Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Zircon: Kwanini kombora jipya la Urusi ni hatari na lina uwezo gani?
- Author, Sergey Morfinov
- Nafasi, BBC
- Iliyochapishwa
Shambulio la anga la Urusi dhidi ya Ukraine Februari 7, lililofanya uharibifu wa kuuwa, liliacha swali ikiwa wanajeshi wa Urusi walitumia kombora lao jipya zaidi la Zircon dhidi ya mji mkuu wa Ukraine kwa mara ya kwanza.
Kombora hili lenye kasi, ni mojawapo ya maendeleo ya hivi karibuni katika teknolojia ya roketi ya Urusi.
Tofauti na kombora la Kinzhals, ambalo hurushwa kutoka katika ndege, Zircons lilitengenezwa kwa ajili ya kurushwa kutoka kwenye manowari na nyambizi.
Hadi sasa, hakuna taarifa za kutosha kuhusu makombora haya na sifa zao za kiufundi.
Kombora lenye kasi lapiga Kyiv
Februari 7 majira ya 1:40 asubuhi, chaneli za telegram ziliripoti kuwa kombora linaondoka Crimea na linaelekea Kyiv. Baadaye kidogo, Jeshi la Wanahewa la Ukraine lilithibitisha "kombora lenye kasi kubwa" linaelekea mji mkuu.
Jeshi la Anga halijathibitisha, wala halijakanusha, kwamba lilikuwa kombora la Zircon.
Akijibu swali kutoka BBC, Yuriy Ignat, msemaji wa Vikosi vya Angani vya Ukraine, alijibu kwamba wachunguzi wanachunguza suala hili, na wataweza kufikia hitimisho juu ya aina gani ya kombora lilirushwa kutoka Crimea.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, wanajeshi wa Urusi wamerusha aina mpya za makombora. Wachunguzi walithibitisha Urusi ilirusha makombora ya balestiki ya Korea Kaskazini ya KN-23 huko Kharkov.
Lakini vyanzo rasmi vya Urusi havijatoa maelezo yoyote kuhusu suala hilo.
Zircon ni kombora la aina gani?
3M22 Zircon lilitengenezwa kama kombora lenye kasi kubwa la hypersonic la kupambana na meli. Urusi imepanga kuliweka kombora hilo katika jeshi lake la majini.
Utengenezaji wa makombora haya ulijulikana miaka kadhaa iliyopita, mwaka 2019. Vladimir Putin alidai kwamba Zircon linaweza kushambulia baharini na ardhini kwa umbali wa zaidi ya kilomita 1,000.
Hapo awali, gazeti la serikali Rossiyskaya Gazeta liliandika juu ya kasi ya kombora hili kuwa mara tano hadi sita ya kasi ya sauti. Lakini katika majaribio ya kombora hilo kasi ya ilikuwa mara 8 ya kasi ya sauti.
Kufuati shambulio la hivi karibuni la Kyiv, la kombora hilo kutoka Crimea, kulingana na kituo cha ufuatiliaji cha Monitor, kinasema kombora hilo halijavuka kikomo cha kasi cha hypersonic.
Kadhalika, hakuna uwazi juu ya aina ya makombora ya Zircons. Pamoja na umbali wa kilomita 1,000 uliotangazwa na Putin, vyanzo vingine vya Urusi vilisema ni la kilomita 300-600.
Lakini uwezo wake katika masafa unaweza kubadilika kutokana na kuboreshwa, pia itategemea umbali wa kupaa kwake na hali ya hewa wakati wa kupaa.
Uzito wa kichwa cha kombora lake ni kati ya kilo 300-400. Makombora hayo yalianza kutumika rasmi katika meli za Urusi mwezi Januari 2023. Yalianza kuzalishwa kwa wingi tangu 2022.
Kwa ujumla, Urusi inajaribu kuficha taarifa kuhusu kombora Zircon.
"Hakuna picha za kuaminika za kombora hili kwa umma, ili liweze kuonekana vizuri na vya kutosha," mtaalamu wa mambo ya kijeshi, Ivan Kirichevsky amesema kwenye redio NV.
Picha za Zircons kawaida huchapishwa ama kwa njia ya animesheni au kama video ya uzinduzi kutoka katika meli, na video hizo hupigwa kutoka mbali sana, kiasi cha kutoweza kuona vizuri.
Sasa inajulikana kuwa manowari zinazobeba makombora hayo ni ile ya Admiral Gorshkov na Marshal Shaposhnikov, pamoja na nyambizi ya nyuklia ya Severodvinsk. Lakini zote ni sehemu ya vikosi vya Kaskazini au Pasifiki na ziko mbali na Bahari Nyeusi.
Kwa hivyo, swali limejitokeza ni jinsi gani hasa kombora la Zircon lilirushwa, ikiwa kweli ni kombora hilo.
Mwaka 2022, vyombo vya habari vya Urusi viliripoti juu uundwaji wa tata la kurushia makombora katika eneo la pwani.
Kwa hivyo, kuna uwezekano kwamba Februari 7, Zircon ilirushwa kutoka Crimea kutoka katika tata la Bastion la kurushia kombora la Zircon. Ama lilirushwa kutoka kituo cha Utes, karibu na Sevastopol.
Ni roketi hatari
Waangalizi wa kijeshi wa Urusi huita Zircon "ni la muuaji." Kombora lenye kasi kubwa, linaongozwa, lina ulinzi na haliwezi kutunguliwa.
Lakini kombora lililoanguka huko Kyiv kuna uwezekano lilidunguliwa au kuzimwa na mifumo ya teknolojia. Mifumo ya PATRIOT na SAMP/T ina uwezo wa kuzuia kombora.
Uwezekano mwingine ni kukosekana usahihi ambapo makombora ya kushambulia meli yanakabiliwa nayo yanaporushwa dhidi ya malengo ya ardhini.
Mtaalamu wa masuala ya kijeshi Alexander Kovalenko anaamini, halikuwa kombora la Zircon kwenda Kyiv, lakini ni kombora jingine lakini wakati wa utengenezwaji wake kuna vifaa vya 3M22 vilitumika."
Ikiwa matumizi ya Zircon yatathibitishwa, itakuwa changamoto mpya kwa ulinzi wa anga wa Ukraine, itamaanisha jeshi la Urusi linatumia aina ya pili ya makombora ya hypersonic dhidi ya Ukraine - pamoja na kombora la Daggers.
Kila shambulio la kombora huongeza ubunifu wa watenegenzaji wa Urusi na huwaruhusu kuboresha silaha zao.
"Siku chache zijazo ukweli kuhusu Zircon huko Kyiv utajulikana. Kombora hili lilirushwa kutoka mzinga gani! Ni swali ambalo hata NATO watataka kupata jawabu," anasema Ivan Kirichevsky.