Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Oleksandr Syrskyi: Sifa tano kuhusu kamanda mpya wa jeshi la Ukraine
Siku chache zilizopita, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alimfuta kazi kamanda mkuu wa jeshi la nchi hiyo Valerii Zaluzhnyi.
Hatua hiyo ilikuja baada ya uvumi kuhusu mpasuko kati ya rais na Jenerali Zaluzhnyi, ambaye ameongoza mapambano ya Ukraine dhidi ya Urusi tangu mzozo huo uanze.
Jenerali Oleksandr Syrskyi alitangazwa kuchukua nafasi yake. Ni mabadiliko makubwa zaidi kwa uongozi wa kijeshi wa Ukraine tangu uvamizi wa Urusi uanze Februari 2022.
Rais alisema yeye na Jenerali Zaluzhnyi walikuwa na "mazungumzo ya wazi" kuhusu mabadiliko yanayohitajika katika jeshi, na alimshukuru jenerali kwa kuilinda Ukraine dhidi ya Urusi.
Kanali-Jenerali Oleksandr Syrskyi, ameongoza vikosi vya ardhini vya Ukraine tangu 2019, alipandishwa cheo na kuwa kamanda wa vikosi vya jeshi siku ya Alhamisi wakati vita na Urusi vikikaribia mwaka wake wa tatu.
Anachukua nafasi ya Valeriy Zaluzhnyi .
Miaka ya Mwanzo
Alexander Syrsky alizaliwa 1965 katika kijiji cha Novinki, mkoa wa Vladimir wakati huo ulikuwa sehemu ya Muungano wa Sovieti. Ameishi Ukraine tangu miaka ya 1980.
Kama walivyo wanajeshi wengi wa rika lake katika vikosi vya jeshi la Ukraine, alisoma Moscow - katika Shule ya Higher Military Command. Alihitimu 1986 na kutumikia Kikosi cha Wanajeshi wa Soviet kwa miaka mitano.
Baba yake alikuwa mwanajeshi, naye alifuata nyayo zake tangu utoto. Katika miaka ya 70, baba yake Syrsky alihamishiwa Ukraine, na familia nzima ilihamia naye.
Safari yake Jeshini
Katika miaka ya 80, aliongoza kikosi cha jeshi kilichokuwa huko Lubny, mkoa wa Poltava. Katika miaka ya 90, aliongoza kikosi na jeshi katika mkoa wa Kharkov. Na katika miaka ya 2000, kikosi cha APU 72.
Mnamo 1996, alihitimu katika Chuo cha Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine, na mwaka 2005, alihitimu Chuo cha Kitaifa cha Ulinzi cha Ukraine.
Mwaka 2009, kwa amri ya Rais Viktor Yushchenko, Syrsky alipata cheo cha meja jenerali.
Mwaka 2013, mwaka wa mwisho wa amani kwa Ukraine, Syrsky alikuwa naibu mkuu wa Kamandi Kuu yKituo Kikuu ya vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine.
Katika nafasi hii, alikuwa, alihusika na ushirikiano wa jeshi la Ukraine na NATO na utekelezaji wa mipango katika Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine.
Syrskyi alikua mkuu wa vikosi vya ardhini vya Ukraine mwaka 2019.
Hapo awali aliongoza wanajeshi wa Ukraine wanaopigana na waasi wanaoungwa mkono na Moscow katika mikoa ya mashariki ya Donetsk na Luhansk tangu mwaka 2014.
Ulinzi wa Kyiv
Muda mfupi kabla ya uvamizi wa Urusi kwa Ukraine, Syrsky mwenyewe alipendekeza kwa uongozi wa nchi hiyo kumteua kuwa kamanda wa ulinzi wa Kyiv.
Ili kuilinda Kyiv, Syrsky alipanga safu mbili za ulinzi - moja ndani ya jiji, nyingine katika vitongoji. Aliunda mfumo wa mawasiliano kati ya amri kuu na vikosi vya mashinani.
Wakati huo huo, aliwawezesha maafisa wa mashinani kufanya maamuzi ya haraka ya kimbinu.
Kwa kutambua kwamba wanajeshi wa kawaida huenda wasitoshe kuilinda Kyiv - Syrsky aliamuru kuundwa na kupelekwa vikosi kutoka vituo vya mafunzo na vyuo vikuu vya kijeshi kutoka miji mingine ya Ukraine.
Aliongoza ulinzi uliofanikiwa wa mji mkuu wa Kyiv katika miezi ya mapema. Katika siku za mwisho za Machi, askari wa Urusi waliondoka kutoka mji mkuu wa Ukraine.
Kwa operesheni hii, ambayo ilidumu zaidi ya mwezi mmoja - alipewa tuzo ya shujaa wa Ukraine mwezi April 2022. Tuzo ya heshima kubwa zaidi katika nchi hiyo.
Julai 2022, Syrskyi alipanga na kutekeleza mashambulio yaliyowarudisha nyuma wanajeshi wa Urusi mbali na jiji la Kharkiv na kuchukua tena sehemu za ardhi upande wa mashariki na kusini mashariki.
Bakhmut
Ushindi mkubwa zaidi wa Ukraine katika vita vya sasa dhidi ya Urusi unahusishwa na jina lake; wasifu na uzoefu wa jenerali huyo mwenye umri wa miaka 58 unaendana na uteuzi huu.
Lakini wakosoaji wa uteuzi wake wanasema katika hali ya sasa, uteuzi wowote wa kamanda wa Wanajeshi wa Ukraine hauwezi kubadilisha hali ya sasa kwa kiasi kikubwa katika uwanja wa vita.
Mapema mwaka jana, Syrskyi aliongoza ulinzi wa mji wa mashariki wa Bakhmut, ambapo maelfu ya wanajeshi wa pande zote mbili waliuawa katika moja ya mapigano yaliyomwaga damu nyingi zaidi katika vita hivyo hadi sasa.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kijeshi walihoji iwapo kupigania mji ulioharibiwa kulikuwa na thamani ya watu wengi kuuawa na kujeruhiwa.
Syrskyi alisema ulinzi mkali wa Ukraine huko Bakhmut umeharibu juhudi za jumla za vita vya Urusi kwa kulizuia kundi la mamluki la Wagner.
Motisha kwa Vikosi vyake
Syrskyi anasema kipaumbele chake ni kutoa motisha kwa wanajeshi wake. Mara kwa mara hupigwa picha akiwa katika ukaguzi katika mstari wa mbele wa mapambano.
Ameviambia vyombo vya habari vya Magharibi, yeye hulala masaa manne na nusu tu usiku na hupumzika kwa kwenda mazoezi. Katika mahojiano na gazeti la Uingereza la Guardian, alisema kabla ya vita alikuwa akilala masaa matano usiku, na mwishoni mwa wiki hulala masaa matano na nusu.
"Kamanda wa Vikosi vya Ardhini amethibitisha kwa dhati sifa ya mtu ambaye kukamilisha kazi ni muhimu zaidi kuliko idadi ya maisha inayohitajika," liliandika gazeti la Ukrayinska Pravda.
Alipoulizwa na mwandishi wa habari wa ABC News, Ian Pannell jinsi alivyonuia kumaliza vita, Syrsky alijibu, akitabasamu: “Tumejitolea kuleta amani. Lakini baada ya ushindi wetu."
Alipoulizwa “vita vitaishaje?'
Alijibu, "wakati bendera za Ukraine zikiruka kwenye mipaka yetu na kuirudisha Crimea."
Syrskyi ameoa na ana watoto wawili.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Lizzy Masinga