilikuwa "kesi ya kipekee na ngumu" na kwamba ilikuwa bado inafanya kazi ili kukubaliana juu ya kiasi cha fidia ambacho kingelipwa.

Claire na Joan wamekuwa wakigundua ni kiasi gani wanachofanana, kama vile ladha yao ya nguo na chakula, na jinsi wanavyotumia chai yao. Wamekuwa likizoni, wakichunguza mizizi yao ya kibayolojia huko Ireland, na walikwa Pamoja wakati wa Krismasi iliyopita.

“Tuko karibu sana,” Claire asema kuhusu familia yake mpya iliyogunduliwa. “Ningependa kutumia wakati mwingi kadiri niwezavyo pamoja nao, bila shaka, lakini wakati huo umepita. Imechukuliwa.”

Wakati Claire sasa anamwita “Mama”, Joan ananiambia kwamba Jessica hafanyi hivyo tena. Lakini Joan anahisi tu kwamba amepata binti mwingine.

“Haileti tofauti yoyote kwangu kwamba Jessica si binti yangu wa kumzaa,” anasema. "Yeye bado ni binti yangu na atakuwa daima."

Imetafsiriwa na Florian Kaijage